Wengi husema muda ni fedha, lakini hilo siyo sahihi, muda ni zaidi ya fedha.
Na sababu pekee kwamba muda ni zaidi ya fedha, ukishapoteza muda huwezi kuupata tena. Poteza fedha na unaweza kutafuta nyingine, lakini ukipoteza muda, ndiyo umepotea moja kwa moja.
Hivyo muda ni zaidi ya fedha, kama unahitaji kutumia vizuri fedha zako ili kufikia mafanikio unayotaka, unahitaji kuwa makini zaidi na matumizi ya muda wako ili kufanikiwa.
Lakini muda na fedha vinafanana kwa kitu kimoja, jinsi vinavyotumika. Kuna mambo mawili unaweza kuyafanya na fedha yoyote unayokuwa nayo, kuitumia fedha hiyo au kuiwekeza. Ukiitumia ndiyo imeondoka na huipati tena, ukiiwekeza inakuzalishia faida zaidi kwa ajili ya baadaye.

Kadhalika kwenye muda, unaweza kufanya mambo hayo mawili. Unaweza kuutumia muda ulionao, kufanya kile kilichopo mbele yako na hapo muda huo unakuwa umeondoka. Lakini pia unaweza kuwekeza muda ulionao, na ukaweza kutengeneza makubwa zaidi kwa siku za baadaye.
Unapowekeza muda wako, unatengeneza muda zaidi kwa ajili yako siku za baadaye. Hii ni kwa sababu muda mdogo unaotumia kufanya kitu kitakachokunufaisha baadaye, unakusaidia kupata muda zaidi baadaye.
Njia bora kabisa ya kuwekeza muda wako ni kwenye kujifunza. Abraham Lincolin aliyekuwa raisi wa marekani aliwahi kunukuliwa akisema, ukinipa masaa 6 ya kukata mti, nitatumia masaa manne ya kunoa shoka langu. Hii ina mantiki kubwa kwa sababu shoka kali linakata mti haraka kuliko shoka gumu. Hivyo muda unaokuwa umewekeza kunoa shoka, unapunguza muda utakaohitaji kwenye kukata mti.
SOMA; UKURASA WA 819; Umasikini Wa Muda…
Kadhalika, muda wowote unaotumia kujifunza kuhusu kile unachofanya, unapunguza sana muda utakaotumia kwenye kufanya kitu hicho. Hebu angalia, pale unapokuwa hujui kile unachofanya, unajaribu jaribu vitu vingi na unakosea, kote huko muda wako unapotea. Lakini unapojua kile hasa unachofanya, unaokoa sana muda wako.
Wekeza vizuri muda wako kwa kujifunza sana kuhusiana na chochote unachofanya. Usitake kurudia makosa ambayo tayari wengine walishayafanya. Jifunze kupitia makosa ya wengine na chukua hatua sahihi. Muda unaowekeza kwenye kujifunza utaokoa muda mwingi kwenye kuchukua hatua.
Kabla hujaanza kufanya chochote kipya, tenga muda wa kujifunza kwanza kuhusu kitu hicho, utaokoa muda mwingi kwenye ufanyaji na utapata matokeo bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog