Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifikiri kwamba kikwazo cha wateja kununua kwao ni bei. Wengi wanashawishika kwamba wakishusha bei basi watapata wateja wengi.

Na wakijaribu kufanya hivyo mwanzoni wanaweza kuona ongezeko la wateja, lakini mwisho wa siku hilo haliwasaidii kwenye ukuaji wa biashara zao.

Hii ni kwa sababu moja, wateja makini wa biashara yako, hawatumii bei kama kigezo pekee cha kununua. Na wale wateja wanaotumia bei kama kigezo pekee cha kununua, siyo wateja makini na sahihi wa biashara yako.

Kwa sababu ukishusha bei leo wakaja, wakisikia kuna mwingine kashusha bei, basi watakuacha na kwenda kule.

Wewe huhitaji wateja wa aina hii, wanaowinda bei, bali unahitaji wateja wenye uhitaji ambao unaweza kuutimiza, wenye matatizo ambayo unaweza kuyatatua, na ukawatatulia kwa namna ambayo ni bora kabisa, na wakanufaika sana na unachofanya.

Hivyo basi, wateja makini na sahihi wa biashara yako, hawatakumbuka sana ni kiasi gani wamelipa, bali watakachokumbuka maisha yao yote, ni ile thamani ambayo wameipata.

SOMA; Mambo Matano (05) Muhimu Ya Kuzingatia Wakati Wa Kupanga Bei Ya Huduma Au Bidhaa Kwenye Biashara Yako.

Kama thamani itakuwa bora, watakumbuka na kurudi tena, pia watawaambia wengine nao waje. Kama thamani itakuwa ya hivyo watakumbuka na kukuepuka, na pia watawaambia wengine wasije kabisa kwako.

Kama unataka kuwa mfanyabiashara makini, unayetaka kutengeneza wateja makini, cha kupigana nacho siyo bei bali thamani unayompa mteja. Fanya kitu ambacho mteja hatakusahau kwa maisha yake yote, na hapo utakuwa umejitengenezea mteja wa muda mrefu wa biashara yako, tena asiyejali kuhusu bei.

Bei au gharama waliyolipa wengi wanasahau haraka, lakini thamani waliyopata, iwe nzuri au mbaya, watu wataendelea kuikumbuka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha