“It’s not what happens to you, but how you react to it that matters.” – Epictetus

AMKA mwanamafanikio,
Amka kwenye siku hii mpya, siku bora na ya kipekee kabisa kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wetu ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo kwa pamoja tunakwenda kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USISINGIZIE KILICHOTOKEA, BALI HATUA ULIZOCHUKUA…
Huwa tunapenda sana kusingizia vitu fulani vilivyotokea kwenye maisha yetu kama ndiyo sababu ya sisi kushindwa kufika tulipotaka kufika, kama hatujafika.
Labda tunasema tulinyanyaswa au kudhulumiwa.
Lada tunajiambia tuliingia kwenye biashara na zikafa,
Labda tunasema tulisoma lakini hatukupata ajira nzuri,
Au tumepata ajira lakini hazina malipo mazuri.
Huenda tunajiambia tulimwamini mtu fulani na akatuangusha.
Au tunasema isingekuwa serikali, wasingekuwa wazazi, isingekuwa jamii au yasingekuwa mazingira basi tungepiga hatua sana.

Huku ni kujidanganya rafiki,
Upo hapo ulipo sasa, siyo kwa sababu ya chochote kilichotokea kwenye maisha yako, bali kwa sababu ya hatua ulizochukua.
Yaani kilichokufikisha hapo ulipo sasa, ni zile hatua ulizochukua, baada ya chochote unachojiambia sasa kama ndiyo sababu.

Ndiyo maana, watu wawili wanaweza kutokea mazingira yaliyofanana kabisa, wote wanapitia kitu cha aina moja, lakini mmoja anafanikiwa sana na mwingine anashindwa kabisa.
Tatizo siyo kinachotokea, tatizo ni zile hatua ambazo mtu anachukua baada ya kitu kutokea.

Asubuhi ya leo tafakari, jikumbushe kila tukio unalojiambia kwenye maisha yako kwamba limekuwa kikwazo kwako kufika unakotaka. Na angalia kama kweli kikwazo kwako ni tukio lile au hatua ambazo ulichukua au hukuchukua.

Kwamba ulianza biashara kwa kushirikiana na mtu na biashara ikafa? Sasa unataka kutuambia kwamba ushirikiano wako na mtu au biashara yako kufa ndiyo imekukwamisha? Si kweli, kilichokukwamisha ni wewe kukata tamaa, kutokurudi tena kwenye biashara kwa sababu ile uliyokuwa nayo imekufa. Rudi kwenye biashara sasa, ukiwa na uzoefu kwamba biashara inahitaji umakini na unaposhirikiana na mwingine, unahitaji kuwa makini zaidi na zaidi. Na hatua hii utakayochukua ndiyo italeta mabadiliko kwenye maisha yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu, siku ya kutokusingizia yaliyotokea, bali kuangalia hatua ambazo umechukua. Haijalishi unakutana na nini, wewe kazana unakweza kufanya nini.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha