Kuna makadirio mawili ambayo sisi binadamu hatujawahi kupatia kwa asilimia mia moja kwenye kukadiria. Makadirio hayo ni ya muda na fedha. Muda wowote utakaokadiria kufanya kitu, utahitaji zaidi ya hapo. Na kiasi cha fedha unachokadiria kutumia, utatumia zaidi ya hapo.
Leo nataka tuzungumzie makadirio ya muda, hasa pale unapotaka kufika eneo fulani ndani ya muda fulani.

Kama unajua inakuchukua dakika 10 kufika sehemu unayotaka kufika, na unapaswa kufika muda kamili kwa sababu ya jambo muhimu unalokwenda kushiriki, usisubiri mpaka zibaki dakika 10 ndiyo uanze safari.
Badala yake anza safari dakika 30 kabla ya muda. Hapo utakuwa na nafasi nzuri ya kufika kabla ya muda, na kama lolote litatokea, na mara nyingi yatatokea usiyotegemea yatokee, hutachelewa.
Pia utakuwa na utulivu na amani ya moyo pale unapokutana na ambacho hukutegemea kukutana nacho.
SOMA; UKURASA WA 1187; Kiwango Sahihi Cha Kuchukua Hatua…
Kwa mfano kama umezoea kutumia dakika kumi, na ukaondoka kabla ya dakika 10, halafu ukakutana na foleni kali, utaanza kupata wasiwasi na hofu kubwa kwamba unachelewa. Hilo litakusumbua na hata kama utafika ndani ya muda, akili yako itakuwa haijatulia.
Lakini kama utakuwa umeondoka mapema, hata ukutane na foleni, hutapata wasiwasi kwa sababu unajua tayari upo ndani ya muda. Utafika ukiwa na utulivu mkubwa na kuweza kufanya kile unachotaka kufanya vizuri.
Faida nyingine ya kuondoka mapema kabla ya muda ni unapata muda wa kujiandaa na kile unachokwenda kufanya. Kama ni mkutano unapowahi kabla ya muda, unajiandaa vizuri.
Pia unapowahi kufika mahali, unaweza kutumia muda wa ziada unaopata kwa kujifunza kwa kusoma au kusikiliza vitabu.
Muhimu zaidi; kamwe usichelewe kwenye kitu muhimu kinachowahusisha watu wengine, kama mkutano au usaili, unapochelewa unajijengea picha mbaya kwa wengine, kwamba haupo makini, hujali kile ulichojia au hujui unafanya nini. Hata kama utakuwa na sababu kwamba kulikuwa na foleni, hiyo haisaidii, unapaswa kuwahi kabla ya muda mliopanga kukutana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog