Kila mtu kuna wakati fulani kwenye maisha yake anafanya maamuzi ambayo baadaye yanakuja kuwa mabaya kwake.

Kila mtu kuna wakati ambapo anaangushwa, anaahidiwa kitu fulani na hakitekelezwi kama kilivyoahidiwa.

Kila mtu kuna wakati anakasirishwa na vitu au watu fulani.

Kila mtu kuna wakati anashindwa kupata majibu sahihi ya anachohitaji, au anakosea kwenye vitu anavyohitaji.

Kila mtu kuna wakati anasemwa vibaya, kuchukiwa na hata kufanyiwa mabaya na watu wengine.

Kila mtu kuna wakati amewahi kushindwa kwenye jambo muhimu sana, ambalo aliweka nguvu zake zote na alikuwa na uhakika wa kufanikiwa.

Hivyo ndivyo dunia inavyokwenda na kila mtu kuna maumivu ambayo ameshayaonja hapa duniani.

Hivyo basi, mambo haya yanapotokea kwako, usitake kuona kama wewe ni wa tofauti sana, kwamba wewe hukustahili na kamwe usiache kufanya kile ambacho unafanya au kufika kule unakotaka kufika.

SOMA; UKURASA WA 66; Dalili Za Kuanguka, Zijue Na Jinsi Ya Kuepuka.

Mambo hayo mabaya unayoona yamekutokea wewe, jua kila mtu kwa wakati fulani yalishamtokea. Na wale ambao unaona wamefanikiwa, siyo kwamba hawakukutana na uliyokutana nayo wewe, bali waliyavuka na kusonga mbele zaidi.

Usikubali chochote unachokutana nacho kwenye safari ya maisha yako kiwe ndiyo mwisho au ukomo wa ndoto zako kubwa. Kama bado una pumua, ipo njia ya wewe kuweza kufikia ndoto zako.

Kauli maarufu ya kama huwezi kuruka kimbia, kama huwezi kukimbia tembea, kama huwezi kutembea tamaa, muhimu ni ufanye kitu kusonga mbele, usibaki pale ulipo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha