Rafiki yangu mpendwa,

Kama walivyosema wahenga, fedha ni sabuni ya roho, fedha ndiyo kitu pekee ambacho kila mtu anakipenda na kina matumizi mazuri kwake. Vitu vingine vyote kila mtu ana upendeleo binafsi. Mfano kuna watu wanakula nyama na kuna ambao hawali nyama. Kuna wanaokunywa pombe na kuna wasiokunywa pombe. Lakini fedha, fedha ni nzuri kwa wote, fedha inaweza kufanya mazuri kwa kila mtu.

Lakini fedha zimekuwa na changamoto nyingi sana. Na changamoto zote za fedha zimegawanyika kwenye makundi matatu. Kundi la kwanza ni changamoto ya kipato, hapa wengi wamekuwa na kipato kidogo ukilinganisha na mahitaji yao. Changamoto ya pili ni matumizi, hapa wengi wamekuwa na matumizi makubwa kuliko kipato hivyo kujikuta wanaingia kwenye madeni. Na changamoto ya tatu ni kuizalisha fedha, hapa wengi wamekuwa wanashindwa kuitumia fedha waliyonayo kupata fedha zaidi. Ukiweza kutatua changamoto hizi tatu za fedha, hutakuwa na tatizo la fedha kwenye maisha yako.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto, ambapo tunapeana ushauri muhimu wa jinsi ya kuvuka changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa tunayopigania kwenye maisha yetu.

Kwenye makala ya leo, tutakwenda kupata ushauri kuhusu eneo la fedha. Na kabla hatujapata ushauri wenyewe, tupate maoni aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

Naomba ushauri kuhusu jinsi ya 1. kudhibiti mzunguko wangu wa pesa (Cash flow). Naona nina tatizo la pesa kutokukaa mfukoni 2. Nina biashara ya stationery, mwaka wa pili huu sioni faida naomba mwongozo. – Maxmillian C.

Kama alivyouandikia msomaji mwenzetu Maxmillian, changamoto ya fedha imekuwa kikwazo kwa wengi kufanikiwa. Na kama nilivyoeleza kwenye utangulizi, changamoto kuu za fedha ni tatu.

Kwenye makala ya leo, nakwenda kukushirikisha hatua tatu muhimu za kuondokana na changamoto za kifedha, kwa kutumia changamoto za mwenzetu Max.

HATUA YA KWANZA; ONGEZA SANA KIPATO CHAKO.

Hatua ya kwanza unayopaswa kuchukua, popote pale ulipo sasa, bila ya kujali kipato chako ni kidogo au kikubwa kiasi gani, unahitaji kuongeza kipato chako.

Zoezi la kuongeza kipato ni zoezi endelevu, ambalo halina mwisho kama bado upo hai. Hupaswi kuzoea kipato ambacho unacho, hupaswi kujiwekea ukomo kwenye kipato chako.

Ongeza kipato chako na utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zako za kifedha. Kama upo kwenye ajira, ambapo kipato kinaongezeka taratibu na baada ya muda mrefu, kuwa na biashara ya pembeni inayokuingizia kipato. Kama tayari upo kwenye biashara, wafikie wateja wapya na uza bidhaa na huduma nyingi zaidi.

Ongeza kipato chako na safari yako ya kupunguza changamoto za kifedha itakuwa pazuri.

SOMA; Maana Halisi Ya Dhana Ya Kujilipa Wewe Mwenyewe Kwanza Kabla Hujafanya Matumizi Ya Fedha Zako.

HATUA YA PILI; WEKA AKIBA KABLA YA MATUMIZI.

Tabia ya matumizi ni moja, huwa yanaongezeka kadiri kipato kinavyoongezeka. Ndiyo maana watu wengi huwa wanakuwa na kipato kikubwa, lakini bado hakitoshelezi matumizi yao. Kwa sababu matumizi yanaongezeka kadiri kipato kinavyoongezeka.

Unahitaji kuwa makini ili matumizi yasimeze ongezeko lako la kipato. Na unachohitaji kufanya ni kuweka akiba kabla ya matumizi. Kabla hujatumia fedha yoyote unayoipata, weka pembeni sehemu ya fedha hiyo kwanza.

Kiwango kizuri cha kuweka akiba, na unachoweza kuanza nacho ni asilimia kumi ya kipato chako. Kila unapopata fedha, asilimia kumi ya fedha hiyo iweke pembeni, usiiguse kabisa, hata kama unakufa njaa. Hii ndiyo hazina yako, hiyo ndiyo mbegu ya kukutoa kwenye umasikini. Mkulima makini huwa hali mbegu.

Kile kiasi unachoweka pembeni, unakiwekeza au kukizungusha kwenye shughuli zinazozalisha faida zaidi. Usikae nacho tu kama akiba kwa muda mrefu, bali kitumie kuzalisha fedha zaidi na zaidi.

HATUA YA TATU; ONGEZA FAIDA KWENYE BIASHARA YAKO.

Kama una bishara, ambayo una mteja mmoja anayenunua, basi jua una mgodi wa dhahabu, ambao bado hata haujaguswa. Hivyo unaweza kuchimba dhahabu na utajiri utakavyo kwenye biashara yako.

Biashara yoyote ile, unaweza kuongeza faida mara dufu kwa kufanya mambo haya matatu;

Moja; ongeza idadi ya wateja wanaoijua biashara yako na anaonunua. Hakikisha unawafikia watu wengi sana na biashara yako na wanajua kwa hakika biashara yako inawezaje kuwasaidia kupata wanachotaka na maisha yao kuwa bora.

Mbili; ongeza kiwango na kiasi cha manunuzi ambacho wateja wanafanya kwenye biashara yako. usikubali mteja anunue mara moja halafu asije tena. Usikubali mteja aje kwako na anunue kile tu alichopanga kununua. Mfanye mteja anunue mara nyingi kwenye biashara yako, na mteja anapokuja kwenye biashara yako, hakikisha unamuuzia vitu vingine vitakavyomsaidia zaidi.

Tatu; punguza gharama za kuendesha biashara yako na ongeza kiasi cha faida kwenye kila unachouza. Kama unachouza ni muhimu kwa wateja wako, unaweza kuongeza bei ili kupata faida zaidi. Pia kwa kudhibiti gharama zako za kuendesha biashara, utaweza kuongeza faida mara dufu.

Rafiki, hizo ndiyo hatua unazopaswa kuanza kuchukua sasa, kama bado ulikuwa hujaanza kuchukua, ili kusimamia mzunguko wako wa fedha, kutuliza fedha yako na kuongeza faida kwenye biashara.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji