Upo usemi kwamba yai likipasuliwa kwa nguvu ya nje kiumbe aliyepo ndani anakufa. Lakini likipasuliwa kwa nguvu ya ndani, kiumbe aliyepo ndani anaishi. Ni usemi unaoeleza vizuri sana namna asili inavyofanya kazi.
Kila kiumbe hai, kina nguvu ya uhai ndani yake, kina nguvu ya ukuaji ndani yake. Na ili kiumbe hai aweze kufikia anakopaswa kufikia, ukuaji lazima uanzie ndani na siyo nje.
Kama ukuaji wa kiumbe hai utaanzia ndani, unakuwa ukuaji imara na wa kudumu. Lakini kama ukuaji utakuwa wa nje, wa kulazimisha, ukuaji huo hautakuwa imara na hautadumu.
Unaweza kuona hili kwa kuangalia vitu vinavyokua kwa asili na vinavyokua kwa kuchochewa. Vinavyokua kwa asili vinakua taratibu lakini vinadumu sana. Lakini vinavyokua kwa kuchochewa, vinakua haraka na kupotea haraka.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Jukumu Muhimu Kwenye Maisha Yako Ambalo Huenda Bado Hujalifanya.
Rafiki yangu, ili kupata mafanikio ya kweli, ili kupiga hatua kubwa na zitakazodumu kwenye maisha yako, tengeneza ukuaji wa ndani. Anza kujitengeneza na kujikuza zaidi kutokea ndani yako na siyo nje.
Pata msukumo wa kutaka kuwa bora zaidi kila siku kwa sababu unajua unaweza kuwa bora, kwa sababu unapanga kwenda mbali zaidi. Usitake kukua kwa sababu kuna wengine wanakua, au unataka kuwaonesha wengine kwamba na wewe unaweza kukuza zaidi. Kwa njia hiyo utakua, lakini ukuaji wako hautadumu sana.
Ukuaji halisi na wa kudumu unaanzia ndani yako, kazana kukua zaidi kila siku na isitokee siku ukajiambia umeshamaliza kukua. Kila siku kwako ni siku ya ukuaji.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,