Kuna aina kuu tatu za watu katika mahusiano na utoaji. Na katika aina hizi, kuna moja ambayo watu wanafanikiwa sana wakati nyingine mbili watu wanaishia kuwa kawaida na hata kushindwa kabisa.

Aina ya kwanza ni wachukuaji, hawa ni watu ambao wanataka kupata vitu kutoka kwa wengine. Wanapenda kunufaika wao zaidi kuliko wengine na wapo tayari kuchukua zaidi na zaidi. Watu hawa wana tamaa ya kupata zaidi na hawatosheki, hivyo kuenda mbali zaidi na hata kudhulumu wengine. Watu hawa wanaweza kupata kile wanachotaka, lakini hakidumu kwa muda mrefu na wanakuwa hawana amani na kile walichopata, maana wanajua wamewanyonya wengine.

Aina ya pili ni nipe nikupe. Hawa ni watu ambao wanatoa kama tu watapewa. Watu hawa watatoa sawasawa na wanavyopokea. Hivyo kama hakuna wanachopata, watu hawa hawatoi chochote. Hawa ni watu wanaopima kila wanachofanya na wanataka wapate kwanza kabla hawajatoa. Watu hawa huwa wanapata wanachotaka, lakini kwa ugumu sana. Kwa sababu kuna wakati wanahitajika kutoa kabla hawajapata, lakini wao wanakuwa hawapo tayari kufanya hivyo.

SOMA; UKURASA WA 811; Upo Muda Wa Kutoa, Lakini Haupo Wa Kurudisha…

Aina ya tatu ni watoaji. Hawa ni wale watu ambao wapo tayari kutoa chochote wanachoweza kutoa, bila ya kutegemea kupata chochote. Watu hawa wanatoa zaidi na zaidi kwa sababu wanajua ndiyo kitu sahihi kutoa. Wanapoona kuna eneo lenye uhitaji, na wao wanaweza kufanya kitu, basi wanachukua hatua na kufanya kitu. Watu hawa hujitengenezea jina zuri, sifa na mahusiano bora kabisa. Katika utoaji wao huo, wanajikuta wanapata zaidi na zaidi, kuliko hata walivyotoa.

Katika makundi haya matatu, mwisho wa siku, watoaji ndiyo wanaofikia mafanikio makubwa, na mafanikio yanayodumu. Japo kwa haraka wachukuaji wanaweza kupata wanachotaka, wanaodumu zaidi ni watoaji.

Angalia nini jamii inayokuzunguka inahitaji kisha toa kadiri uwezavyo, ni sawa na kupanda mbegu, baadaye utavuna mpaka utashangaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog