Rafiki yangu mpendwa,

Mwandishi mmoja aliwahi kusema kwamba, binadamu huwa tunazaliwa na hofu mbili pekee, hofu ya kuanguka chini na hofu ya sauti kali. Ndiyo maana mtoto aliyezaliwa leo, ukimshika na kutaka kumwachia atakung’ang’ania sana. pia ukitoa sauti kali, atashtuka sana.

Hofu nyingine zote ambazo watu wanazo kwenye maisha yao hawakuzaliwa nazo, bali wamezitengeneza wao wenyewe kwenye akili zao. Mazingira waliyokulia, malezi waliyopata, elimu waliyopata vinakuwa vimetengeneza hofu fulani ndani yake.

Kwa mfano mtoto aliyekulia kwenye familia ya wafanyabiashara, na mara kwa mara akawa anahusishwa kwenye biashara za wazazi wake, hawezi kuwa na hofu ya kuanzisha biashara, kwa sababu amekuwa anawaona wazazi wake wakifanya biashara kila siku.

Lakini mtoto aliyezaliwa kwenye familia ambayo hakuna wafanyabiashara, au akamwona mzazi akijaribu kiashara na akashindwa, atakuwa na hofu kubwa sana ya kuingia kwenye biashara. Hofu yake ya kushindwa kwenye biashara itakuwa kubwa kiasi cha kumzuia asiweze kuchukua hatua.

Hofu ya kushindwa ni moja ya hofu ambazo watu tunajitengenezea wenyewe. Hofu nyingine ni kama hofu ya kifo, hofu ya kukataliwa, hofu ya kupoteza na hata hofu ya wengine watakuchukuliaje.

Katika hofu hizi za kujitengenezea wenyewe, kuna aina ya tofauti ya hofu, ambayo imewafanya wengine kuwa watumwa na kushindwa kuishi maisha yenye maana kwao.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Hofu hiyo ni HOFU YA KUPITWA. Hii ni aina ya hofu ambayo unaona kuna kitu kinakupita wewe. Kila unapowaangalia wengine, unaona kama maisha yao ni bora na mazuri kuliko yako. Unaona wao mambo yao ni mazuri kuliko yako.

Hofu hii imekuwa mbaya sana kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii, ambayo watu wanachagua matukio mazuri ya maisha yao na kuyaweka kwenye mitandao ya kijamii, lakini yale mabaya hawayaweki. Wale wasiojua, wanaona mtu anayeweka matukio yake mazuri kwenye mitandao ya kijamii hayo ndiyo maisha yake ya kila siku.

Hofu ya kupitwa ni mateso ya kisaikolojia ambayo watu wanajitengenezea wao wenyewe. Ni njia ya kutengeneza picha mbaya kabisa kwenye fikra zetu kuhusu hali zetu ukilinganisha na hali za wengine. Ni kufikiri kwamba kila mtu ana maisha mazuri mara zote ila wewe tu ndiyo maisha yako hayaeleweki. Ni kufikiri kwamba kama na wewe utafanya wanachofanya wao, basi maisha yako yatakuwa bora kama yao.

SOMA; Jifunze Na Wafundishe Wengine Kuthamini Kazi Yako (Na Maamuzi Muhimu Sana Ya Kufanya Kuhusu Kazi Yako Leo).

Njia pekee ya kuondokana na hofu hii na kuzuia isikufanye kuwa mtumwa wako na wa wengine, ni kuacha kuendeshwa na hisia na kuanza kufikiri sawasawa. Unapofikiri sawasawa unajua kabisa kwamba hakuna mtu ambaye maisha yake yamenyooka tu, ambaye hakutani na vikwazo au changamoto. Unafikiri kwa kina na hata kujaribu kufuatilia maisha halisi ya wachache wanaokufanya uone wewe uko nyuma, unakuta kuna mengi ambayo hukuyajua.

Unapaswa kujua kwamba hakuna kitu chochote ambacho kimekamilika na kipo sahihi mara zote. Kwamba hakuna anayeyaendesha maisha yake kwa ukamilifu wa hali ya juu, ambaye hakuna anachokosa. Kila maisha yana vikwazo na changamoto zake. Na wale unaowaangalia na kutamani maisha yao yangekuwa kama yao, huenda ungepewa maisha yao wala usingeweza kuyaishia.

Elewa kwamba kila kitu kwenye maisha kinakuja na gharama zake. Na chochote unachotaka kupata, jua kuna gharama unapaswa kulipa ili kupata. Na siyo kila aina ya gharama wewe unaweza kuwa tayari kuilipa, kwa sababu siyo kila kitu kinaendana na wewe. Hivyo kabla hujaendelea kujiambia kwamba kuna kitu unakosa kwa sababu maisha yako hayapo kama ya wengine, jikumbushe kwamba kuna gharama za kulipa kwenye kila maisha.

Mwisho kabisa, hakuna chochote unachokosa kama umeshajua nini unataka kwenye maisha yako na unafanyia kazi kupata kile unachotaka. Ukishajua unachotaka, akili yako yote, mawazo yako yote, nguvu zako zote, muda wako wote na juhudi zako zote unapaswa kuelekeza kwenye kile unachotaka. Acha kukimbizana na kila unachoona kwa wengine. Chagua kufanyia kazi yale muhimu kwako na utakuwa na maisha bora kabisa.

Wakati unajiambia kwamba kuna kitu unakosa kwa sababu umeangalia wengine na kuona wana kitu ambacho wewe huna, jua wengine pia kuna kitu wanajiambia wanakosa wanapokuangalia wewe na kuona vile ambavyo wao hawana. Usipoteze muda wako na nguvu zako kwenye hofu ya kukosa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha