Kikwazo namba moja kwenye mauzo katika biashara nyingi ni mteja kukosa machaguo zaidi wakati ananunua.

Mteja anaweza kuja kwenye biashara yako, akiwa na shida au uhitaji fulani. Wewe kama mfanyabiashara ukamweleza na kumpa kile ambacho unaona kinamfaa.

Sasa utafanya kosa kubwa sana, kama utampa kitu kimoja tu. Maana wakati wote huo mteja yupo kwenye njia panga ya ninunue au nisinunue. Hivyo unapompa kitu kimoja, anaendelea na ubishani ndani yake iwapo anunue au asinunue. Na kwa kuwa kununua kunaumiza, atafikia hitimisho la kutokununua.

Njia bora ya kumwondoa mteja kwenye njia panda hiyo ya anunue au asinunue ni kumpa machaguo mawili. Unamsikiliza shida aliyonayo, kisha unachagua bidhaa au huduma mbili zinazoweza kumsaidia. Kisha unamwelezea kila bidhaa au kila huduma inavyoweza kumsaidia. Halafu mwisho unamuuliza katika hizi mbili unataka ipi.

Kwa kufanya hivyo unakuwa umemhamisha kwenye njia panda ya ninunue au nisinunue na kumweka kwenye njia panda ya ninunue hii au ninunue ile. Ukishaweza kumfikisha mteja hapo, kwa nafasi kubwa sana atanunua. Kwa sababu unakuwa umemtoa upande hasi wa kutonunua na kumfikisha upande chanya wa kipi anunue.

SOMA; BIASHARA LEO; Ushauri Bora Kabisa Wa Biashara Yako Upo Kwenye Tabia Za Wateja Wako…

Mpe mteja machaguo mawili au matatu, na hakikisha yote ni bora kabisa kwake, kisha mpe nafasi ya kuchagua. Hii ni njia bora ya kumweka mteja upande wa kununua.

Angalizo; usimpe mteja machaguo mengi sana, hata kama yapo, mpe yale ambayo ni bora kabisa, mawili au matatu. Kwa sababu ukimpa machaguo mengi sana, utamfanya asinunue. Maana atakuwa na wasiwasi kwamba anachochagua kinaweza kisiwe bora sana ukilinganisha na vingine vilivyopo. Hivyo atakuambia anaenda kufikiria kwanza, na mteja akishakuambia hivyo, jua amekuhama kirahisi.

Kuwa na chaguo zaidi ya moja, lakini yasizidi matatu, ili kumweka mteja kwenye hali ya kuchagua anunue kipi kati ya ulivyomwonesha, badala ya kuwa kwenye hali ya kufikiria anunue au asinunue.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha