Kwanza kabisa futa dhana kwamba unaweza kuwabadili watu, huwezi, hiyo ni kazi ngumu sana unayoweza kujipa kwenye maisha yako. Hata kama watu watakuahidi kubadilika, bado siyo wewe utakaowabadili, ila watabadilika wao wenyewe.

Nakukumbusha hili kwa sababu watu wengi sana wameingia kwenye matatizo, watu waliamini wenzao watabadilika, lakini wanakuja kugundua hawawezi kubadilika. Na kinachowaumiza siyo tu hawabadiliki, bali wanajua vitu vingine ambavyo vilifichwa, ambavyo ni vibaya zaidi.

Watu wanaidanganya sana hili maeneo matatu, moja kwenye mahusiano, watu wawili wanakutana, wanashawishiana kwamba wamependana na wapo tayari kwenda pamoja, ila mmoja anakuwa na tabia fulani ambazo mwenzake hazipendi, anaahidi kubadilika, wanaingia kwenye mahusiano, tabia hazibadiliki na baadaye wanashindwa kwenda pamoja.

Eneo la pili ni watu wanaokutana, wenye kiu ya mafanikio, wanakubaliana kushirikiana kwenye biashara, lakini mmoja anaonekana kuwa na tabia ambazo zitaathiri biashara, anaahidi kubadilika, lakini habadiliki na biashara inakufa au ushirikiano kuvunjika.

SOMA; UKURASA WA 737; Watu Wanakuangalia Zaidi Ya Kukusikiliza….

Eneo la tatu ni kupata wafanyakazi, watu wanatafuta watu wa kuwasaidia kwenye kazi zao, wanapata mtu ambaye anaonekana kuweza kazi vizuri, lakini kuna tabia fulani ambazo anazo na hazitaendana na kazi ile, wanawaambia na watu hao wanaahidi kubadilika. Lakini hawabadiliki na kazi inawashinda.

Rafiki yangu, kabla hujaingia kirahisi kwenye mtego wa watu kubadilika, naomba ukumbuke kwamba mabadiliko ni magumu na yanaumiza. Hivyo lazima mtu awe na sababu kubwa sana ndani yake, ambayo inamuumiza sana kuliko maumivu ya mabadiliko. Kama hakuna sababu ya aina hiyo, hata kama atakula viapo vya aina gani, kwamba atabadilika, hatabadilika.

Sasa ili kuokoa muda wako na nguvu zako, na ili kutokurudi tena nyuma, achana na watu ambao wanahitaji kubadilika, na nenda na wale ambao hawana cha kubadilisha.

Yaani angalia watu ambao unaweza kujihusisha nao, ambao hawahitaji kubadilika, na hapo ni rahisi kwenda pamoja. Na nielewe hapa, sisemi utafute mtu mkamilifu, kwa sababu hakuna aliyekamilika, kila mtu ana changamoto zake.

Jukumu lako ni kuchagua wale ambao changamoto zao hazina madhara kwenye kile mnakwenda kufanya pamoja, hivyo hata kama hatabadilika, haitadhuru kile mnachofanya.

Kwa mfano kama kazi unayotaka kumpa mtu inahitaji umakini na muda mwingi ndani ya kazi na haya nje ya kazi, ukipata mtu ambaye ni mlevi, kazi hiyo haitamfaa. Sasa hata kama atakuahidi anaacha ulevi, sitakushauri uende naye, maana utasumbuka. Itakuwa rahisi kwako kupata mtu ambaye siyo mlevi kabisa, na hapo sehemu kubwa ya matatizo itakuwa imezuiwa.

Watu wanapenda kuwa vile walivyo, na wengi ndivyo walivyo, juhudi zako za kutaka kuwabadili watu haziwezi kuzaa matunda bora, sana sana zitazaa majeruhi. Nenda na wale watu ambao tayari wana kile unachotaka, au hawana kile ambacho hutaki. Mengine mtachukuliana kibinadamu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha