Kuna njia mbili za kusoma makala hii fupi sana,

Njia ya kwanza ni kuweka mawazo yako yote kwenye makala hii, kuondokana na kelele zote, na ukaisoma na kuielewa ndani ya dakika tano na ukatoka na kitu cha kufanyia kazi.

Njia ya pili ni kuisoma makala hii huku akili yako ikiwa imechukuliwa na usumbufu wa aina nyingine, unasoma huku unajibu kila ujumbe unaoingia. Itakuchukua zaidi ya dakika kumi kusoma makala hii fupi na utamaliza ukiwa hujui hata nini umeondoka nacho.

Na unavyosoma makala hii, ndivyo unavyofanya kila kitu kwenye maisha yako. Si unakumbuka usemi kwamba unavyofanya chochote ndivyo unavyofanya kila kitu?

Kile unachochagua kufanya, kile ambacho kipo mbele yako sasa, ndiyo kitu muhimu zaidi kuliko vyote duniani kwa sasa. Na ndiyo maana unakifanya, na kama siyo kweli, kama siyo kitu muhimu kuliko vyote kwenye dunia yako kwa sasa, basi kiache mara moja na fanya kile ambacho ni muhimu zaidi.

Hivyo unapofanya kile kitu ambacho ni muhimu zaidi kwenye maisha yako, weka akili na mawazo yako yote pale, weka nguvu zako zote hapo, weka umakini wako wote hapo, toa kila unachopaswa kutoa katika kufanya hicho ambacho ni muhimu zaidi kwako.

SOMA; UKURASA WA 804; Kama Kila Kitu Ni Kipaumbele, Huna Kipaumbele….

Jitoe kwenye kila aina ya usumbufu unaoingilia ufanyaji wako, jiweke kwenye utulivu wa kipekee kabisa, utulivu ambao unaifanya akili yako itulie kwenye kile unachofanya.

Tumia msimamo huu na utaona ni jinsi gani unahitaji kufanya vitu vichache sana kwenye maisha yako, na pia jinsi gani vitu hivyo vichache siyo vigumu kama ulivyokuwa unafikiri.

Kile kilichopo mbele yako, kile ulichokubali kufanya, ndiyo kitu muhimu kuliko vingine vyote kwenye dunia yako kwa sasa. Kama si hivyo basi inabidi uache kufanya mara moja na uende kwenye kile ambacho ni muhimu zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog