Kitu chochote kikubwa unachotaka kwenye maisha yako, kitahitaji muda mpaka kukipata kweli. Kadiri kile unachotaka kinavyokuwa kikubwa, ndivyo muda wa kukipata unakuwa mkubwa pia.

Lakini wengi wamekuwa wanakosa kila wanachotaka, kwa sababu ya haraka. Wengi wamekuwa hawa subira wala uvumilivu, wamekuwa wanataka kitu na wanakitaka sasa.

Hata wahenga walisema, haraka haraka haina baraka. Chochote unachokazana kufanya kwa haraka, jua kuna kitu utajikosesha, kuna vitu hutaviangalia vizuri na hili litasababisha matatizo makubwa zaidi baadaye.

Angalia makosa yote makubwa ambayo umewahi kufanya kwenye maisha yako, angalia uwekezaji ambao umewahi kufanya na ukapoteza kila kitu, angalia mambo ambayo umewahi kudanganywa, kulaghaiwa na hata kutapeliwa. Ukiangalia yote hayo utaona kitu kimoja, haraka ilikuponza. Uliweka haraka kwenye kufanya maamuzi, uliweka haraka kwenye kuchukua hatua na uliweka haraka kwenye kutaka matokeo.

SOMA; UKURASA WA 991; Kinachoota Haraka, Hupotea Haraka…

Haraka zako zikakuzuia usiuone ukweli jinsi ulivyo na hivyo ukafanya mambo ambayo siyo sahihi.

Mipango yote mikubwa ya maisha yako, inahitaji kuchukua hatua kwa wakati. Unahitaji kupiga hatua moja, kisha kupima kabla hujachukua hatua nyingine. Usikimbilie kuchukua kila hatua kama vile kuna kitu unachelewa, kila unapopata msukumo wa kuweka haraka, jikumbushe kipi muhimu na hatua zipi ni muhimu.

Ukishindwa kujizuia kwenye haraka, utabomoa msingi mzima uliokuwa umejijengea huko nyuma wa kupata kile unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha