“Don’t you see the plants, the birds, the ants and spiders and bees going about their individual tasks, putting the world in order, as best they can? And you’re not willing to do your job as a human being? Why aren’t you running to do what your nature demands?” – Marcus Aurelius.
Amka mwanamafanikio,
Amka siyo tu kutoka usingizini, bali kutoka kwenye ndoto ambazo hazikupeleki popote.
Unapoipata siku mpya, siku nzuri na ya kipekee kama hii ya leo, ni nafasi nzuri kwako kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wetu wa maisha kwa mwaka huu 2018 ni TATUA, AMUA NA ONGOZA. Kwa pamoja hivi viwili vinatuwezesha kuwa na maisha bora sana.
Asubuhi ya leo tutafakari HATA MTI NA NDEGE VINAKUSHINDA?
Rafiki, kila kiumbe hai ambacho unakiona mbele yako, kina jukumu moja kubwa sana, kuifanya dunia iende sawa.
Mti unafanya kazi kubwa ya kubadili nishaji ya jua kuwa nishati kemikali, ambayo viumbe wengine wanaitumia kama chakula.
Mti unatumia hewa ya ukaa ambayo kwetu ni uchafu na kuzalisha hewa ya oksijeni ambayo kwetu ndiyo maisha.
Kadhalika, ndege utawaona wanaruka angani, lakini wapo kwenye jukumu kubwa la kuhakikisha dunia ipo kwenye mpango wake mzuri.
Ndege atatua mti mmoja kisha kwenda mwingine, kwa kufanya hivyo anasambaza mbegu za miti kwenye maeneo mbalimbali.
Kila kiumne unachokiona, hata mchwa, kipo kwenye harakati za kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi kila siku.
Halafu unakuja wewe, wewe mtu mwenye utashi wa hali ya juu, mwenye uwezo wa kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi.
Halafu hakuna kikubwa unachofanya ili kuiweka dunia kwenye usawa wake, kuifanya dunia iwe sehemu salama ya kuishi.
Pamoja na uwezo mkubwa sana ulionao, unaamua kuutumia kwenye kuhofia utakula nini kesho au utapata wapi hela ya kuendesha maisha yako.
Kweli unachagua kuyatumia maisha yako kwa vitu vidogo kama hivyo?
Eti kuna siku unaamka na kujiambia leo ni mwisho wa wiki, au leo ni siku ya mapumziko, au leo sijisikii vizuri na ukachagua kulala tu!!
Kama miti ingechagua siku fulani kiwa siku ya mafanikio na isifanye kazi yake, dunia nzima tungekufa.
Kama ndege na mchwa wangekuwa wanaamka asubuhi na kusema leo hatujisikii vizuri wacha tulale, dunia isingekuwa hapa ilipo sasa.
Ninachokukumbusha mwanamafanikio, unapoamka asubuhi, na kuanza kujipa sababu kwa nini usiendelee kufanya makubwa, kwa nini leo upumzike, kwa nini leo hujisikii vizuri, angalia nje na tafuta mti uliopo karibu na uangalie.
Angalia namna mti huo umeshaianza siku yake bila ya kujali ni siku gani.
Wasikie ndege wanavyoruka na kulia, wameshaianza siku yao na hawana mjadala.
Na hapo jiulize je unataka kushindwa na viumbe wadogo kama mti na ndege?
Amka na nenda kaitawale dunia, nenda kaifanye dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi, nenda kafanye kile ambacho dunia inapaswa kukujua wewe ndiyo mfanyaji.
Na fanya hivi kila siku, bila ya kujali ni ijumaa, jumapili au jumatatu, bila ya kujali kuna mvua au kuna jua, na bila ya kujali unajisikia au hujisikii.
Unachagua kufanya yako, kwa sababu kila kiumbe anakazana kufanya yake.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kufanya na siyo kutafuta sababu.
#Fanya #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYoueLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa #WashindeWanyama
Rafiki na Kocha Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha