Maisha ni mfululizo wa changamoto, kwamba ukimaliza changamoto moja, unakuwa umekaribisha changamoto nyingine.
Dhana ambayo wengi wamekuwa nayo ni kwamba wanaweza kumaliza kabisa changamoto zote ambazo wanazo, kitu ambacho siyo kweli.
Ndiyo maana njia yoyote ya mkato unayokutana nayo ya kutatua chochote kinachokukwamisha, haitafanya kazi. Kwa sababu njia ya mkato inafikiri changamoto ni moja, lakini kwa uhalisia changamoto zinaongozana, ukitatua moja inafuata nyingine.
Hivyo njia pekee ya kuzishinda changamoto za maisha, ni kwa kuwa imara wewe kwanza, kiasi kwamba changamoto yoyote unayokutana nayo, unajua unaweza kuikabili. Na hata kama hutaweza kuishinda kwa uwezo wako, basi haitakuangusha na utaacha muda uishinde changamoto hiyo.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hakuna Kisichokuwa Na Changamoto.
Hakuna kitu kimoja utakachofanya kwenye maisha yako ambacho kitamaliza kabisa changamoto. Ila kwa wewe kuwa imara utajiondolea hofu ya kuangushwa na kila aina ya changamoto.
Na hili watu wamekuwa hawalielewi mpaka pale wanapopata fedha, mtu anapokuwa hana fedha huwa anafikiri akipata fedha nyingi basi changamoto zake zote za fedha zitaisha. Anashangazwa pale anapopata fedha ndiyo changamoto zinakuwa kubwa zaidi. Hapa ndipo wengi hujiambia kwamba bora wakiwa hawana fedha wanakuwa na amani kuliko wakiwa na fedha nyingi.
Ukweli ni kwamba fedha haina tatizo lolote, ila wewe unapokuwa na fedha nyingi zaidi, unakaribisha changamoto zaidi. Hivyo ni vyema kabla hujapata fedha nyingi, uwe umeshajijenga na kuwa imara, kiasi cha kuweza kushinda kila aina ya changamoto.
Maisha siyo safari ya kushinda changamoto moja kubwa halafu baada ya hapo maisha yakawa raha mustarehe kama zile hadithi tulikuwa tunaambiana utotoni. Bali maisha ni mfululizo wa changamoto ambazo zitaendelea kuibuka kila unapopiga hatua kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,