AMKA mwanamafanikio,
Amka kwenye siku hii nzuri, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Amka kwenye siku hii mpya tuliyoipata, nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana kwenye maisha yako.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UNAMSIKILIZA NANI?
Kwenye haya maisha, unahitaji kuchagua kabisa kwamba unamsikiliza nani na utafuata nini.
Unahitaji kuamua kama utajisikiliza wewe mwenyewe kwa yale yaliyopo ndani yako na kuyafanyia kazi.
Au utawasikiliza wengine, ambao huwa hawakosi cha kuongea na kushauri kwenye lolote unalofanya kwenye maisha yako.
Iko hivi mwanamafanikio, kitu chochote utakachojaribu kufanya kwenye maisha yako, wapo watakaokuambia unakosea sana, wapo watakaokuambia haiwezekani, utashindwa, wapo watakaokuambia ya nini unafanya, na wapo wachache watakuambia vizuri, songa mbele.
Usisahau pia wapo ambao watanyamaza tu, hawatasema chochote, ila utakapoingia kwenye changamoto watasema tulijua.
Umuhimu wa wewe kujua nini unataka na maisha yako, umuhimu wa kuwa na falsafa ya maisha unayoiishi siku zote, umuhimu wa kuwa na msingi wa maisha unaotumia kufanya maamuzi ni kukusaidia pale unapokuwa njia panda. Pale unapofikiria ufanye unachotaka wewe au ufanye wanachotaka wengine.
Ili kufanikiwa kwenye maisha, kuna mtu mmoja pekee unayepaswa kumsikiliza, wewe mwenyewe, ile sauti yako ya ndani. Huyu ndiye mtu anayejua kwa hakika nini unataka. Wengine wote watasema sana kwa nje, ila hawajui kwa uhakika.
Hivyo mwanamafanikio, yafanye maisha yako kuwa rahisi,
Chagua nani unayemsikiliza na kumfuata kwenye maisha yako.
Kama kuna kitu unakitaka kweli, na kila wakati unakifikiria, chagua kukifanya na usimsikilize yeyote, au chagua kiwasikiloza wengine na uendelee kujilaumu ndani yako maisha yako yote.
Chagua nani unayemsikiliza, halafu ukishachukua hatua usiendelee kulalamika tena, usiendelee kujiuliza uliza nifanye hichi au kile, maana hapo unakuwa unapoteza muda.
Fanya kile unachotaka na kifanye kweli, au fanya kile wengine wanachotaka ufanye na kifanye kweli.
Pande zote mbili zitakuwa na magumu, zitakuwa na changamoto na kitakuwa na kushindwa. Kitu pekee kitakachokuwezesha wewe kushinda siyo kile ulichochagua kufanya, bali kiasi ulichojitoa kufanya.
Amua utamsikiliza nani na chukua hatua, usipoteze muda wako kwenye kubishana na wewe mwenyewe iwapo ufanye hili au ufanye lile. Amua na fanya.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu, siku ya kuamua unayemsikiliza na kuwapotezea wengine wote.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #JiwasheMoto
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha