Siku mpya,
Siku nzuri
Na siku ya mafanikio.
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUWA MGUMU KWAKO MWENYEWE…
Moja ya kikwazo kikubwa kwenye mafanikio ya wengi ni ULAINI, watu wamekuwa laini sana kwao wenyewe.
Na tunaishi kwenye dunia ambayo inawashawishi watu kuwa laini.

Ni rahisi mtu kulalamika na kuwalaumu wengine badala ya kukubali yeye ndiye mwenye makosa na kuchukua hayua.
Ni rahisi mtu kusema nitafanya kesho na leo akaipoteza, asiweze hata kusimama na kusema kipi cha maana alichofanya leo mpaka aweze kuahirisha mambo muhimu afanye kesho.
Ni rahisi mtu kuacha kujaribu pale anapokutana na ugumu na kuanza kuidanganya dunia kwamba nimejaribu sana na nimefanya kila kitu lakini haiwezekani.

Kwenye haya maisha, wanaofanikiwa ni wale ambao ni wagumu, ambao ni wagumu kwao wenyewe.
Wale ambao hawajibembelezi, wanauangalia ukweli kama ulivyo na wanaupokea, japo unauma.
Wale ambao hawatafuti sababu ya kuelezea kwa nini hawajafanya, bali wanafanya.
Wale ambao hata baada ya kushindwa, wanafanya tena na tena na tana, mpaka wapate wanachotaka na haijalishi ni muda kiasi gani utawachukua.

Rafiki, hebu jitafakari asubuhi hii, je wewe ni MUGUMU au wewe ni laini?
Kama umekuwa unajipa urahisi, unalalamikia wengine, unaonhea ongea lakini hufanyi, wewe ni laini na siyo tu kwamba hutafanikiwa, bali dunia itakudharau na kukusukuma itakavyo.
Watu laini huwa hawaheshimiwi, kila mtu anawadharau, anajua siyo wafanyaji wa jambo lolote la maana, zaidi ya maneno, sababu na malalamiko.

Lakini kama wewe ni mtu wa kuchukua hatua ngumu, mtu wa kufanya, mtu wa kuendelea hata baada ya kushindwa na mtu usiyetoa sababu bali matokeo, siyo tu kwamba utafanikiwa, bali dunia itakuheshimu na kukupa kile unachotaka.
Dunia na watu wanawaheshimu sana wale ambao ni wagumu, wale ambao ni wafanyaji.

Kuwa mgumu kwako wewe mwenyewe, na dunia itakuheshimu na kukupa kila unachotaka. Na hata wale wanaokuzunguka, watachagua kuwa wagumu au watakimbia na kutoa nafasi kwa wagumu kuwa na wewe.

Uwe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuwa mgumu sana na kufanya na siyo kusema tu na kutoa sababu.
#KuwaMgumu #Fanya #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYoueLife

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha