Tukisema ukweli kama ulivyo;

Kuna watu wana akili kuliko wewe, na huna cha kufanya kuwazidi watu hao akili.

Kuna watu wana mtandao mkubwa wa watu wanaojuana nao kuliko wee, na huna cha kufanya kuwazidi watu hao.

Kuna watu wanaweza kupewa nafasi nzuri hata kama hawastahili, na huna cha kufanya kwenye hilo.

Pia kuna watu wenye elimu kuliko wewe, ambapo huenda ikawa vigumu kwako kufikia elimu ambayo wamefikia.

Maeneo hayo na mengine yanayofanana na hayo, ni magumu sana kwako kushindana. Maana wale unaotaka kushindana nao, tayari wameshapiga hatua fulani kuliko wewe, hivyo wanakuwa upande mzuri kuliko wewe.

Katika hali kama hiyo, kuna eneo moja ambalo unaweza kushindana na asiwepo yeyote wa kukushinda. Eneo hili haliangalii umetokea wapi, haliangalii elimu yako na wala haliangalii nani anakujua au unamjua nani.

Ni eneo ambalo unaweza kushindana na yeyote na ukamwacha mbali sana. Ni eneo ambalo ukilifanyia kazi vizuri linaweza kukupa chochote unachotaka. Na hili ni eneo ambalo unapaswa kulipenda sana na kuliheshimu zaidi.

Eneo ninalozungumzia hapa ni kazi. Kazi ndiyo kitu pekee unachoweza kukitumia kwenye ushindani pale ambapo huna sifa  nyingine yoyote. Hata kama wale wanaokuzunguka wana sifa nyingi kiasi gani, wewe unaweza kushindana nao na ukawaacha mbali sana kwenye kazi.

SOMA; UKURASA WA 941; Juhudi Hizo Weka Kwenye Kila Eneo La Maisha Yako…

Kwa chochote unachofanya, hata kama ni kidogo kiasi gani, weka kazi kubwa sana, weka umakini wa hali ya juu, weka ubunifu wa kipekee na toa matokeo ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kuyatoa.

Weka kazi sana, kiasi kwamba mtu akiangalia anaona tofauti kubwa kati ya ulichofanya wewe na walichofanya wengine. Na kwa njia hii utajiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa zaidi na kupiga hatua zaidi ya walivyopiga wengine.

Hakuna mtu ambaye amewahi kufukuzwa kazi kwa sababu amefanya kazi zaidi, lakini wengi wanafukuzwa kazi kwa sababu hawafanyi kazi zao vizuri, hii inaonesha jinsi gani kazi ilivyo na thamani.

Hakuna mtu amewahi kushindwa kwenye biashara  kwa sababu ameweka kazi zaidi, lakini wengi wanashindwa kwenye biashara kwa sababu hawajaweka juhudi kubwa.

Kazi ni bora, kazi ni nzuri, kazi inakutofautisha na watu wengine wote wanaokuzunguka na wanaofanya unachofanya. Weka kazi sana na hutabaki pale ulipo sasa.

Nimalizie kwa kukuambia hili rafiki yangu, chochote ambacho wengine wanacho ila wewe huna, unaweza kukipata kwa kuweka kazi zaidi. Penda kazi na weka kazi, maisha yako yatakuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha