Ni kutokuishi kwa kiwango cha uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Hichi ni kitu ambacho utakijutia sana, na hutajisamehe kwa kosa hilo. Ukiwa bado mdogo, bado kijana, bado mtu mzima unaweza kujidanganya kwamba muda bado unao.

Ni pale unapokuwa mzee, pale unapokuwa huna tena muda mrefu wala nguvu za kupambana, ndiyo utaangalia nyuma na kuona hujaweza kufanya kulingana na uwezo wako, hilo litakusikitisha na utajitia sana.

Utaona kama maisha yako yote umeyapoteza kwa mambo yasiyo muhimu. Utaumia sana pale utakapoona wale ambao walitumia uwezo mkubwa uliopo ndani yao, ambao unajua hata hawana uwezo mkubwa kama wako wakiwa na maisha ya furaha na mafanikio.

SOMA; UKURASA WA 938; Nyakati Ngumu Ndiyo Za Kutengeneza Maana.

Kitu kikubwa sana kitakachokuzuia wewe kuishi uwezo mkubwa uliopo ndani yako kitakuwa usumbufu unaoruhusu kwenye maisha yako. Unaporuhusu kila aina ya usumbufu kuingia kwenye maisha yako, unapoteza muda mwingi kuhangaika na usumbufu kuliko kufanya yale muhimu.

Kitu kingine kitakachokuzuia kuishi uwezo mkubwa uliopo ndani yako ni kuridhika haraka na vitu vidogo. Kwa mfano watu wengi walioajiriwa wamekuwa wanasahau kabisa uwezo mkubwa uliopo ndani yao. Kinachowafanya wasahau uwezo huo ni mshahara wanaopata kila mwezi, wanauzoea na kuutegemea, na hivyo kufikiri hawawezi kuishi nje ya mshahara huo.

Rafiki yangu mpendwa, hakuna kitu kibaya kwenye maisha kama majuto. Majuto ni mabaya kwa sababu wakati unajutia, unakuwa huna tena hatua kubwa unazoweza kuchukua.

Hivyo kabla hujafika kwenye hatua ya majuto, chukua hatua sasa wakati bado unaweza. Jua uwezo mkubwa uliopo ndani yako na ufanyie kazi. Usikubali kabisa uwezo wako upotee, usijisahau kwa chochote unachotapa sasa. Weka juhudi kuweza kutumia uwezo uliopo ndani yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha