Rafiki yangu mpendwa,
Sihitaji tena kutumia muda mwingi kukushawishi kwa nini fedha ni muhimu na kwa nini kutengeneza kipato zaidi inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako. Kwa sababu kama mpaka sasa hujalielewa hilo, una tatizo kubwa zaidi ambalo msaada wake hauwezi kupatikana kwenye makala kama hii.
Kosa kubwa ambalo watu wengi wamekuwa wanalifanya kwenye fedha ni kua na ukomo kwenye kipato wanachotengeneza. Hili siyo tu ni kosa, bali ni chanzo kikuu cha umasikini kwa wengi.
Ninachoamini ni kwamba, kama mtu anaweza kutengeneza shilingi elfu moja, basi anaweza kutengeneza elfu kumi, kama anaweza kutengeneza elfu kumi basi pia anaweza kutengeneza laki moja. Kama mtu anaweza kutengeneza laki moja anaweza kutengeneza milioni. Na kama mtu anaweza kutengeneza milioni, basi anaweza kutengeneza mamilioni zaidi mpaka bilioni.
Kinachowazuia watu wasitengeneze kipato zaidi ya wanachotengeneza sasa ni ukomo waliojiwekea kwenye kipato. Watu wengi wanakuwa wamekubaliana na kipato wanachotengeneza sasa, wameshayapanga maisha yao kwa kipato hicho na hawapo tayari kujituma zaidi ili kutengeneza kipato zaidi.
Rafiki, hakuna ubishi kwamba kila mtu anahitaji kutengeneza kipato zaidi. Siyo tu kwa mahitaji binafsi, bali pia kama njia ya kuwasaidia wengine. Kwa sababu kadiri unavyokuwa na kipato zaidi ndivyo na wengine wanavyonufaika, iwe ni moja kwa moja au siyo moja kwa moja.
Watu wengi wamekuwa wanajiwekea ukomo wa kipato kwa njia hizi tatu ambazo zinawazuia kufikia uhuru wa kifedha.
Moja; uhaba wa mifereji ya kuingiza kipato.
Kipato chako ni kama bahari na zile njia unazotumia kuingiza kipato ni kama mifereji au mito inayoingiza maji baharini. Kama una njia chache za kuingiza kipato, kipato chako kitakuwa kidogo.
Kama kipato chako ni mshahara pekee, au kama una biashara moja pekee, umejiwekea ukomo wa kipato, ambao hautakuacha salama, hasa kwa zama hizi ambazo dunia inakwenda kasi sana.
Mbili; kujithaminisha chini.
Njia nyingine wengi wamekuwa wanajiwekea ukomo kwenye kipato ni kujithaminisha chini. Dunia inakupa kile unachoitaka ikupe, na siyo unachojiambia unastahili kupata. Watu wengi wamekuwa wanaogopa kutaka kulipwa kiasi kikubwa, na hivyo wanaishiwa kulipwa kiasi kidogo.
Wengi wamekuwa wanafikiri wakitaka walipwe kiasi kikubwa, iwe ni kwenye kazi au biashara basi watakosa wa kuwaajiri au wateja wa kununua. Lakini mtu hupaswi kuhofia hili kama utafanyia kazi namba tatu hapo chini.
Tatu; kutokutoa thamani kubwa.
Malipo yako ni sawasawa na thamani unayoitoa kwa wengine. Kama unalipwa kidogo ni kiashiria kwamba unatoa thamani ndogo. Na kama unahitaji kulipwa zaidi, lazima utoe thamani zaidi.
Watu wengi wamekuwa hawapo tayari kutoa thamani zaidi, hawapo tayari kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora zaidi. Wengi wanafanya kwa mazoea na ndiyo maana hawawezi kutaka kulipwa zaidi.
Zifuatazo ni njia za kuondoa ukomo uliojiwekea kwenye kipato.
- Ongeza mifereji yako ya kipato.
Kama una mifereji ya kipato chini ya mitano, upo kwenye hatari, chochote kinaweza kutokea na kikakuangusha kabisa. Unahitaji kuwa na mifereji mingi zaidi ya kipato, na mifereji hiyo iwe tofauti tofauti kiasi kwamba chochote kinachoweza kutokea, hakiwezi kukausha mifereji yote kwa wakati mmoja.
Kama umeajiriwa hakikisha unaanzisha biashara ya pembeni, na kama tayari una biashara, hakikisha unaanzisha biashara nyingine. Unachohitaji ni uhuru wa kifedha na unahitaji kuwa na vyanzo vingi uwezavyo. Pia unahitaji kuwa na uwekezaji endelevu, huu utakuwa chanzo chako kizuri cha kipato baadaye.
- Toa thamani kubwa sana.
Chochote unachogusa, usikiache kawaida, bali acha alama ya kipekee, alama ambayo kila anayeangalia anasema kitu hichi kimefanywa vizuri. Toa thamani kubwa sana, thamani ambayo haipatikani kwingine kokote na watu lazima waje kwako tu kuipata.
Ukitoa thamani kubwa unajiondoa kwenye ushindani na ukishajiondoa kwenye ushindani wewe ndiye utakayepanga bei yako mwenyewe na huna haja ya kuangalia wengine wamepanga bei kiasi gani. Maana watu hawana uwezo wa kulinganisha unachotoa wewe na wanachotoa wengine.
SOMA; Mambo 10 Ya Kujifunza Kuhusu Fedha Na Utajiri Kutoka Kwenye Orodha Ya Mabilionea Ya Mwaka 2018.
- Usione aibu kutaka malipo makubwa zaidi.
Kama unatoa thamani kubwa, thamani ambayo haiwezi kutolewa na mwingine ila wewe tu, una nguvu ya kudai malipo makubwa zaidi. Na kama unatoa thamani kubwa kweli, usione aibu kutaka malipo makubwa.
Malipo makubwa ni haki yako kama unatoa thamani kubwa, usijiweke nyuma kwa sababu unaona watu watakuona una tamaa ya fedha. Unapaswa kulipwa kulingana na thamani kubwa unayotoa, na kama unaowapa thamani hiyo kubwa hawapo tayari kuilipia, tafuta wengine walio tayari kulipia thamani hiyo kubwa.
- Acha kufikiria kusukuma maisha, fikiria kutengeneza maisha.
Kama unachotaka ni hela ya kula leo, kama unachofikiria ni kusukuma maisha yako kwa leo tu, hicho ndiyo utakachopata. Utajiwekea ukomo kwamba ukishapata hela ya kula basi mengine yote yako sawa.
Kujiondoa kwenye ukomo huu anza kufikiria kutengeneza maisha, anza kufikiria makubwa. Anza kufikiria mara kumi ya kipato unachotengeneza sasa na ongeza juhudi zako mara dufu ili kufikia kiwango chako kipya. Na kila unapoongeza kipato chako, usiridhike, fikiria tena mara kumi ya kipato ulichofikia. Siyo kwamba unakuwa na tamaa, bali unatengeneza maisha ya uhuru mkubwa kwako.
- Kuwa na mpango bora wa uwekezaji, unaozalisha kipato.
Una ukomo wa muda na nguvu za kufanya kazi, lakini fedha haina ukomo wa aina hiyo. wanasema fedha hailali, fedha haijui muda na fedha haijui kuchoka. Fedha ipo tayari kuzunguka masaa 24 kwa siku, siku saba za wiki na mwaka mzima.
Usilaze fedha zako, badala yake chagua kuziwekeza kwenye uwekezaji bora, ambao unazalisha kipato. Hapa sasa unakuwa unatengeneza kipato hata kama haupo moja kwa moja. Na huu ndiyo uhuru wa kweli wa kifedha, kuweza kutengeneza kipato bila ya uwepo wako wa moja kwa moja.
Rafiki, usikubali wewe au watu wanaokuzunguka kuweka ukomo kwenye kipato chako. Katika wakati wowote wa maisha yako, unahitaji kuwa unatengeneza kipato zaidi. Usiwe mtu wa kuridhika haraka na kukubali ukomo kwenye kipato chako. Tengeneza mifereji zaidi, toa thamani zaidi, dai kulipwa zaidi, fikiria mara kumi ya kipato ulichonacho na wekeza vizuri.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha