Tatizo letu sisi watu, huwa tunaanzia chini kabisa, tukijua hatuna kitu na hivyo hatuna cha kupoteza. Tunaweka juhudi kubwa sana, tunachukua hatari kubwa kwa sababu tunajua hakuna tunachoweza kupoteza. Juhudi hizo na hatari tunazochukua zinaanza kuzaa matunda. Tunaanza kupata vitu ambavyo hatukuwa navyo hapo awali.
Na hapo ndipo matatizo makubwa sana yanapoanzia kwenye maisha ya wengi. Baada ya mtu kuanza kupata kitu, kinachofuata ni hofu ya kuchukua hatua zaidi, hofu ya kushinda na hofu ya kupoteza kile ambacho mtu anakuwa amekipata mwanzoni.

Mtu anaacha kukazana kuwa bora zaidi na kupiga hatua kubwa zaidi na anaanza kulinda pale alipo, kukazana asianguke, kuchunga asipoteze kile alichonacho tayari.
Hapa ndipo mafanikio ya wengi yanapofika kikomo na wengi wanaanza kuporomoka. Ni sawa na timu ya mpira, ambayo ilianza kwa kushambulia na ikapata magoli halafu ikaacha kushambulia na kuanza kujilinda, ni rahisi zaidi kufungwa kwa mabadiliko hayo.
Unapokazana kubaki pale ambapo mtu upo, unapokazana usipoteze kile ambacho tayari umeshapata, unajizuia kufanikiwa zaidi, unajizuia kupiga hatua zaidi.
Mafanikio makubwa yanakuja pale unapokuwa tayari kuchukua hatua zaidi, pale unapokuwa tayari kupoteza kile ambacho tayari unacho, lakini kwa kujua unaweza kupata kikubwa zaidi.
Mafanikio makubwa zaidi yanakuja pale mtu unapojua kwamba hatua yoyote kubwa uliyopiga mpaka sasa, siyo kubwa kama unavyodhani, siyo kubwa ukilinganisha na makubwa zaidi unayoweza kufanya.
Kukazana kubaki hapo ulipo sasa ni kuchagua kurudi nyuma, kwa sababu hata kama unaona umebaki ulipo, kumbuka dunia inasonga mbele, hivyo wewe unakuwa umebaki nyuma.
SOMA; UKURASA WA 944; Hatua Muhimu Kuchukua Pale Unapozama…
Pia kile ulichonacho sasa, ndiyo kinakuzuia kupata unachotaka. Kama una kikombe kimoja cha kunywea chai, ambacho tayari kimejaa chai ya rangi, lakini pia kuna chai ya maziwa, na wewe unataka chai ya maziwa, huwezi kupata chai ya maziwa kama hutakuwa tayari kupoteza chai ya rangi iliyojaa kwenye kikombe chako.
Maisha yako ndivyo yalivyo rafiki, kuna vitu unakazana navyo sasa, kuna vitu hutaki kuvipoteza na hivyo vinakufanya unashindwa kupiga hatua zaidi.
Kukazana kubali hapo ulipo siyo mkakati wa ukuaji, siyo mkakati wa mafanikio. Ni njia ya kushindwa, njia ya kuanguka na njia ya kurudi nyuma. Usikubali mafanikio kidogo unayopata yawe kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa zaidi.
Mafanikio yoyote unayojisifia umepata mpaka sasa, yasahau kabisa na kuwa kama unaanza upya. Kuwa tayari kupoteza kile ambacho unacho sasa, kama unataka kupata kikubwa zaidi. Na wakati wowote ule kwenye maisha yako, usikazane kubaki pale ulipo wakati huo, badala yake kazana kupiga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog