Kila kitu kina faida na hasara, kila kitu.
Faida ya kuwa na malengo na mipango mikubwa kwenye maisha yako ni kwamba kama hutakata tamaa, utafikia malengo na mipango hiyo na maisha yako yatakuwa bora sana.
Lakini ipo hasara ya kuwa na malengo na mipango mikubwa, ambayo ni kushindwa. Utashindwa kwenye mengi utakayojaribu, hatua nyingi utakazochukua hazitaleta matokeo uliyotegemea kupata. Na kushindwa huku kutakukatisha tamaa, na utafika mahali uone hakuna haja ya kuendelea kujisumbua, bora kuwa kawaida.

Ipo njia moja kubwa ua kutuwezesha kuondokana na hasara hiyo ya kuwa na malengo na mipango mikubwa. Njia hiyo ni kujikubali wewe mwenyewe, kujikubali kwa namna ulivyo kama mtu.
SOMA; UKURASA WA 1073; Darasa La Kushindwa Kwako….
Kujikubali maana yake unajua wewe kama mtu unaweza kufanya nini na huwezi kufanya nini. Na pale unaposhindwa, unaelewa kwamba kushindwa kule hakujakubadili wewe kama mtu. Kwamba kushindwa ni tukio tu, na halina uhusiano na utu wako.
Kwa kujikubali, maana yake huwezi kukata tamaa, kwa jambo lolote lile, hata liwe gumu kiasi gani, hutakata tamaa, maana umejitofautisha wewe na chochote unachofanya.
Anza kujikubali wewe mwenyewe, anza kujikubali wewe kama mtu na jua chochote kikubwa unachotaka kufanya, utashindwa, lakini kushindwa huko hakuhusiani wala kubadili utu wako, bali ni sehemu ya safari.
Endelea kuchukua hatua zaidi kuelekea kwenye mafanikio yako, bila ya kujali unapitia nini.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog