Ili biashara ifanikiwe sana, lazima ijijenge kama himaya, imiliki sehemu kubwa ya soko, iwe na wateja wanaoitegemea biashara hiyo, wanaoiamini na ambao wapo tayari kuwaalika wengine kuja kwenye biashara hiyo.
Hivyo badala ya kukazana kupata faida ya muda mfupi kwenye biashara yako, kazana kujenga himaya yako kibiashara, himaya ambayo itakuwa imara na hakuna wa kuiangusha.
Ili kujenga himaya imara kibiashara, unahitaji kufanya yafuatayo;
- Kazi ya himaya yako ya kibiashara ni kuwahudumia wateja wako, kuwapa kile ambacho wanahitaji kweli, kuwasaidia kutatua matatizo yao, kuwapa thamani kubwa zaidi kuliko fedha wanayolipa. Kwa njia hii wateja wataiamini biashara yako na kuichukulia kama eneo muhimu la maisha yao binafsi.
- Jali sana kuhusu wateja wa biashara yako, wale ndiyo marafiki zako wa kweli kwenye maisha, maana ndiyo wanaoweka chakula mezani kwako, ndiyo wanaokuvalisha, wanaoweka mafuta kwenye gari na wanaopeleka watoto wako shule. Lazima uwajali sana hawa marafiki wako wa kweli, uvae viatu vyao, ujiweke kwenye nafasi zao na ujiulize kama wewe ndiye ungekuwa unahudumiwa na wewe, kwa namna unavyowahudumia, ungeendelea kupata huduma kwako au ungeenda kwa wengine.
- Wasaidie wateja wako kujenga himaya zao pia. Kila mteja wako kuna himaya anakazana kujenga, inaweza kuwa familia yake, kazi yake au hata biashara yake pia. Unapompa mteja wako huduma, jua ni himaya gani anakazana kujenga, na kuwa wa msaada kwake katika kujenga himaya hiyo.
Kwa kujenga himaya imara, himaya ambayo watu hawawezi kuishi bila ya kuwepo kwenye himaya hiyo, unatengeneza wateja na marafiki wa kudumu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,