Rafiki yangu mpendwa,

Hongera sana kwa juma namba 25 ambalo tumekuwa nalo na sasa juma hili limetuacha.

Lakini pamoja na juma kuisha, huwa kuna mambo ambayo tunabaki nayo kuhusu juma au wakati husika.

Kama ulijifunza kwenye juma hili basi utabaki na yale uliyoifunza, na utaweza kuyatumia kufanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Kama kuna hatua ambazo umepiga katika juma hili, kadiri unavyokwenda na kuangalia nyuma, utalikumbuka juma hili kwamba ulipiga hatua fulani, ulianzisha biashara yako, ulianza kufanya unachopenda na kadhalika.

Na kama kuna kitu ulipanga kufanya halafu hukufanya, basi utabaki ukijitua juma hili maisha yako, hasa pale ulichopanga kufanya ni muhimu na kutokana na muda kupita huwezi kukifanya tena.

Nina imani kwenye juma hili tunalomaliza huna majuto na kama utakuwa nayo basi utachukua hatua mara moja ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.

Na katika kujifunza, kabla juma hili halijaisha, nakushirikisha mambo haya matano muhimu, ambayo unapaswa kujifunza kwa kina, kuyatafakari maisha yako na kuona ni namna gani unaweza kuyatumia kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Unapokwenda kulianza juma namba 26 basi unatumia haya uliyojifunza, ili kuhakikisha unapiga hatua zaidi kwenye maisha yako. Na kama mengine yote huwezi kuyaanza mapema, angalau anza namba tano leo hii, na usikubali tena kuendelea kujizuia kufanya makubwa kwa kujiwekea ukomo ambao haupo.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Karibu rafiki yangu kwenye tano hizi za juma, ujifunze na kutafakari kupitia mambo haya matano niliyokukusanyia, uchukue hatua na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUUZA KITU CHOCHOTE KWA MTU YEYOTE.

Kama umesahau nichukue nafasi hii kukukumbusha kwamba kila mmoja wetu ni muuzaji, kila mtu kuna kitu anauza. Na kama hujafika pale unapotaka kufika, kama hujapata unachotaka kupata kwenye maisha yako, basi bila ya shaka shida inaanzia kwenye mauzo. Huenda hujui nini unauza na hujui njia ya kuuza vizuri ili uweze kupata na kufika unakotaka.

Mwandishi na aliyekuwa muuzaji mzuri sana wa magari Joe Girard, ambaye aliingia kwenye kitabu cha maajabu cha dunia, GUINESS, kama muuzaji bora sana kuwahi kutokea hapa duniani, anatushirikisha jinsi gani KILA MTU, ANAWEZA KUUZA CHOCHOTE KWA MTU YEYOTE.

Kwenye kitabu chake cha HOW TO SELL ANYTHING TO ANYBODY, Joe anatushirikisha historia ya maisha yake, tangu akiwa mdogo na mpaka anaingia kwenye uuzaji wa magari. Ni safari ambayo ilikuwa ngumu sana kwake na aliweza kuondoka kwenye magumu na kupata kila anachotaka kwa kuamua kuuza kweli.

Joe anaanza kitabu kwa kutushirikisha utoto wake, ambao haukuwa mzuri sana, kwa sababu baba yake hakuwa anampenda akiwa mtoto, alimpiga sana na kumpa maneno ya kukatisha tamaa, ya kwamba hataweza kufanya chochote kwenye maisha yake. Mpaka anafikisha miaka 35 hakuwa ameweza kufanya chochote kwenye maisha yake, alikuwa ameshajaribu kila aina ya kazi, na kila aina ya biashara lakini bado alikuwa hana maisha ya uhakika.

Akiwa na miaka 35 ndiyo kama aliamshwa usingizini, pale mke wake alipomwambia hakuna chakula cha watoto, na akijiangalia mfukoni hakuwa na hela, na hapo ndipo alipoamua kwamba atauza kitu kuhakikisha watoto wake wanakula.

Kwenye kitabu hichi Joe ametushirikisha mambo muhimu sana ya kuzingatia kwenye uuzaji wa kitu chochote kile na kwa mtu yeyote yule, na hapa nitakushirikisha mambo kumi muhimu unayoweza kufanyia kazi kuhakikisha biashara yako au chochote unachouza kinakuwa na mafanikio makubwa.

  1. Kuna vitu viwili muhimu sana unapaswa kuvipata kwenye mauzo, cha kwanza unapaswa kupata fedha, na cha pili unapaswa kupata urafiki. Sasa watu wengi huangalia cha kwanza, kupata fedha pekee na hivyo huwa tayari kufanya chochote wauze. Ila kama utamuuzia mtu kitu ambacho hakimfai, jua siyo tu umempoteza mteja huyo, bali umepoteza wateja wengine wengi. Unahitaji kutengeneza urafiki na kila mteja wako, kwa kujali hasa hitaji lake na kuhakikisha anarudi kununua kwako na anawaambia wengine kuhusu unachofanya. kama utapata fedha na ukakosa urafiki, hutadumu kwenye biashara kwa muda mrefu.
  2. Unahitaji kutaka kitu, na kukitaka hasa, ili kikusukume kwenye mauzo. Watu wengi huwa hawafanikiwi kwa sababu hawajui nini hasa wanachotaka, au kama wanajua basi wanachotaka ni kidogo sana kiasi kwamba hakiwasukumi. Unahitaji kuwa na kitu kikubwa unachotaka kwenye maisha yako, kiasi kwamba unapata msukumo wa kuuza zaidi kila siku. Kama unachowaza ni kupata tu hela ya kula na kusukuma maisha, ukishaipata utaanza kuwa mzembe na mvivu. Weka malengo makubwa sana na fanya malengo hayo yakusukume kila siku.
  3. Usiwe na mtazamo hasi kuhusu mteja yeyote unayefanya naye biashara. Ipo tabia ya wafanyabiashara kuwa na mitazamo hasi kwa baadhi ya wateja wao. Wanaona wateja fulani ni wasumbufu au hawatosheki. Upo kwenye biashara kwa ajili ya wateja na hivyo unapaswa kuwapenda na kuwa na mtazamo chanya kwa kila mteja unayefanya naye biashara. Kama mteja ameweza kununua kwako, jua amekuamini sana na fedha zake ambazo amezitafuta kwa jasho, hivyo mheshimu na mpe kile ambacho anapaswa kupata.
  4. Sheria ya Girard ya 250. Girard ana sheria yake anayoiita sheria ya 250. Kwenye sheria hii anasema kwamba kwa wastani watu wanaohudhuria shughuli yoyote, iwe ni sherehe, msiba au chochote ni 250. Hivyo basi, kila mtu mmoja anawajua watu 250. Hivyo ukimfanyia ubaya mteja mmoja, jua umejiharibia kwa watu 250 ambao wangeweza kuwa wateja wako. Kama utaharibu kwa mteja mmoja, jua atasema kile kibaya ulichofanya na utakachoshangaa jina lako linaharibika haraka, usisahau kwamba habari mbaya zinasambaa kwa kasi kuliko nzuri. Utakuta watu wanahadithiana kwamba wewe ni mfanyabiashara mbaya wakati hawajawahi hata kufika kwenye biashara yako. hiyo ndiyo nguvu ya mtu mmoja kwenye watu 250. Hivyo usikubali mteja yeyote aondoke kwenye biashara yako hajatosheka na kile alicholipia. Pia ukifanya uzuri kwa mteja mmoja, jua taarifa zako zitafika kwa watu 250.

Naboresha kidogo sheria hii na SHERIA YA 100 YA KOCHA MAKIRITA. Sheria ya 250 ya Girard aliiandika kabla hatujawa na mitandao ya kijamii, ndiyo maana alitumia mihadhara ambayo watu wanakutana, ambapo wastani ni watu 250. Lakini sasa hivi tuna mitandao ya kijamii, na hata kama watu hawajawahi kukutana basi wanawasiliana kila siku. Kwa uzoefu wangu mwenyewe, naweza kusema kwa wastani mtu mmoja anajuana na watu 1000 kwenye mitandao ya kijamii anayotumia. Hivyo jua ukiharibu kwa mteja mmoja, akaeleza kile ambacho hakuridhika nacho kwenye mitandao ya kijamii, basi umepoteza wateja 1000.

  1. Usijiunge na kikundi cha waliokata tamaa. Kwenye kila aina ya biashara na hata kazi, huwa kuna kikundi fulani cha watu ambao wameshakata tamaa. Watu hao hukutana mara kwa mara, labda mwanzo wa siku au mwisho wa siku na kuanza kuambiana jinsi gani mambo ni magumu, hakuna wateja, biashara haziendi na kadhalika. Kama unataka kufanikiwa kwenye mauzo, kaa mbali na kikundi cha aina hiyo. Kwanza usiwe kwenye kikundi cha aina yoyote ile, maana huo muda unautoa wapi? Unapaswa kuwa bize kuwasailiana na wateja wako, na siyo kuliwazana na walioshindwa kwa nini mambo ni magumu.
  2. Usisubiri wateja waje, watafute wateja ndiyo wakutafute. Girard anasema kilichomtofautisha yeye na wauzaji wengine ni kutokusubiri wateja waje, bali yeye kuwatafuta wateja. Kwenye biashara ya kuuza magari, wauzaji huwa wanasubiri mpaka mteja aje kwenye eneo la mauzo kisha kuanza kumshawishi kununua. Girard hakufanya hivyo, badala yake alitafuta kitabu cha namba za simu na kuanza kuwapigia simu watu ambao hata hawajui, akiwauliza kuhusu uhitaji wao wa magari. Kwa njia hii aliweza kuwauzia watu wengi zaidi. Ukishajua nini unauza, na ukawajua wateja wako ni watu wa aina gani, kawafuate kule walipo na siyo kusubiri mpaka waje unakouzia. Wenzako nao wanasubiri wateja waje, ukiwafuata wateja, hata kama ni kwa njia ya simu, utauza zaidi ya wengine.
  3. Ukishamuuzia mteja amekuwa mteja wako wa milele. Girard anatuambia tena jinsi ambavyo tunafanya makosa kwenye mauzo, mtu unamuuzia mteja na ukishachukua hela basi unamsahau kabisa na kuanza kutafuta wateja wengine. Hakuna mteja anayenunua mara moja tu, na hata kama anachonunua ni cha mara moja, vipo vingine ambavyo anaweza kununua kwako. Ukishamuuzia mteja, na hata usipomuuzia, kama tu umeongea naye, basi pata mawasiliano yake, pata namba yake ya simu, pata barua pepe yake na jua wapi anakaa na hata kazi anazofanya. Jua pia kuhusu familia yake kama utaweza na jua tarehe yake ya kuzaliwa. Ukishapata vitu hivyo, endelea kuwasiliana na mteja huyo mara kwa mara. Kumtumia jumbe nzuri, kama za siku ya kuzaliwa na pia kumkumbusha kurudi kama kuna bidhaa mpya imeingia au kuna huduma bora zaidi zinazopatikana. Mteja akishanunua kwako, mfanye kuwa mteja wa kudumu.
  4. Mfanye mteja wako kuwa mwakilishi na wakala wako. Girard anatuambia hakuna rasilimali kubwa kwenye biashara kama mteja ambaye tayari ameshanunua, na kama umezingatia lile jambo la pili, la kujenga urafiki, basi hapo umemaliza kabisa. unapaswa kumfanya mteja huyo kuwa mwakilishi na wakala wa biashara yako, ambaye atawaambia wengine kuhusu huduma nzuri aliyopata na kuwashawishi wenye uhitaji waje kwako pia. Girard anasema alikuwa akishamuuzia mtu gari, anampa kadi zake za biashara na kumwambia kama anajua mtu anayehitaji gari, basi ampe kadi yake ya biashara na nyuma ya kadi aandike jina lake, iwapo mtu huyo ataenda na akanunua gari, basi yeye aliyemfanya akaenda anapata dola 50. Ni fedha ndogo lakini watu wanapenda vya bure, na wengi sana walileta watu.
  5. Uaminifu ni msingi muhimu sana. Yote tuliyojifunza hapa, hayatawezekana kama utakoa kitu kimoja, uaminifu. Unahitaji kuwa na uaminifu wa hali ya juu sana. Wakati mwingine uaminifu wako utakukosesha wateja, hasa pale utakapowaeleza ukweli kwamba kile wanachohitaji hasa wewe huna. Lakini hilo litakusaidia, badala ya kuwadanganya wateja kwamba una wanachotaka, ukawapatia na kisiwafae, watakosa imani na wewe na watawaambia wale watu 250 na 1000 mtandaoni kwamba wasije kununua kwako. Timiza kile unachoahidi na hakikisha unampa mteja kile hasa anachotaka na kitakachomsaidia.
  6. Zana muhimu unazopaswa kuwa nazo na kuzitumia kwenye mauzo. Girard pia ametushirikisha zana zake za mauzo, ambazo anatuambia ni silaha zake za vita. Zana hizo ni simu, sanduku la posta, kalamu, faili lenye taarifa za wateja na kadi za biashara. Hizi ni zana ambazo ukizitumia vizuri utaweza kuuza sana. Na kwa zama tunazoishi sasa, napenda kuziboresha zaidi zana hizi za mauzo, unahitaji kuwa na; 1. Simu 2. Tovuti yenye blog 3. Mfumo wa kutuma email 4. Mfumo wenye taarifa za wateja wako kwenye kompyuta na 5. Kadi ya biashara (business card). Zana hizi unapaswa kuwa nazo, haijalishi unafanya biashara ya aina gani.

Rafiki, najua unauza, iwe unajua au hujui, anza kufanyia kazi mambo haya kumi mara moja, na nakuhakikishia, baada ya muda utaona matunda bora kabisa kwenye biashara yako, au chochote unachouza. Na nikukumbushe tu kwamba, hata kama umeajiriwa, kuna kitu unauza, hasa kama unakutana moja kwa moja na wale wanaotumia unachofanya.

#2 MAKALA YA WIKI; FANYA HIVI ILI DUNIA IKUPE UNACHOTAKA.

Umewahi kuona kuna baadhi ya watu wanapata kila wanachotaka, halafu kuna wengine wanaonekana kama wana kisirani sana, hawapati chochote? Najua pia umeshawahi kusikia kwamba wenye nacho huongezewa na wasio nacho hunyang’anywa hata kidogo walichonacho.

Ukweli ni kwamba, watu waliofanikiwa, wamejifunza kitu kimoja muhimu sana, wamejifunza jinsi ya kuitega dunia iwape chochote ambacho wanataka kupata. Na kwa kuwa wameshajua siri kubwa kuhusu dunia, dunia haiwezi kuwanyima chochote wanachotaka.

Kama na wewe unataka kujua siri hii ya kupata chochote unachotaka kupata, soma makala ya wiki hii na utajua jambo muhimu la kufanya ili uweze kupata kila unachotaka. Makala ya wiki hii ni hii hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuitega Dunia Ikupe Chochote Unachotaka Kwenye Maisha Yako. (https://amkamtanzania.com/2018/06/23/hivi-ndivyo-unavyoweza-kuitega-dunia-ikupe-chochote-unachotaka-kwenye-maisha-yako/)

vitabu softcopy

#3 #TUONGEE PESA;  SEHEMU YA KUANZIA ILI KUKUZA KIPATO CHAKO.

Nani ambaye hapendi fedha zaidi? Nani ambaye hapendi kipato chake kiongezeke zaidi ya alichonacho sasa? Kila mtu anapenda fedha zaidi, lakini wanafiki utawasikia wakisema usiongee sana kuhusu fedha na utajiri, utaonekana ni mtu mwenye tamaa.

Mimi napenda fedha na kila wakati napenda kupata fedha zaidi. Siyo kwa sababu fedha hizo zitanipa furaha, ila kwa sababu nikipata fedha zaidi najua kwamba nimewasaidia wengi zaidi. Kwa sababu fedha ni zao la thamani ninayotoa.

Na pia sipendi kukaa karibu na wale wanaosema mabaya kuhusu fedha, wanaosema fedha ni mbaya, matajiri ni watu wabaya na fedha haileti furaha, hao nakaa nao mbali mno. Sambamba na wale wanaosema fedha ni ngumu na hakuna fedha, hao pia nawaepuka kama ukoma, maana sitaki wachafue akili yangu. Akili ambayo inajua kitu kimoja kuhusu fedha, kwamba fedha ni muhimu na fedha ni matokeo ya thamani ambayo mtu umezalisha.

Rafiki yangu, hichi ndicho nimekuwa nakushirikisha mara kwa mara, nyoosha akili yako na mawazo yako kuhusu fedha. Kama unataka kuongeza kipato chako, sehemu ya kuanzia ni kwenye akili yako, yale mawazo ambayo yanatawala akili yako.

Ukianza kukaa na masikini, ukasikitika nao kwamba hela hakuna, hela zimekuwa ngumu na hela ni mbaya, ukaanza kusikiliza ujinga wanaojazana kwamba matajiri ni watu wabaya na matajiri wamepata fedha zao kwa njia ambazo siyo nzuri, nakuhakikishia utaishia kuwa kama wao.

Nyoosha mawazo yako kuhusu fedha rafiki, jiambie fedha ni nzuri, jiambie unaipenda fedha na jiambie unahitaji kutoa thamani zaidi ili kupata fedha zaidi. Na ukiwasikia watu wanaongea ubaya kuhusu fedha, ondoka mara moja au hamisha mawazo yako na yapeleke kwenye uzuri wa fedha.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KAMA HUTAKI KUKUZA BIASHARA YAKO, USISHIRIKI SEMINA HII.

Rafiki, kwa muda sasa nimekuwa nakushirikisha kuhusu semina ya kukuza biashara nitakayoendesha mwezi julai kupitia KISIMA CHA MAARIFA. Kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, na utakuwa umelipa ada yako kiasi cha kuweza kuwepo kwenye KISIMA CHA MAARIFA mwezi julai, basi una nafasi nzuri ya kushiriki semina hii. Kama ada yako inaisha kabla ya julai, unapaswa kulipa mapema ili usikose nafasi hii ya kipekee sana.

Nataka kuongea zaidi na wale ambao bado hawajajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, hawa ndiyo wapo kwenye hatari kubwa ya kukosa mambo mazuri sana, ambayo hawataweza kuyapata kokote.

Mwezi julai nimekuandalia semina ya kuweza kukuza biashara yako na kuweza kupata faida kwa zaidi ya asilimia 50. Ili ushiriki semina hii unapaswa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA.

Kama unataka kukuza biashara yako rafiki yangu, kama unataka kupiga hatua zaidi ya hapo ulipo sasa, basi neno langu kwako ni moja, JIUNGE NA KISIMA CHA MAARIFA leo hii.

Lakini kama hutaki kukuza biashara yako, kama umeridhika na hapo ulipo sasa, na hutamani kupiga hatua zaidi, hutaki kujijengea uhuru zaidi, basi usijisumbue kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, unaweza kuendelea kubaki hapo ulipo, lakini tafadhali sana, usiwapigie watu kelele na malalamiko yako kwamba mambo ni magumu.

Kama unataka kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe sasa hivi wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717396253 nitakutumia utaratibu wa kujiunga na uchukue hatua mara moja ili uwe ndani ya kundi, na ujihakikishie kushiriki semina hii ya kipekee sana. Fanya sasa, au usifanye na miaka kumi ijayo, utajutia sana hatua ambayo hukuchukua leo.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; NJIA YA KUJUA UKOMO WAKO.

“The only way of finding the limits of the possible is by going beyond them

into the impossible.” – Arthur C. Clarke

Kuna mtu anasoma hapa, ambaye hajawahi kufanya biashara kwenye maisha yake, lakini utamkuta anasema biashara ni ngumu, si mchezo.

Kuna mtu anasoma hapa, hajawahi kufanya kazi masaa 16 kwa siku na siku 7 za wiki lakini atakuambia nimefanya kazi sana na siwezi zaidi.

Kuna mtu anasoma hapa, ambaye hajawahi kusoma kitabu kimoja akakimaliza na kufanyia kazi yale yote ambayo amejifunza, lakini utakuta anasema nimesoma mengi sana lakini hayasaidii.

Rafiki yangu, kabla hujasema chochote hakiwezekani au hakifanyi kazi, jiulize kwanza kama umekifanya kwa zaidi ya ulivyozoea kufanya au wengine walivyozoea kufanya.

Usiniambie una matatizo ya kifedha wakati unafanya kazi kwa miaka kumi, kila siku unaamka asubuhi, unaenda kazini unarudi jioni na kupoteza muda, mwisho wa wiki unapoteza muda kwa mambo yasiyo ya msingi.

Usiniambie kwamba fedha ni ngumu halafu unapata muda wa kuangalia mpira kwa zaidi ya masaa mwili, unapata muda wa kukaa vijiweni na kujadili  maisha ya wengine, unapata muda wa kukaa baa na marafiki mkinywa pombe.

Niambie mambo ni magumu ukiwa umeshafanya zaidi ya wengine wanavyofanya, zaidi ya ulivyozoea kufanya na uwe na ushahidi wa kuonesha hilo, na hapo nitakubaliana na wewe.

Na nina uhakika kama utafanya zaidi ya ulivyozoea, kama utafanya zaidi ya wanavyofanya wengine, hutakuwa hata na muda wa kusema mambo ni magumu, maana utakuwa na mengi ya kufanya na utapata matokeo bora zaidi ya ulivyozoea kupata sasa.

Rafiki yangu, ni yapi katika haya uliyojifunza unakwenda kuyafanyia kazi mara moja kwenye maisha yako? sikushauri hata uchague, chukua kila kitu na anza kukifanyia kazi mara moja, maana kama hujafika unakotaka kufika, huna anasa ya kuchagua.

Juma namba 26, juma la kuugawa mwaka huu 2018 tunalokwenda kuanza likawe juma bora sana kwako rafiki, juma la kuuza zaidi, juma la kunyoosha mawazo yako kuhusu fedha, juma la kuitega dunia ikupe kila unachotaka na juma la kuchukua hatua zaidi ya ulivyozoea kufanya. Naamini juma hili litakwenda kuwa kubwa sana kwako rafiki, na hutoniangusha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji