Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HAKUNA ANAYEIANZA SIKU KWA KUTAKA MABAYA, LAKINI YANATOKEOA…
Hakuna mtu anayeianza siku yake akijiambia leo nataka kuwa na siku ya hovyo kabisa.
Leo nataka kwenda kugombana na kila nitakayekutana naye.
Leo nataka kwenda kushindwa kwenye kila ninachojaribu.
Hakuna yeyote mwenye akili timamu anayeianza siku yale hivyo.
Lakini kwa wengi hivyo ndivyo siku zao zinavyoisha.

Hii ina maana kwamba, kama watu hawaanzi wakitegemea mabaya, lakini wanamaliza na mabaya, hapo katikati, kuna mambo yanatokea, ambayo watu wanakuwa hawana udhibiti nayo.
Na hayo ndiyo yanayoharibu siku za wengi.

Bondia mmoja aliwahi kusema, kila bondia anayeingia kwenye pambano huwa ana mpango mzuri, lakini akishapigwa ngumi ya uso, mipango yote inavurugika. Nafikiri ndiyo sababu mabondia huwa wanalinda sana uso.

Sasa tukirudi kwenye siku zetu, kila mtu huwa anakuwa na mpango mzuri wa jinsi ya kuiendesha siku yake, mpaka pale anapokutana uso kwa uso na dunia halisi, dunia ambayo inaenda kinyume na mipango hii. Dunia ambayo inampiga ngumi usoni na anapoteana kabisa.

Hivyo basi rafiki, kwa mipango yoyote tunayojiwekea kwenye siku zetu, tuwe na mpango mbadala, tuwe na hatua mbadala za kuchukua, pale mambo yanapokwenda tofauti na tulivyotegemea yaende.
Kwa sababu bila ya mpango wa aina hii, utakapokutana na ambacho hukutegemea, ni rahisi sana kupoteana na siku yako ikapotea.

Kumbuka wakati wewe unapanga kufanya makubwa, kuna wengine wanajipanga kuhakikisha hakuna hatua utakayoweza kupiga.
Iwapo wanajua njia yako ni mojw, ni rahisi kwao kuiziba na ukapata shida.
Kuwa na njia nyingi, njia mbadala kiasi kwamba anayefikiria kukuzuia hajui hata atumie njia ipi.

Ukawe na siku bora sana leo, siku ya kufanya makubwa, siku ya kuwa na mipango mbadala na kutokukubali kurudishwa nyuma na chochote.
#Fanya #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha