Kwa wale ambao hawajui ni biashara gani wafanye,

Wale ambao wanataka kuingia kwenye biashara lakini hawajui waanzie wapi,

Na hata kwa wale ambao wanataka kuingia kwenye biashara lakini hawana mtaji wa kuanza biashara,

Zipo njia mbili za kuingia kwenye biashara na hata kuanza biashara yoyote.

Njia ya kwanza ni kununua halafu kuuza, au hata kutengeneza na kuuza, au kufikiri na kuuza. Hapa unaanza na kitu ambacho unaweza kukinunua na kukiuza, au unaweza kukitengeneza au hata kuja na wazo unaloweza kuuza. Ni kitu gani ambacho watu wanahitaji na unaweza kuwapatia, kinunue, au kitengeneze kisha wauzie.

SOMA; BIASHARA LEO; Vitu Ambavyo Havilipi Moja Kwa Moja Kwenye Biashara Yako.

Njia ya pili ni kuuza halafu kununua au kuuza kisha kupata fedha ya kutengeneza na kuuza zaidi. Hapa kwa wale ambao hawana fedha ya kuanza kununua, inabidi wauze kwanza, wauze kile walichonacho kisha wapate fedha ya kununua au kutengeneza na kuuza. Hivyo unaweza kuuza ulichonacho sasa, ambacho hutumii au hakina manufaa, kisha ukapata fedha ya kununua na kuuza zaidi. Pia unaweza kuuza kitu ambacho mwingine anauza lakini hajalifikia soko vizuri, na ukapata fedha za kuendelea kununua na kuuza.

Rafiki, usipoteze muda wowote kufikiria ufanye biashara gani au uanzeje biashara. Wewe jiulize tu ni kitu gani unaweza kununua na ukauza. Na kama huna uwezo wa kununua, basi jiulize kipi unaweza kuuza na ukapata fedha ya kukuwezesha kununua na kuuza.

Usiifanye biashara kwako kuwa ngumu zaidi kwa kujipa mawazo ambayo hayakupelekei kuchukua hatua. Nunua na uuze, au uza kisha ununue, halafu uuze.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha