Chochote unachofanya kwenye maisha yako, hebu jikumbushe siku ya kwanza kabisa kufanya ilikuwaje?
Kazi yako, kumbuka siku ya kwanza kabisa ulipoanza kazi, ulikuwa na hamasa kiasi gani, uliwahi kiasi gani na ulikuwa na utayari kiasi gani wa kufanya kila unachoambiwa kufanya? Kwa hakika hamasa ulikuwa juu, uliwahi sana na ulikuwa tayari kufanya chochote unachoambiwa ufanye. Hukuona kosa au mapungufu yoyote kwenye kazi hiyo na ulijituma bila ya ukomo. Lakini muda ulivyozidi kwenda ulianza kuzoea kazi hiyo, hamasa ikaanza kupungua, ukaanza kuchelewa na kuanza kuona mapungufu yaliyopo kwenye kazi hiyo.

Kwenye biashara pia, siku za mwanzo jikumbushe zilivyokuwa, ulikuwa unamwona mteja kama mfalme, unakazana kumpa huduma bora na hukukubali mteja aondoke bila ya kununua, kwa sababu ulijua manunuzi ya mteja mmoja ndiyo yatakayokuweka kwenye biashara. Uliwahi kufungua biashara yako na ulikaa kwenye biashara kwa muda mrefu. Lakini siku zilivyokwenda, ulipoanza kupata wateja wengi na faida kubwa, ulipokua zaidi kibiashara ukaanza kujisahau, ukaanza kuwachukulia wateja kawaida na ile hamasa ya mwanzo ikawa haipo tena.
Kwenye maisha ya mahusiano, jikumbushe siku ya kwanza na mwenza wako, jinsi ulivyokuwa na hamasa kubwa, jinsi ulivyoona mazuri yake mengi, ambayo hakuna upungufu wake wowote ulioweza kuzidi mazuri yake, hukuambiwa wala hukusikia lolote, na pia hukuona yale ambayo wengine walikuwa wanaona wazi kuhusu mwenza wako. Lakini baada ya muda kupiga ukaanza kumzoea, ukaanza kuona mapungufu yake, ambayo yakawa ni makubwa kuliko mazuri yake, ukaanza kuona hakufai tena.
SOMA; UKURASA WA 1000; Siku Elfu Moja (1000) Za Kuandika Kila Siku Bila Ya Kuacha Hata Siku Moja.
Katika kila hali unayopitia kwenye maisha yako, ambayo mwanzoni ilikuwa inakupa hamasa kubwa, lakini baadaye kama ukaichoka na kuzoea, kinachobadilika siyo hali au kitu, kinachobadilika ni wewe, ambapo unaacha kufanya kwa hamasa na unaanza kufanya kwa mazoea.
Kitu chochote utakachofanya kwa mazoea kwenye maisha yako kitaanguka, kwa sababu mazoea ni mabaya sana. mazoea hayaoni utofauti mkubwa uliopo kwenye chochote, mazoea hayana hamasa na mazoea yanaua kabisa ubunifu wowote.
Chochote unachofanya, jikumbushe siku ya kwanza kufanya na kila siku endelea kufanya kama vile ndiyo siku ya kwanza kwako kufanya. Hili ni swala la kuchagua na yeyote anaweza kuchagua na akafanya kwa ubora wa hali ya juu na hamasa kubwa sana, kama vile ndiyo siku ya kwanza kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,