“There just isn’t enough time for everything on our ‘to do’ list — and there never will be. Successful people don’t try to do everything. They learn to focus on the most important tasks and make sure they get done.” — Brian Tracy
Siku mpya,
Siku nzuri na siku ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIKAZANE KUFANYA KILA KITU…
Kitu kimoja kinachowafanya wengi kushindwa kupiga hatua kwenye maisha yao, ni kutaka kufanya kila kitu.
Watu wengi wanapenda kufanya kila kitu na kuwa kila mahali na hawataki kupitwa.
Lakini unapoangalia, unagundua masaa tuliyonayo kwa siku ni 24 pekee. Na hata nguvu zetu binafsi, zina ukomo wake, tunaanza siku tukiwa na nguvu na hamasa kubwa, lakini kadiri siku inakwenda nguvu na hamasa zinapungua.
Hivyo mpango siyo kujaribu kufanya kila kitu, siyo kutaka kuwa kila mahali.
Mpango ni kuwa na kipaumbele, kuchagua yale machache muhimu sana ambayo yanastahili muda wako na nguvu zako.
Ili kuchagua hayo muhimu lazima pia ujue wapi hasa unataka kufika na maisha yako, kipi hasa unachotaka kufanya kwenye haya maisha.
Baada ya hapo linda sana muda wako, usiruhusu muda ukuponyoke kwa kufanya kisicho muhimu.
Kila unapojikuta umeshaanza kufanya kitu, acha kwa dakika moja na jiulize je hichi ninachofanya sasa kinachangia kufika kule ninakotaka kufika?
Unapojikuta umeingia kwenye mitandao ya kijamii au unasoma habari, jiulize je hilo unalofanya linachangia kufikia malengo yako makubwa?
Kama jibu ni hapana unaacha mara moja kufanya, na usijipe maneno ya kujifariji kwamba ni muda mchache tu unatumia.
Rafiki, hujafika kwenye anasa ya kuweza kumudu kupoteza hata dakika yako moja.
Huna muda wa kufanya kila kitum ila una muda wa kufanya yale muhimu zaidi.
Yajue muhimu kwako ni yapi na fanya hayo tu.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya yale ambayo ni muhumu kabisa.
#Fanya #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYoueLife
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha