Rafiki, kwenye kila eneo la maisha yetu, tunaweza kuvipanga vitu kwenye makundi manne.

Bora, nzuri, kawaida na hovyo. Tukitaka tunaweza kuongeza makundi mawili zaidi, bora sana na hovyo kabisa. Lakini napenda tubaki na makundi hayo manne, ili tuweze kupanga vizuri hatua za kuchukua.

Hovyo ni kitu ambacho hakipaswi kufanywa kabisa, kwa sababu siyo tu kinakukosesha unachotaka sasa, bali pia kinakuzuia usipate ambacho ungeweza kupata baadaye. Ukifanya kitu chochote hovyo, unaharibu ambacho ungepata sasa na unaharibu ambacho ungepata baadaye pia. Kuliko ufanye kitu hovyo, ni bora usifanye kabisa, unajiharibia zaidi.

Mambo ya Kawaida

Kawaida ni kiwango ambacho hakina maana kufanya, unaweza kupata unachotaka kwa kufanya kawaida, lakini siyo kama utakavyotaka. Ukifanya kawaida utapata yale yanayobaki baada ya wanaofanya zaidi kupata wanachotaka. Bila kusahau ukifanya kawaida, ni rahisi sana kupata matokeo mabovu. Kawaida ni sawa na hovyo, usifanye chochote kwa ukawaida.

SOMA; UKURASA WA 966; Kitu Pekee Unachomiliki Kwenye Maisha Yako, Unachopaswa Kukitunza Sana…

Nzuri ni kiwango ambacho wengi wanapenda kufanya, na wanaona ni cha juu kwenye ufanyaji. Lakini uzuri nao una changamoto kubwa, ukifanya vizuri unaishia kupata kawaida. Hii ni kwa sababu wengi ambao wamechoshwa na kawaida wanaweza kufanya vizuri. Hivyo ukifanya vizuri, bado unakuwa kwenye ushindani mkali wa wengi wanaojaribu kufanya vizuri.

Bora ndiyo kiwango cha mafanikio, kiwango ambacho wachache sana ndiyo wanaweza kukifikia, kiwango ambacho kinatoa majibu bora au majibu mazuri. Hakuna yeyote anayefanya kwa ubora na akapata matokeo ya kawaida. Hayupo.

Hivyo wewe kama mwanamafanikio, chochote unachojihusisha nacho, lazima kiwe kwenye kiwago cha ubora. Chini ya hapo unapoteza muda wako na hujajitoa kufanikiwa.

Nzuri si nzuri tena, nzuri ni kawaida na kawaida ni hovyo. Bora ndiyo mpango mzima, bora inaweza kuleta nzuri lakini kamwe haitakuwa kawaida.

Nikukumbushe bora inahitaji kujitoa sana, kujitoa kuliko wengine wote wanavyojitoa na zaidi ya ulivyozoea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog