“Expecting is the greatest impediment to living. In anticipation of tomorrow, it loses today” – Lucius Annaeus Seneca
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIIPOTEZE LEO….
Leo ndiyo leo,
Leo ndiyo siku ya kufanya yale makubwa uliyojiahidi utayafanya.
Leo ndiyo siku ya kuchukua hatua ili kusogea karibu na mafanikio yako.
Na leo ndiyo siku pekee ambayo una uhakika nayo, jana imeshapita ha kesho bado haijafika.
Pamoja na umuhimu huu wa leo, wa siku uliyonayo, bado wengi wanachagua kupoteza siku zao.
Wanafanya hivyo kwa kuweka mategemeo makubwa sana kwenye kesho, badala ya kuitumia leo.
Wanapanga kufanya vitu, lakini inapofika kwenye kuchukua hatua wanasema watafanya kesho.
Na mara zote kesho imekuwa ni janja sana, huwa haifiki, maana ni rahisi kusema kesho.
Unapoianza siku yako leo, orodhesha kila kitu utakachokwenda kufanya leo na muda utakaofanya, kisha fanya.
Anza na yale mambo ambayo ni muhimu kabisa, na fanya hayo mpaka yakamilike.
Usikubali kujiambia kwamba utafanya kesho, au kuwa na matumaini kwamba kesho itakuwa tofauti na leo.
Rafiki, nikukumbushe kwamba kwenye asili hakuna tofauti ya siku,
Ile kwamba leo ni jumatatu na kesho ni jumanne ni kitu tulichotengeneza sisi binadamu kwenye fikra zetu.
Kwa asili jua linachomoza na siku inaanza, jua linatua na siku inaisha, usiku unaanza.
Hivyo kama leo haiwezi kuwa siku nzuri kwako, nikuhakikishie kesho pia haitakuwa siku nzuri kwako.
Kwa sababu siku haziwi nzuri au mbaya zenyewe, siku ni siku, wewe ndiye utakayeifanya siku yako iwe nzuri au mbaya.
Usikubali kuipoteza siku ya leo,
Usikubali siku yako yoyote ipotee,
Badala yake pangilia siku yako vizuri na ishi kwa mipangilio hiyo, chochote kisisogezwe au kusubiri kesho, maana ipo siku hutaiona kesho.
Ukawe na siku bora sana leo rafiki, siku ya kufanya makubwa na kutokuipoteza kwa kutegemea kesho.
#NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha