Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 30 limekuwa juma jema kabisa kwa kila mmoja wetu. Ni imani yangu kwamba ndani ya juma hili, umeweza kupiga hatua kubwa kuelekea kwenye mafanikio yako. Na ninaposema hatua kubwa namaanisha kile hasa ulichofanya na siyo maandalizi. Kwa sababu nilichojifunza kwa wengi, ni wanatumia muda mwingi kujiandaa kuanza kuliko kuanza. Leo nataka nikuambie kwamba, kama unatumia muda mwingi kujiandaa kuanza, hujiandai, bali unajificha.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, tunaishi kanuni moja rahisi sana ya kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Kanuni hiyo ni MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MATOKEO MAKUBWA. Kama hutaki kujifunza chochote kuhusu mafanikio, kama hutaki kujua siri nyingine yoyote, basi shika hiyo na fanyia kazi kila siku.

Kwenye kila unachotaka kufanya, kwanza pata maarifa sahihi juu ya kitu hicho, kijue kwa undani, halafu chukua hatua kubwa sana, zaidi ya wengine walivyozoea kuchukua. Halafu sasa ndiyo unaweza kupata matokeo makubwa sana kupitia hicho unachofanya.

MIMI NI MSHINDI

Karibu rafiki kwenye TANO ZA JUMA, ambapo nakuwa nimekukusanyia mambo matano muhimu ya kujifunza na kuchukua hatua ili maisha yako yaweze kuwa bora sana.

Karibu ujifunze mambo haya matano, uyatafakari kwenye maisha yako, uchague kuchukua hatua na kisha uweze kupata matokeo bora kabisa.

#1 KITABU NILICHOSOMA; SULUHISHO LA KIROHO, MAJIBU YA CHANGAMOTO KUBWA ZA MAISHA.

Juma hili moja ya vitabu nilivyosoma ni kitabu cha Deepak Chopra kinachoitwa SPIRITUAL SOLUTIONS; ANSWERS TO LIFE’S GREATEST CHALLENGES.

Chopra ni mwalimu wa kiroho wa zama zetu, ambaye ameandika na kufundisha sana kuhusu imani, hasa imani ndani ya mtu binafsi, kabla ya kuweka dini na vitu vingine. Kwenye ulimwengu tunaoishi sasa, ambapo mamlaka za kidini zinapoteza nguvu, watu wengi hawana imani thabiti, wengi hawapo vizuri kiroho na ndiyo maana wengi wanakutana na changamoto kubwa sana kwenye maisha yao.

Chopra anatuambia kwamba, kila changamoto tunayokutana nayo kwenye maisha, suluhisho lake linaanzia ndani yetu, na linaanzia kwenye imani yetu. Na kweli unapoangalia kila kitu kwenye maisha yako, kama ukiwa muwazi kabisa, kama utaondoa kutafuta sababu, utaona jinsi ambavyo wewe mwenyewe umechangia kwenye tatizo uliloingia.

Hakuna anayeweza kubisha kwamba maisha hayana changamoto, maisha yana changamoto nyingi, maisha yanaweza kuonekana magumu sana. Lakini maisha huwa yanakuwa magumu zaidi kwa wale wasioelewa wapo hapa duniani kwa ajili ya nini na wanaenda wapi. Wale ambao wanasukuma tu maisha, wanaishi leo wakisubiri kesho, kila kinachotokea kwenye maisha yao ni shida kubwa.

Lakini kwa wale waliokua kiroho, wale wenye imani ndani yao, wanaojua wapo hapa duniani kwa ajili ya nini na wanajua wanaenda wapi, kila linalotokea wanajua ni hatua kuelekea kule wanakotaka kufika.

Ngazi tatu za utambuzi kwenye matatizo.

Kwenye kitabu chake, Chopra anatushirikisha kwamba kuna ngazi tatu za utambuzi tunapokutana na matatizo na changamoto. Na kadiri unavyokwenda ngazi ya juu, ndivyo changamoto zinaacha kuwa kikwazo kwenye maisha yako.

Ngazi ya kwanza ya utambuzi ni utambuzi wa kusinyaa. Hapa Chopra anatuambia mtu anapokutana na tatizo, anasinyaa kwenye ngazi ya tatizo hilo. Kwa maneno mengine mtu anakuwa mdogo kwenye ngazi ya tatizo. Mtu anakuwa ndiyo tatizo lenyewe, na kila anapokazana kutoka kwenye tatizo hilo ndiyo tatizo linazidi kuwa kubwa. Utagundua upo kwenye ngazi ya kusinyaa pale kila unapochukua hatua, tatizo linazidi kuwa kubwa kuliko mwanzo. Hii ndiyo ngazi ambayo wengi wanaendesha maisha yao, na ndiyo maana wengi matatizo yao hayaishi.

Ngazi ya pili ni utambuzi wa kupanuka. Hapa Chopra anatuambia, mtu anakuwa juu ya tatizo, mtu anatanuka na kukua zaidi ya tatizo, anaweza kuliona tatizo na suluhisho la tatizo linaonekana kirahisi. Kwenye ngazi hii ya kupanuka, mtu anaacha kujiona ndani ya tatizo na anaweza kuliona tatizo tofauti na yeye. Utagundua kwamba upo kwenye ngazi hii pale unapojiona hujakwama kwenye tatizo, una tatizo na unaelewa ni tatizo na umeshaona njia ya kuondoka kwenye tatizo hilo. Katika ngazi hii ya utambuzi, wakati mwingine suluhisho linajionesha lenyewe na nguvu usizoweza kuzielezea zinakusaidia kutatua tatizo lako.

Ngazi ya tatu ni utambuzi kamili. Hii ni ngazi ya utambuzi ambapo hakuna tatizo linalokusibu. Kila changamoto unayokutana nayo ni fursa kwako kupiga hatua zaidi. Kwenye ngazi hii, unajiona kabisa upo upande mmoja na nguvu kubwa inayoendesha dunia. Hii ndiyo ngazi ya utambuzi ambapo mtu unakuwa umekua sana kiroho, kiasi kwamba hakuna chochote kinachoweza kuwa kikwazo kwako kupata unachotaka. Hata kama hupati kile unachotaka, mchakato mzima wa kukipata unakuwa furaha na mafanikio kwako. Kwenye ngazi hii ya utambuzi, hakuna popote unapokwama, unapokutana na changamoto unafurahia ukijua ni sehemu ya kawaida ya safari. Hulalamiki wala kujitetea kwa vyovyote. Unayakubali majukumu yako na kuchukua hatua.

Rafiki, kabla hatujaendelea, hebu jiulize kwanza swali hili, upo kwenye ngazi ipi ya utambuzi? Na hapa kuwa mkweli kwako binafsi, usijiambie kile unachotaka wengine wakuone, angalia matatizo na changamoto kubwa unazopitia kwenye maisha yako, kisha angalia jinsi unavyozifanyia kazi, na jipe jibu unazifanyia kazi kwenye ngazi ipi. Kisha kazana kupanda ngazi ya juu zaidi ili tatizo lolote lisikurudishe nyuma.

Kila mstari wa kitabu hichi, ukiusoma kuna kitu unajifunza, ambacho unaweza kufanyia kazi. Ila kwa hapa, nataka nimalizie kwa kukushirikisha maeneo matano ya kubadili kwenye maisha yako ili uweze kupata suluhisho la matatizo na changamoto unazopitia kwenye maisha.

Chopra anatuambia matatizo mengi tunayokutana nayo, yanaanzia kwenye maeneo haya matano. Ina maana kwamba, kama mtu utabadili maeneo haya matano, hakuna tatizo lolote litakalokuwa kikwazo kwenye maisha yako.

Eneo la kwanza; mtazamo.

Matatizo mengi unayokutana nayo kwenye maisha yako ni kutokana na mtazamo ambao unao juu ya kile kinachotokea. Mengi unayoona ni matatizo makubwa na huwezi kuyavuka, ni kwa namna unavyoyatazama. Hivyo changamoto yoyote unayokutana nayo, kabla hujaiogopa, anza kwanza kuhoji mtazamo wako juu ya changamoto hiyo. Jaribu kuangalia wengine waliokutana na changamoto hiyo na hatua walizochukua, utaona jinsi ilivyo rahisi kuchukua hatua.

Eneo la pili; imani.

Imani ulizonazo, zinachangia sana kwenye matatizo na changamoto unazokutana nazo. Ubaya wa imani ni kwamba mtu unaweza hata usijue kama ni imani iliyopo ndani yako, hasa kama ni kitu umezoea kufanya. Unahitaji kubadili imani yako juu yako mwenyewe na kile unachokutana nacho. Mambo mengi unayojiambia huwezi siyo kweli kwamba huwezi, ila hujawahi kujaribu kufanya. Kuwa mtu wa kujaribu na utavuka changamoto nyingi.

Eneo la tatu; ubashiri

Kitu kingine unachopaswa kufanyia kazi kwenye changamoto ni ule ubashiri unaokuwa nao kutokana na kile kinachotokea. Sisi binadamu ni viumbe ambao tunapenda kupata sababu ya kwa nini kitu kimetokea. Na pale ambapo sababu hazipo wazi, huwa tunajaribu kutengeneza sababu zetu wenyewe, kwa kuunganisha alama ambazo hata hazina uhusiano. Unapokutana na changamoto yoyote, iangalie kama changamoto na acha kutengeneza ubashiri wowote. Acha kujaribu kuunganisha vitu ambavyo havina uhusiano, angalia changamoto na unatokaje kwenye changamoto hiyo.

Eneo la nne; matarajio.

Eneo lenye shida kubwa kwenye changamoto na matatizo ni yale matarajio ambayo mtu anakuwa nayo. Kadiri mtu anavyokuwa na matarajio makubwa, ndivyo maumivu yanavyokuwa makubwa pia. Lakini hili halimaanishi kwamba usiwe na matarajio kabisa, unachopaswa kujua ni kwamba, unapokuwa na changamoto yoyote, jaribu kwanza kuweka matarajio yako pembeni na chukua hatua kutatua changamoto hiyo. Unapoanza kuweka matarajio yoyote, hasa kutoka kwa wengine, unazidi kukuza changamoto yoyote unayokutana nayo.

Eneo la tano; hisia.

Huwa tunadhani kwamba tunafanya maamuzi kwa kufikiria, lakini ukweli ni kwamba maamuzi mengi huwa tunayafanya kwa hisia, halafu tunajiridhisha kwa kufikiria baadaye. Lakini wakati wa matatizo na changamoto, ni wakati wa kuwa makini sana kwa sababu hisia zinakuzuia kuona uhalisia wa mambo. Hivyo unapokuwa kwenye changamoto, tuliza kwanza hisia zako kabla hujafanya maamuzi yoyote, utajiepusha kuingia kwenye matatizo zaidi.

Rafiki, fanyia ngazi kupanda ngazi ya utambuzi kwenye changamoto unazokutana nazo, na fanyia kazi maeneo haya matano na utaanza kuziona changamoto na matatizo kama fursa kwako kukua zaidi badala ya kuona kama ukomo na kikwazo kwako kufanikiwa.

Matatizo na changamoto havitaisha kwenye maisha, hivyo usitake kutokukutana na vitu hivyo, badala yake kazana kuwa imara ili unapokutana navyo visiwe kikwazo kwako.

#2 MAKALA YA WIKI; NJIA SABA ZA KUPATA MTAJI WA KUANZA BIASHARA.

Sababu kwamba hujaingia kwenye biashara kwa kuwa huna mtaji ni sababu ya kizamani, iliyopitwa na wakati na isiyo na mashiko. Mtu angetumia sababu hii mwaka 1950 tungeweza kumwelewa. Lakini kutumia sababu hii mwaka 2018 na kuendelea, ni kutaka tu kujifariji, kutokutaka kuuangalia ukweli na kukwepa kuweka kazi.

Kwa wale ambao wanajidanganya na sababu hii, wiki hii nilikuandikia makala ya kukuamsha kutoka kwenye huo usingizi. Isome makala na kama ninavyosema, chukua hatua. Makala ya wiki hii ni hii hapa, unaweza kufungua kuisoma; Usisingizie Fedha Tena; Njia Saba Za Kupata Mtaji Wa Kuanza Biashara Hata Kama Huna Pa Kuanzia Kabisa. (https://amkamtanzania.com/2018/07/27/usisingizie-fedha-tena-njia-saba-za-kupata-mtaji-wa-kuanza-biashara-haya-kama-huna-pa-kuanzia-kabisa/)

#3 #TUONGEE PESA; MISINGI MIKUU MIWILI YA UWEKEZAJI.

Watu wengi wasiojua vizuri kuhusu uwekezaji wamekuwa wanasita kuingia kwenye uwekezaji pale wanapoona faida wanayopata ni ndoto. Na hata wanapoingia huwa wanakosa uvumilivu pale wanapoona faida wanayopata ni ndogo kuliko wangetumia fedha hiyo kwa shughuli nyingine.

Na hii ni kweli kabisa, mfano kama una milioni moja, ukiamua kuizalisha wewe mwenyewe kwenye biashara yoyote unayochagua kufanya, ndani ya mwaka utaweza kupata faida ya zaidi ya asilimia 20. Lakini ukichukua fedha hiyo na kuiwekeza, labda kwenye masoko ya mitaji au uwekezaji mwingine, kiasi kikubwa sana unachoweza kupata kwa mwaka ni asilimia 7, uwekezaji mwingi utakupa chini ya asilimia 5 kwa mwaka.

Kwa fikra hizi, wengi huona bora wazalishe fedha zao wenyewe badala ya kuwekeza. Na mimi mara zote nimekuwa nakuambia, unahitaji kuzalisha fedha zako na unahitaji kuwekeza pia. Kwa sababu uwekezaji huangalii ndani ya mwaka mmoja, bali unaangalia miaka 10, 20 na mpaka 50 ijayo.

Misingi miwili mikuu ya uwekezaji ni MUDA NA MSIMAMO.

MUDA; unahitaji kuanza mapema na unahitaji kuendelea kuwekeza na kuwa na subira kwa sababu matunda ya uwekezaji utayavuna baada ya muda mrefu. Hivyo unapoanza kuwekeza, fikiria miaka kuanzia kumi na kuendelea ijayo, usitake kutumia uwekezaji kama sehemu ya kupata fedha za haraka, hutapata.

MSIMAMO; Unahitaji kuchagua unawekeza maeneo gani na kuchagua kiwango utakachowekeza kila mwezi na kisha kufanya hivyo. Unahitaji kuwa na msimamo kwenye aina ya uwekezaji na kiasi unachowekeza mara kwa mara kama unataka kunufaika na uwekezaji wako miaka mingi ijayo.

Simamia misingi hiyo miwili muhimu kwenye uwekezaji, anza mapema, weka mipango ya muda mrefu na kuwa na msimamo.

Na kwa wale wanaosema hawawekezi kwa sababu faida ni ndogo, jua huangalii faida ya leo, bali unaangalia faida ya miaka 30 ijayo, ambapo hutakuwa na nguvu za kupambana kama ulivyonazo sasa, na hapo faida uliyoiona ndogo leo, itakuwa imezaliana kwa kiasi kikubwa sana.

Zalisha fedha zako utakavyo, lakini usisahau kuwekeza, uwekezaji ni eneo muhimu sana la maisha yako kama upo makini na maisha yako.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; JINSI YA KUSOMA KITABU KIMOJA KILA MWEZI.

Huwa sipendi sana kulazimisha mfumo wangu wa maisha kwa watu wengine, kwa sababu najua kila mtu yupo huru kuchagua maisha gani aendeshe. Lakini huwa siwezi kuwavumilia wale ambao hawakosi malalamiko na visingizio. Mfano unamkuta mtu analalamika kwamba kazi yake haimlipi, kwamba biashara yake haifanyi vizuri miaka na miaka. Unamuuliza ni vitabu gani huwa unasoma anaishia kukutolea macho.

Mimi watu wa aina hii siwezi kuwavumilia, na huwa natumia maneno makali kwao, kwamba hawajui nini wanataka kwenye maisha yao, wanaenda enda tu. Kama umeridhika na maisha yako kama yalivyo, kama huna mpango wa kupiga hatua zaidi ya hapo ulipo, hukupaswa hata kuwa unasoma hapa. Lakini kama unasoma hapa, najua kitu kimoja kuhusu wewe, unataka kupiga hatua zaidi, hujaridhika na hapo ulipo sasa.

Na kwa kuwa upo hapa sasa nikuambie hili, kama hujawahi kusoma kitabu chochote ukamaliza, kama ndani ya mwaka mmoja unasoma vitabu chini ya kumi, hakuna kinachoweza kukusaidia kutoka hapo ulipo sasa. Ninachoweza kusema ni kwamba umekwama hapo ulipo na umetaka mwenyewe.

Kama unataka kupiga hatua ni lazima usome vitabu rafiki, NI LAZIMA, siyo ombi. Nisisitize tena, ni lazima. Lakini wengi wana sababu zisizoisha kuhusu usomaji wa vitabu, wapo wanaosema hawana muda, wengine hawajui wapate wapi vitabu na kadhalika.

Nimekuandalia program rahisi sana kwako kuweza kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi, kwa kusoma KURASA KUMI TU ZA KITABU KILA SIKU. Kama umechoshwa na maisha unayoenda nayo sasa, kama unataka zaidi na bado hujawa kwenye program hii, nitumie ujumbe sasa hivi, kwa njia ya wasap, namba 0717396253 ujumbe uwe na maneno KURASA KUMI ZA KITABU. Tuma ujumbe kwenye wasap tu na nitakupa maelekezo zaidi.

Wito wangu kwako rafiki yangu, soma vitabu, hii ndiyo njia rahisi kabisa kwako kupiga hatua zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; JINSI YA KUFANYA YASIYOWEZEKANA.

“If you believe in what you are doing, then let nothing hold you up in your

work. Much of the best work of the world has been done against seeming

impossibilities.” – Dale Carnegie

kuna vitu ambavyo unataka kufanya kwenye maisha yako, lakini ukiangalia wanaokuzunguka hakuna aliyewahi kufanya. Na kama hiyo haitoshi, watu wanakuambia kabisa kwamba unachotaka kufanya hakiwezekani kabisa. hapa ndipo ndoto za wengi zinapofia na wanarudi kuishi maisha ya kawaida.

Usikubali ndoto yoyote uliyonayo ife kizembe kiasi hicho. Unachohitaji ni kuwa na imani isiyoyumbishwa juu ya kile unachotaka. Amini sana kwamba inawezekana, na unaweza kufanya, hata kama hakuna aliyewahi kufanya. Na usimsikilize yeyote anayekuambia haiwezekani. Kisha jua kiasi cha kazi unayohitaji kuweka ili kupata unachotaka, na kuwa tayari kuweka kazi hiyo. Kuwa tayari kujifunza kwa kila changamoto na vikwazo unavyokutana navyo.

Ukiweka vitu hivyo pamoja, imani isiyoyumbishwa, utayari wa kuweka kazi na kuchukulia changamoto na vikwazo kama sehemu ya kujifunza, hakuna kitakachoshindikana kwako.

Nakutakia maandalizi na mwanzo mwema wa juma namba 31 la mwaka huu 2018. Nenda kajifunze zaidi, nenda kachukue hatua kubwa ili uweze kupata matokeo bora kabisa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji