Kama kuna ndoto za alinacha, basi ni ile hali ya watu kuishi hovyo leo wakiamini kesho itakuwa bora sana. Ile hali ya watu kuichukulia poa leo, kutokana na changamoto mbalimbali wanazopitia, wakiamini kesho itakuwa nzuri zaidi.

Sikiliza rafiki yangu, jinsi unavyoichukulia leo, ndivyo utakavyoichukulia kesho. Kwa sababu hata kama changamoto zinazokusumbua leo zitaisha, kesho itakuja na changamoto nyingine mpya kabisa.

Usifikiri kwamba ukishaondokana na changamoto au matatizo uliyonayo sasa ndiyo utaweza kuwa na maisha ya furaha. Maisha ya furaha hayahusiani kwa vyovyote vile na changamoto yoyote unayopitia.

Ifurahie siku ya leo na ifurahie kila siku unayoipata, bila ya kujali ni changamoto zipi unazopitia kwenye siku hiyo.

SOMA; SIKU YA 17; Jinsi Tengeneza Bahati Yako Mwenyewe

Fanya yale unayopenda kufanya na weka hamasa na juhudi kubwa kwenye kufanya hayo unayoyapenda. Kwa njia hii utahamasika zaidi wewe mwenyewe na pia utawahamasisha wale wanaokuzunguka.

Kama unataka kesho yako iwe bora kabisa, basi chagua kuifanya leo iwe siku bora kwako. Kwa sababu siku bora huwa hazitokei, bali huwa zinatengenezwa kwa namna ambavyo mtu unaishi kila siku yako.

Leo ni siku muhimu kwako, siku ya kuweka msingi muhimu kwa ajili ya kesho, chukua hatua leo ili kesho iweze kuwa bora zaidi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog