Rafiki yangu mpendwa,

Huwa natumia muda mwingi kukushirikisha yapi muhimu ya kufanya ili uweze kupiga hatua. Lakini nimekuwa sikuambii sana yapi ya kutokufanya, kwa sababu ukitumia muda mwingi kufikiria yapi ya kutokufanya, unaweza ukajikuta unafanya hayo hayo. Si unajua kwamba tunakuwa kile tunachofikiri muda mwingi?

Lakini pamoja na hilo, kuna hatari wengi wanakuwa wameingia, pamoja na kufanya yale mazuri wanayojifunza, kuna mabaya wamekuwa wanafanya ambayo yanawafanya wazidi kurudi nyuma. Hivyo kujifunza yapi ya kutokufanya au yapi ya kuacha kufanya, kunasaidia kuondoa vikwazo kwenye safari yetu ya mafanikio.

Sihitaji kukuambia zaidi kwa nini ni muhimu kila mtu anapaswa kuwa na biashara zama hizi. Labda kama una ajira inayokulipa sana na unayochagua jinsi ya kutumia muda wako utakavyo na huna mikopo, wala hujawahi kulalamika fedha haitoshi. Lakini kama haupo kwenye kundi hilo, ambalo kwa wengi ninaowajua, hata wenye ajira zinazowalipa sana kuna vingi wanakosa, basi unahitaji kuwa kwenye biashara na siyo tu biashara ndogo, bali biashara inayokua kwa kasi na kuweza kununua uhuru wako.

Lakini wapo wengi wameingia kwenye biashara na hawapigi hatua, wapo pale pale miaka yote. Wengine biashara zimeshakufa kabisa na wameshakata tamaa ya kurudi tena kwenye biashara. Wengine wanawaangalia wanaofanya biashara jinsi wanasumbuka na kujiambia bado hawajawa tayari kuingia kwenye biashara.

Na hapa ndipo ninapokuja mimi rafiki yangu, kukupa MAARIFA sahihi na HATUA za kuchukua ili kuweza kuanzisha na kukuza biashara yako na ikuletee mafanikio makubwa sana.

MIMI NI MSHINDI

Mwezi julai mwaka huu 2018 nimekuandalia semina ya kukuza biashara yako kwa kuongeza faida kwa zaidi ya asilimia 50. Usikose kushiriki semina hii, kama kweli umejitoa kwa ajili ya mafanikio. Maelezo zaidi kuhusu semina hii nitakupa mwishoni mwa makala hii, baada ya kuwa nimekushirikisha aina tano za biashara ambazo haziwezi kukua na kumletea mtu mafanikio.

Rafiki yangu, zipo aina nyingi za biashara ambazo haziwezi kukua na kumletea mtu mafanikio. Lakini kwa uzoefu wangu binafsi kupitia watu niliofanya nao kazi kwa kuwakochi kwenye biashara zao, nimegundua aina hizi tano za biashara ni hatari zaidi maana zimewazuia wengi kufanikiwa na biashara nyingi zinazoendeshwa kwa njia hii zimekufa.

Karibu ujue aina hizi tano za biashara, na ni aina za uendeshaji wa biashara ambazo hazileti mafanikio, ili uweze kuziepuka kwenye biashara zako.

MOJA; BIASHARA ZISIZOKUWA NA WATEJA MAALUMU.

Swali; Mteja wa biashara yako ni nani?

Mfanyabiashara; kila mtu ni mteja wa biashara yangu.

Haitachukua muda, biashara ya aina hiyo haitakua na pia itakufa.

Kama biashara haina wateja maalumu, haina kundi la watu ambao inawalenga, haiwezi kufanikiwa. Kwa sababu hakuna kitu kimoja kinachokubalika na kila mtu, hakuna. Ndiyo maana tuna dini nyingi, tuna vyama vingi vya siasa, tuna vinywaji vingi, tuna michezo mingi na kadhalika.

Watu wote hatufanani na hivyo wote hawawezi kutaka kitu cha aina moja.

Unahitaji kujua wateja halisi na maalumu wa biashara yako. Kwamba biashara inawalenga watu wa aina gani. Hii itakuwezesha kuwapatia huduma bora kabisa na pia kujua wapi pa kuwapata wateja hao.

Usiendeshe biashara kama hujachagua wateja gani unaowahudumia, kutaka biashara iwe ya kila mtu ni kuchagua kuua biashara yako.

SOMA; Mambo Matano Ya Kuzingatia Katika Kuendesha Na Kukuza Biashara Kwenye Nyakati Ngumu Kiuchumi.

MBILI; BIASHARA ZISIZO NA MKAKATI WA MASOKO.

Dhumuni kuu la biashara ni kutengeneza wateja, ambao wanaiamini biashara hiyo na wanawaleta wateja wengi zaidi. Bila wateja hakuna biashara, maana chochote unachotoa, unahitaji watu wanunue ndiyo upate faida.

Kama ilivyo kwenye kosa la kwanza hapo juu, kutokuwa na wateja maalumu wa biashara yako, kukosa mkakati wa masoko ni kosa linaloua biashara nyingi.

Watu wengi huendesha biashara kwa mfumo wa wakiona watakuja, na hata mteja anapofika kwenye biashara, wanaamini tayari anajua kila anachotaka na hivyo hawajisumbui kumuuzia zaidi.

Kila biashara inapaswa kuwa na mkakati wa masoko, mkakati ambao unaleta wateja zaidi na wateja wapya kwenye biashara yako. Mkakati ambao unawatumia wateja waliopo kuleta wateja zaidi. Na mkakati ambao unamfanya mteja aje kwenye biashara akiwa amepanga kununua kitu kimoja, anaondoka akiwa amenunua vitu vitatu huku ana furaha kubwa moyoni ya kukutana na wewe.

Kama bado hujajua unawezaje kutengeneza mkakati wa kuendesha biashara yako hivyo, usijali, ndiyo maana nimekuandalia semina ya kukuza biashara kwa kuongeza faida.

TATU; BIASHARA INAYOENDESHWA NA MTU MMOJA.

Kama biashara inaendeshwa na mtu mmoja pekee, au inamtegemea mtu mmoja ndiyo iende, kiasi kwamba kama mtu huyo hayupo basi biashara hiyo haiwezi kuendelea vizuri, biashara hiyo haiwezi kukua.

Na hili halihitaji akili zozote za ziada kuelewa. Maana mtu mmoja ana masaa 24 pekee kwa siku, na nguvu zake zina ukomo hivyo hawezi kufanya kila kitu.

Ili biashara ikue zaidi inahitaji kutumia muda, nguvu na ujuzi wa watu wengine. Pia biashara inapaswa kuwa na mfumo ambao hata kama mtu hayupo, biashara inaweza kujiendesha yenyewe vizuri kabisa.

NNE; BIASHARA AMBAYO FEDHA HAIJULIKANI IKO WAPI.

Kwenye kila dakika, unapaswa kujua fedha yako ya biashara iko wapi. Kama hujui fedha iko wapi, basi chuma ulete ameshakuzidi ujanja. Na unajua chuma ulete kwenye biashara yako ni nani? Ni wewe mwenyewe, kwa uzembe wako na kukosa umakini, unapoteza fedha, lakini kwa kuwa hutaki kujiona mzembe, unatafuta sababu za hivyo kama hiyo ya chuma ulete.

Kama huna mfumo wa kuweka kumbukumbu za fedha kwenye biashara yako, ni swala la muda tu, lakini kwa hakika biashara hiyo itakufa au haitaweza kukua. Kama hujui mzunguko wa fedha kwenye biashara yako ukoje, wewe unanunua na kuuza, kuna siku utaamka asubuhi, kwenye biashara kutakuwa hakuna bidhaa na mfukoni utakuwa huna fedha na utasema hujui fedha zimeenda wapi. Jibu; UMEZIPOTEZA NA KUZITUMIA HOVYO.

Waliosema mali bila daftari hutumika bila habari walikuwa na uzoefu mkubwa, na walikuwa sahihi, usitake kubishana nao, kuwa na daftari na kuwa na mfumo wa kutunza kumbukumbu zote za fedha kwenye biashara yako.

SOMA; Kitu Kimoja Muhimu Unachopaswa Kufanya Kwenye Miaka 10 Ya Mwanzo Ya Biashara Yako Kama Unataka Mafanikio Makubwa.

TANO; BIASHARA ZINAZOANZISHWA BILA YA SABABU KUBWA.

Swali; kwa nini umeanzisha biashara?

Mfanyabiashara; kwa sababu sina kingine cha kufanya, najaribu nione kama naweza kupata kipato kupitia biashara hii.

Hapo ni swala la muda tu, lakini biashara ya aina hiyo haitafika mbali. Kama hakuna sababu kubwa, sababu nzito ya kuanzisha biashara, sababu inayokusukuma hasa, sababu inayokutoa kitandani, sababu inayokufanya uachane na mengine yote yasiyo muhimu, biashara haitafika mbali.

Kwa sababu kuna changamoto nyingi kila biashara inapitia, kama sababu siyo nzito na kubwa, ni rahisi kukatishwa tamaa na changamoto hizi na mtu ukashindwa kuendelea na biashara.

Rafiki yangu, hizo ndizo aina tano za uendeshaji wa biashara ambazo ni hatari sana kwa biashara yoyote ile. Pata muda wa kuitafakari biashara yako na kama kuna chochote kati ya hivyo vitano unafanya, acha mara moja na utaona matunda yake kwenye ukuaji wa biashara yako.

Nilikuahidi kukupa taarifa kuhusu semina yetu ya ukuaji wa biashara, basi maelezo ya semina hii yapo hapo chini, yapitie na chukua hatua leo ili usikose semina hii ya kipekee.

HABARI NJEMA KWA WAFANYABIASHARA WOTE.

Nimeandaa semina ya biashara inayokwenda kwa jina; NJIA TANO ZA KUKUZA BIASHARA YAKO, Ongeza Faida Kwa Zaidi Ya Asilimia 50 Ndani Ya Mwaka Mmoja.

Hii ni semina ambayo kila mfanyabiashara, na hata mfanyabiashara mtarajiwa atajifunza jinsi ya kuongeza faida kwenye biashara yake kwa zaidi ya asilimia 50 ndani ya mwaka mmoja.

Watu wengi wamezoea faida kuwa asilimia 10 na ikizidi sana asilimia 20 kwa mwaka. Kwenye semina hii unakwenda kujifunza mbinu 50 ambazo unakwenda kuzifanyia kazi kwenye biashara yako na faida itaongezeka kwa zaidi ya asilimia 50.

Semina hii utajifunza kwa namna ya kuchukua hatua, hivyo haitakuwa ya kujua tu, bali utakuwa na kila hatua ya kuchukua.

MAELEZO ZAIDI YA SEMINA HII NI KAMA IFUATAVYO;

Katika semina hii muhimu sana kuhusu biashara, tutakwenda kujifunza yafuatayo;

UTANGULIZI; Umuhimu wa biashara na ukuaji wa biashara kwenye zama tunazoishi sasa, maeneo matatu muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako.

NJIA YA KWANZA; WATEJA TARAJIWA, njia 10 za kuwafikia wengi zaidi na biashara yako.

NJIA YA PILI; KIASI CHA WATEJA TARAJIWA WANAOKUWA WATEJA HALISI, njia 10 za kuwashawishi wanaoijua biashara yako kuwa wateja.

NJIA YA TATU; IDADI YA MIAMALA AMBAYO MTEJA MMOJA ANAFANYA, njia 10 za kuongeza idadi ya miamala mteja anayofanya.

NJIA YA NNE; WASTANI WA FEDHA ANAYOLIPA MTEJA, njia 10 za kuongeza wastani wa malipo anayofanya mteja kwenye biashara yako.

NJIA YA TANO; KIASI CHA FAIDA KWENYE KILA UNACHOUZA, njia 10 za kuongeza kiasi cha faida kwenye kila unachouza.

HITIMISHO; KANUNI SAHIHI YA KUTUMIA ILI KUKUZA BIASHARA YAKO KWA KUONGEZA FAIDA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 50 KWA MWAKA.

Njia hizi tano za kukuza biashara zinategemeana, na kama ambavyo tutajifunza kwenye semina hii inayokuja, zote zinafanyika kwa pamoja na siyo kwamba unachagua njia moja na kuacha njia nyingine.

Nikukaribishe sana rafiki yangu kwenye semina hii ya UKUAJI WA BIASHARA YAKO, ni semina ambayo imekuja wakati sahihi kwako kwa sababu kila biashara zina changamoto na kipindi hichi, changamoto zimekuwa nyingi zaidi.

Semina hii itafanyika kwa njia ya mtandao, kupitia kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA. Hivyo unaweza kushiriki semina hii ukiwa popote pale, bila ya kuhitajika kusafiri au kuacha shughuli zako. Unachohitaji kufanya ni kutenga muda kwenye siku yako ya kufuatilia masomo haya na kisha kufanyia kazi.

Semina hii nzuri itafanyika mwezi julai 2018, itafanyika kwa siku saba, kuanzia tarehe 05/07/2018 mpaka tarehe 11/07/2018. Hizi zitakuwa ni siku saba za kujifunza mambo ambayo yataifanya biashara yako iweze kukua kwa kiasi kikubwa sana.

Ili upate nafasi ya kushiriki semina hii unahitaji kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA. Ukishakuwa mwanachama huhitaji kulipa gharama za ziada kushiriki semina hii.

Kama bado hujawa mwanachama, unapaswa kulipa ada ya mwaka ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo kwa sasa ni shilingi elfu hamsini (50,000/=). Hii ni ada ya mwaka mzima, ambayo inakupa nafasi ya kuendelea kujifunza kila siku kwa mwaka mzima tangu ulipolipia.

Ili kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ada, tsh 50,000/= kwa MPESA 0755 953 887 au TIGO PESA/ AIRTEL MONEY 0717 396 253 majina yatakuja AMANI MAKIRITA.

Ukishatuma ada, tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye majina yako kamili na email yako kisha utaunganishwa kwenye kundi la KISIMA CHA MAARIFA na kuendelea kupata mafunzo.

Ili upate nafasi ya kushiriki semina hii, inabidi uwe umejiunga na KISIMA CHA MAARIFA kabla ya tarehe 05/07/2018. Hivyo mwisho kabisa wa kujiunga ili unufaike na semina hii vizuri itakuwa tarehe 03/07/2018

Karibu sana kwenye semina ya UKUAJI WA BIASHARA YAKO, uondoke na vitu vya kwenda kufanyia kazi kwenye biashara yako ili iweze kukua kwa kiasi kikubwa na uweze kufikia malengo makubwa uliyojiwekea kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog