Unapofikiria kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unaanza kwa kujiwekea malengo na mipango mikubwa sana. Unajiwekea malengo makubwa kiasi kwamba watu wa kawaida wakiyasikia wanaona labda umechanganyikiwa, au hujui unachofanya.
Lakini kwa kuwa wakati huo unakuwa na hamasa kubwa, huwasikii sana na unajua hakuna linaloshindikana.
Ni pale unapoanza kufanya ndiyo unakutana na uhalisia wa dunia. Kitu cha kwanza kitakachokukaribisha kitakuwa ni kushindwa. Utashindwa kwenye hatua utakazoanza kuchukua. Utapata matokeo mabaya kuliko ulivyotegemea.
Ni hapa kwenye kushindwa ndiyo mchujo wa kwanza wa mafanikio unapofanyika. Maana wengi huacha baada ya kukutana na kushindwa huku. Wachache sana ndiyo huwa wanavuka na kwenda kwenye mchujo wa pili.
Ni wakati huu mgumu, wakati wa kushindwa ndiyo wengi wanapoteza ile hamasa waliyoanza nayo, ndipo wanapoanza kuwasikia wale waliokuwa wanawakatisha tamaa na kusema labda walikuwa sahihi. Wanaona kwamba walikuwa wanafikiria nini mpaka wakajiwekea malengo makubwa hivyo, kiasi kwamba wameanza kwa kushindwa.
SOMA; UKURASA WA 1004; Unapojishikiza Kwenye Vitu, Unapoteza Uhuru Wako…
Hapa ndipo wengi hushawishika na kushusha viwango vyao vya mafanikio. Kukubali kwamba hawawezi yale makubwa ambayo walikuwa wanayafikiria na ni bora kurudi kwenye madogo waliyozoea, madogo ambayo hawajawahi kushindwa.
Upo usemi kwamba ni bora kuwa samaki mdogo kwenye bahari kubwa kuliko kuwa samaki mkubwa kwenye dimbwi dogo la maji. Unapokuwa na malengo makubwa kabisa na ukashindwa au usiyafikie, bado hutakuwa mtu wa kawaida, kwa sababu utakachopata hakitakuwa sawa na wale wanaofanya kawaida.
Lakini kama utakuwa na malengo madogo na ya kawaida na ukayafikia, hutakuwa na tofauti yoyote kwenye maisha yako. Maana hicho ndiyo ulichozoea, hicho ndiyo kila mtu anafanya.
Kamwe usishushe viwango, hata ukutane na magumu kiasi gani, usijidanganye kwamba ulifikiria juu sana. Mara zote jikumbushe kwamba ulifikiria kwa usahihi na wakati wa magumu siyo wakati wa kupangilia upya malengo yako. Kumbuka kwamba magumu utakutana nayo na utaendelea kukutana nayo. Lakini kushusha viwango vyako ni mwiko.
Mwisho kabisa, kaa mbali na kundi kubwa la watu kama ukoma. Kama kitu kinafanywa na kila mtu, siyo kitu sahihi kwako kufanya, maana hakitakupa utofauti wowote na hakitakufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,