Kuna mambo mengi sana unayoweza kufanya kwenye biashara yako, lakini huwezi kufanya yote, huna muda huo wala nguvu hizo.
Hivyo unahitaji kuwa na kipaumbele wa nini ufanye na nini usifanye, kwenye vile utakavyofanya, nini uanze kufanya kabla ya kingine.
Kwenye kuchagua kipi ufanye, fanya kile ambacho unaweza kupima kwenye biashara yako. Kama kitu huwezi kukipima, au huna muda wa kupima, ni bora usikifanye, maana hakitakusaidia.
Kama kuna njia mpya umetumia ya kutangaza biashara yako, pima ni wateja wangapi wapya wanakuja kwa kutumia njia hiyo.
Kama ni watu wa mauzo unawatumia kuuza biashara yako, pima kila mtu anauza kiasi gani.
Kama ni mafunzo umetoa kwa wafanyakazi wa biashara yako, pima mafunzo hayo yameleta utofauti kiasi gani.
Kama kuna mbinu za kuongeza mauzo, au kupunguza gharama kwenye biashara yako, pima matokeo yake kwenye biashara yako.
SOMA; BIASHARA LEO; Tengeneza Mfumo Wa Biashara Moja Kusimama Kabla Hujaenda Nyingine…
Biashara haiwezi kukua kama haipimwi, hivyo lazima uweze kupima kila unachofanya kwenye biashara yako.
Na kwenye fedha, ndiyo muhimu mno, hesabu fedha kwenye biashara yako kila siku, kila wakati jua fedha ya biashara yako iko wapi, jua kiwango cha mtaji ni kiasi gani, gharama za kuendesha biashara ni kiasi gani, na faida unayopata ni kiasi gani.
Kama umewahi kusikia watu wanasema chuma ulete kwenye biashara, basi ni uzembe wa wao kutokupima na kuhesabu kila kitu, kuendesha biashara kwa mazoea na wasijue fedha ya biashara iko wapi.
Pima kila kitu na usiruhusu chochote kifanyike kwa mazoea au kwa sababu ndivyo watu wamekuwa wanafanya. Pima kila kitu, pima kila kitu, kama huwezi kupima ni bora usifanye, haina manufaa kwako wala kwa biashara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,