Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 26 linatuaga sasa na mwaka wetu 2018 tumeshaugawa nusu, nusu moja imekwenda na nusu nyingine ndiyo tunaianza.

Hii ina maana kwamba, yale uliyopanga kufanya mwaka huu 2018 inabidi uwe umeshafika angalau nusu na kuendelea. Na kama kuna ambayo bado hujapiga hatua, kama kuna ambayo hujaanza kabisa, unahitaji kuchukua hatua kubwa zaidi kwenye nusu hii iliyobaki. Unahitaji kufanya mara mbili zaidi ya ulivyokuwa unafanya. Unahitaji kuweka juhudi zaidi na unahitaji kulinda muda wako zaidi. Usipoteze muda wako kama hakuna anayelipia chochote unachofanya.

Hii ina maana kwamba, kama uliyopanga kufanya mwaka huu bado hata hujafika nusu, basi acha kabisa haya yafuatayo. Acha kabisa kuangalia TV, usiangalie kabisa, sijawahi kuangalia TV kwa muda sasa na hakuna chochote nilichokosa. Acha kabisa kutumia kilevi cha aina yoyote ile, acha mara moja, hakuna utakachokosa. Acha kabisa kukaa na watu mnapiga hadithi au kubishana kwa jambo lolote lile, labda kama mwisho wa ubishi huo kuna mtu anawalipa, kama hakuna anayelipa, acha. Acha mara moja kuhudhuria vikao visivyo na msingi, kama hakuna anayekulipa au kama huongezi nafasi yako ya kutengeneza kipato zaidi usiende. Acha mara moja kutumia mitandao yote ya kijamii kama hakuna anayekulipa kwa kufanya hivyo. Acha kulala muda mrefu, lala masaa 6 mpaka 7 na mengine yanayobaki yapeleke kwenye shughuli za uzalishaji.

Ukishaacha kufanya hayo nimekuambia usifanye hapo juu, na mengine yanayofanana na hayo, utakuwa na masaa 14 mpaka 16 ya kutumia kwenye kazi zako za siku. Sasa unachohitaji kufanya, andika ratiba yako ya kila siku na kila lisaa jaza kitu utakachokuwa unafanya. Usikubali kabisa saa yako yoyote iwe huna cha kufanya. Ratiba yako ikiwa wazi utamkaribisha ibilisi na ataanza kukushawishi mambo yasiyo na msingi kwako.

Jaribu hili rafiki yangu, kwa miezi hii sita iliyobaki kwenye mwaka huu, usitumie muda wako kufanya chochote kile ambacho hulipwi. Na tenga muda mfupi wa kupumzika na kuwa na wale wa karibu kwako. Na inapokuwa kazi basi iwe kazi kweli, usichanganye na kingine chochote. Fanya hivi kwa miezi sita tu, halafu uone je utabaki pale ulipo sasa!

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Rafiki, karibu kwenye tano za juma, ambapo nakukusanyia mambo matano muhimu ambayo unapaswa kujifunza na kuyafanyia kazi ili maisha yako yawe bora zaidi.

Kama ambavyo nimekuwa nakukumbusha, na kama ilivyo kanuni kuu inayotuongoza kwenye KISIMA CHA MAARIFA; MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.

Hivyo rafiki, lazima ujue kilicho sahihi, kulingana na unachofanya na unachotaka. Pia kujua pekee hakutoshi, lazima uchukue hatua kubwa sana. Na hapo ndipo utaweza kupata mafanikio makubwa.

Karibu ujifunze haya matano, uondoke na yale ya kwenda kufanyia kazi na uweze kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; NJIA KUMI ZA KUONGEZA FAIDA KWENYE BIASHARA NA KUIBADILI DUNIA.

Moja kati ya vitabu nilivyosoma juma hili ni kitabu MARKETING THAT MATTERS ambapo waandishi Chip Conley na Eric Friedman wanatushirikisha njia kumi za kuongeza faida kwenye biashara na kuibadili dunia.

Waandishi wanatuambia kwamba lengo la biashara siyo tu kutengeneza faida, bali pia kuifanya dunia kuwa sehemu salama zaidi ya kuishi. Na wamekuja na njia ya kuendesha biashara ambayo inaweza kutimiza hayo mawili.

Watu wengi wamekuwa wakifikiria kwamba ukiwa kwenye biashara lazima uwanyonye wengine ndiyo ufanikiwe, lazima uwadanganye watu, uongeze chumvi kwenye mambo ili uwasukume watu wanunue na wewe upate faida.

Huo ni mtazamo wa kizamani ambao kila aliyefanya hivyo hakubaki salama. Ndiyo alipata faida nyingi kwa muda mfupi, lakini biashara hazikudumu kwa muda mrefu.

Hivyo kama unataka biashara yako idumu vizazi na vizazi na iwe sehemu ya kuifanya dunia kuwa bora, kuna mambo kumi muhimu sana ambayo waandishi wametushirikisha tuyazingatie;

  1. Usiogope kuitangaza biashara yako. Masoko ndiyo msingi muhimu wa biashara yoyote ile. Kikwazo namba moja kwenye biashara yako ni wateja kutokujua kuhusu uwepo wako. Hivyo unahitaji kuitangaza biashara yako na kuhakikisha kila mteja inayemfaa anajua uwepo wa biashara hiyo. Na unapotangaza, eleza kile ambacho biashara yako inafanya, yaani wateja wananufaikaje na biashara hiyo. Ili ufanikiwe kwenye biashara, lazima uwe na mkakati mzuri wa kutangaza na kufikia soko la biashara yako.
  2. Jijue wewe mwenyewe. Unahitaji kujijua wewe na kuijua biashara yako kwa kina. Kuwa na maono na kuyaishi maono hayo kwenye biashara yako kila siku. Maono ya biashara yako lazima yawe wazi na yaeleweke na kila anayejihusisha na biashara yako, kuanzia wasaidizi wako mpaka wateja wako. Wateja wanafurahia pale wanapojua kusudi kubwa la biashara na kuona biashara ikiishi kusudi hilo.
  3. Mafanikio kwako yana maana gani? Huwezi kufanikiwa kama hujui mafanikio kwako yana maana gani. Hivyo lazima ujue biashara yako inakazana kufika wapi, ili uweze kupima kadiri muda unavyokwenda na ujue kama unafanikiwa au unarudi nyuma. Mafanikio yako kwenye biashara ni kufikia yale malengo makubwa uliyojiwekea kibiashara.
  4. Jua soko lako na kazana kutoa huduma bora kabisa kwa wateja wako. Ili ufanikiwe kwenye biashara, lazima kwanza ujue wateja hasa wa biashara yako ni watu gani, wanahitaji nini na wanasukumwa na nini. Kuna vitu vitatu muhimu sana unapaswa kujua kuhusu soko lako, kwanza jua saikolojia ya wateja wako, kuwa na bidhaa ambayo inawafaa na kisha kuwa na ujumbe ambao unawafanya wateja wasambaze kwa wengine pia. Unahitaji kutimiza mahitaji ya msingi ya wateja wako, kisha kuwafanya wajisikie wa thamani sana kufanya biashara na wewe.
  5. Usifuate mazoea ya kibiashara, usiweke ukomo kwenye soko lako. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya biashara kwa mazoea, kwa kujiwekea ukomo, kuchagua kuwauzia watu waliozoea kuwauzia, kwa eneo ambalo wamezoea. Ili kufanikiwa, unahitaji kuondokana na mazoea na kuanza kuangalia wateja wapya unaoweza kuwahudumia kwa biashara yako. Kila wakati tafuta masoko mapya ya biashara yako.
  6. Toa thamani na eleza maadili na msimamo wa biashara yako. Wateja wanataka vitu viwili kutoka kwenye biashara yako, kwanza ile thamani ambayo biashara inatoa, na pili maadili na msimamo wa biashara ile. Sasa hivi wafanyabiashara ni wengi, hivyo wateja wanapenda kufanya biashara na wale ambao wanaamini kile wanachoamini wao. Hivyo lazima biashara yako iwe na maadili ambayo inasimamia, iwe inajulikana wazi kwa wateja kwamba hii ni biashara inayoendana nao.
  7. Hisia zinazidi fikra, ongea na mioyo kabla hujaongea na akili za wateja wako. Watu hawanunui kwa kutumia fikra, bali wananunua kwa kutumia hisia. Hisia ndiyo zinawafanya watu kuchukua hatua, wakati fikra zinawafanya watu kufikia hitimisho la kitu fulani. Hivyo kama unataka kuwauzia wateja wako, gusa hisia zao. Unagusa hisia za wateja wako pale biashara yako inapokuwa halisi na inapokuwa na utu, pale mteja anapoonwa anathaminiwa kama mtu na siyo tu kwa ajili ya kuuziwa. Pale mteja anapoona anachukuliwa kama rafiki, na hapo anaona ni wajibu kwake kuilipa biashara hiyo, kwa sababu imemjali sana.
  8. Tengeneza jumuiya ya wateja wa biashara yako. Binadamu tuna tabia ua kupenda kuwa ndani ya kundi, kuwa kwenye jumuiya fulani. Ukitaka biashara yako ikue na uwafikie wengi, tengeneza jumuiya ya wateja wa biashara yako. Mfanye mteja apende kununua kwako kwa sababu anakuwa kwenye kundi la watu wachache ambao wananufaika na kile unachotoa. Na njia ya kufanya hivi ni kuwa na bidhaa au huduma ambayo haipatikani kwingine popote ile kwako tu.
  9. Fanya unachosema, kuwa halisi na kuwa muwazi. Biashara yako inapaswa kufanya kile ambacho unahubiri, na inapaswa kuwa halisi na ya wazi. Wateja sasa hivi wana nguvu kubwa ya kuchagua wanunue kwa nani. Kama kuna hisia wanapata kwamba biashara yako inaficha baadhi ya vitu, labda taarifa fulani muhimu kwa wateja, wataacha kununua kwako. Wape wateja wako taarifa zote muhimu wanazopaswa kuwa nazo ili waweze kufanya maamuzi sahihi kwao.
  10. Tumia nguvu ya sauti yako kuibadili dunia. Mwisho wa siku, uwepo wako kwenye biashara hautakuwa na maana kama hautasaidia dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. Kadiri biashara yako inavyokuwa na unavyofikia wateja wengi, sauti yako inakuwa kubwa pia. Unaweza kutumia sauti hii kuifanya dunia kuwa sehemu salama, kwa kusaidia mipango mbalimbali ya kijamii. Unaweza pia kurudisha sehemu ya faida ya biashara yako kwenye kusaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii inayokuzunguka. Kwa kufanya hivi, biashara yako inazidi kupata sifa nzuri kwa wateja wako.

Hayo ndiyo mambo 10 ya kuzingatia ili kuweza kukuza biashara yako na kuibadili dunia pia. Anza kuyatekeleza kwenye biashara yako.

#2; MAKALA YA WIKI; NJIA TATU ZA KUMUUZIA MTEJA ANAYEKATAA KUNUNUA.

Kama upo kwenye biashara, unajua hili vizuri, umeshamweleza mteja kuhusu kile unachouza, unaona kabisa kwamba mteja anaelekea kununua, lakini unaibuka upinzani. Mteja nakuambia unauza ghali, sina fedha hiyo, au unachouza siyo imara kama ninavyotaka. Sasa ukikubaliana na mteja kirahisi, hutakuja kuuza kwenye maisha yako yote. Kila mteja atakupa sababu na utamwonea huruma, ila jua akitoka kwako ataenda kununua kwingine.

Zipo njia za kumfanya mteja akose sababu na anunue, na baada ya kununua akupende zaidi na hata arudi kununua tena. Kwenye makala ya wiki hii nimekushirikisha njia tatu za kumuuzia mteja anayekataa kununua. Unaweza kusoma njia hizo hapa; Njia Tatu Za Kumuuzia Mteja Ambaye Amekataa Kununua. Jifunze Hapa Ili Usishindwe Kuuza Tena. (https://amkamtanzania.com/2018/06/28/njia-tatu-za-kumuuzia-mteja-ambaye-amekataa-kununua-jifunze-hapa-ili-usishindwe-kuuza-tena/)

#3 TUONGEE PESA; JINSI YA KUITULIZA FEDHA UNAYOIPATA.

Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba wakipata fedha haikai. Wakati hawana fedha wanakuwa na mawazo mazuri sana ya namna gani watatumia fedha hizo. Lakini wakishaikamata fedha, mawazo yote yanapeperuka, wanajikuta wana mengi mazuri ya kufanya.

Ni mpaka pesa ile inapokwisha ndiyo kama wanaamka usingizini hivi, ndiyo akili zinawarudi na kujikuta hawajafanya chochote kikubwa. Fedha zimeisha na hakuna wanachoweza kuonesha kwamba wameweza kufanya kwa fedha waliyopata.

Ili kuondokana na hali hii, unahitaji kuwa na njia ya kuituliza kila fedha unayoipata, hasa inapokuwa fedha nyingi.

Na njia nzuri ya kuanzia ni kuiweka fedha kwenye gereza. Yaani unapopata fedha yoyote, usikimbilie kuanza kuitumia, badala yake iweke kwenye gereza, eneo ambalo hutaweza kuitoa kwa haraka. Unaweza kuwa na akaunti maalumu ya kufungia fedha zako hizo kwa muda. Au ukawa na uwekezaji unaofanya ili fedha hiyo usiwe nayo kwa muda mrefu.

Kumbuka, ukiwa na fedha, matumizi yatajitokeza yenyewe. Watu wataumwa, vitu vitaharibika na utajikuta unatumia fedha uliyosema ni ya kitu fulani. Usikae na fedha nyingi kama bado hujaweza kujijengea nidhamu kali kifedha, nidhamu ya kulala na njaa wakati una fedha fulani mfukoni kwako ambayo umeipangia kufanya kitu kesho.

Cha muhimu zaidi, hapaswi mtu yeyote yule kujua kwamba una kiasi kikubwa cha fedha wakati wowote na popote ulipo. Ukiruhusu hilo, hutaweza kukaa na fedha kabisa. Maana unapokuwa na fedha, ndivyo wale wanaokuzunguka wanavyokuwa na uhitaji mkubwa wa fedha. Na wakijua unazo, watazitaka, hawatajali una mipango gani, wataona mahitaji yao ni muhimu zaidi kuliko mipango yoyote uliyonayo.

vitabu softcopy

#4 HUDUMA NINAZOTOA; USIKOSE SEMINA HII YA KIPEKEE SANA KWAKO.

Rafiki, kuanzia tarehe 5 ya mwezi huu wa julai tutakuwa na semina ya UKUAJI WA BIASHARA, hii ni semina ambapo tutajifunza mbinu 50 za kuongeza faida kwa zaidi ya asilimia 50 kwenye biashara yako.

Ili kushiriki semina hii, unapaswa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA. Kama tayari ni mwanachama na ada yako iko hai, jiandae kwakupata nondo muhimu sana za kuikuza biashara yako. Kama bado hujawa mwanachama, nakuambia chukua hatua leo na uwe mwanachama, kwani ukikosa semina hii, utaendelea kujiona ni mtu usiye na bahati, au ambaye hukuandaliwa kufanikiwa.

Kumbuka kanuni yetu; MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.

Kwenye semina hii nakwenda kukupa maarifa sahihi na kukuelekeza hatua kubwa za kuchukua na wewe utafurahia mafanikio makubwa. Pia kama utataka, nitakwenda kufanya kazi na wewe moja kwa moja kwenye biashara yako kwa mwaka mzima kutumia mbinu hizo ili biashara yako ikue sana.

Kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, jiunge sasa kwa kulipa ada, tsh 50,000/= (elfu hamsini), lipa kwa namba 0717396253 au 0755953887 ukishatuma malipo tuma ujumbe kwa wasap namba 0717396253 wenye majina yako kamili, email na namba ya simu.

Karibu sana rafiki, usikose semina hii kama upo makini na mafanikio yako kibiashara.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; HUOGI MARA MOJA.

‘People often say that motivation doesn’t last. Well, neither does bathing –

that’s why we recommend it daily.’ – Zig Ziglar

kuna watu wanasema kwamba hamasa huwa haidumu, hivyo hakuna haja ya kuhamasishwa.

Wapo pia wanaosema kwamba wakisoma vitabu hawakumbuki waliyosoma hivyo haina maana kusoma vitabu.

Rafiki, tunaoga kila siku na pia tunakula kila siku, je kula na kuoga hakuna maana? Kwa sababu ukioga leo, kesho unakuwa umeshachafuka, unahitaji kuoga leo. Ukila leo kesho unakuwa na njaa unahitaji kula tena.

Mambo yote muhimu kwenye maisha, tunapaswa kuyafanya kila siku, kila siku. Yaani ukishaona kuna kitu imepita siku hujakifanya, jua siyo muhimu kwako na hutakuja kufanikiwa kwenye kitu hicho.

Kama ni muhimu utafanya kila siku, na ukifanya kila siku utafanikiwa.

Hivyo pata hamasa kila siku, na jifunze zaidi kila siku. Kwa sababu kadiri unavyohamasika kila siku na kadiri unavyojifunza kila siku, ndivyo unavyozidi kuwa bora zaidi.

Ni hayo matano kwa juma hili la 26 rafiki yangu, kila la kheri kwenye juma la 27 tunalokwenda kuanza. Na muhimu sana, fanyia kazi kile nilichokushauri ujaribu kwa miezi hii 6 iliyobaki kwa mwaka huu 2018. Ukiwa na lolote usiache kunijulisha kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji