Ukweli wa maisha ni kwamba, kama unataka kuishi maisha ya mafanikio, basi lazima maisha yako yawe na madhara kwa wengine.

Lazima namna unavyoishi maisha yako kuibue hisia tofauti kwa watu tofauti. Lazima baadhi waone kama umechanganyikiwa na hujui nini unafanya. Wengine waone kwamba unajisumbua tu, hakuna mbali unaweza kwenda. Na pia wanapaswa kuwepo ambao wataona unaringa, unawadharau kwa kutofanya kama wanavyotaka wao. Wengine pia wanahitaji kukuonea huruma kwa namna unavyoendesha maisha yako, kwa sababu wao hawawezi kuyaendesha hivyo.

Kama unaishi maisha yasiyokuwa na madhara kwa wengine, jua unaendesha maisha ambayo siyo ya mafanikio. Utaishi hapa duniani kimya kimya na utaondoka hapa duniani kimya kimya. Hutamsumbua yeyote na mbaya zaidi hutapata makubwa.

Maisha yasiyo na madhara, ni maisha yasiyo na maana kuishi. Usitake kuwafurahisha wengine, au kuwa kama wengine wanavyotaka uwe. Wewe pekee ndiye unayejua ndoto zako kubwa na maono yako makubwa. Ukiwasikiliza wengine, utabaki na maisha yasiyo na madhara kwako wala kwa wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha