Rafiki yangu mpendwa,

Tunaishi kwenye zama bora sana tangu kuwepo kwa maisha hapa duniani. Zama ambazo mambo yamefanywa kuwa rahisi sana. Zama ambazo maarifa na taarifa vinapatikana kwa urahisi sana na yeyote anaweza kujifunza chochote anachotaka kujifunza bila ya kuzuiwa na yeyote au chochote.

Lakini pia wingi wa maarifa na taarifa hizi umekuwa hasara badala ya kuwa faida. Kelele pia zimekuwa nyingi kiasi kwamba mtu anashindwa kujua kitu gani achukue na kipi aache. Kadiri mtu anavyojikuta njia panda, kati ya mawazo mengi yanavyokinzana, ndivyo inavyokuwa vigumu kwake kuchukua hatua.

Leo nakupa siri moja muhimu ya kuweza kufanikiwa kwenye zama hizi tunazoishi ambazo zina mafuriko ya maarifa na taarifa. Ambapo unaweza kujifunza kitu kimoja kwa mwandishi au mwalimu mmoja, mwalimu mwingine akafundisha kitu kingine kinachopingana kabisa.

Unaweza kujifunza kwa mwalimu au mwandishi mmoja kwamba huwezi kufanikiwa bila ya kukopa, lazima utumie mikopo kuanzisha biashara ndiyo ufanikiwe. Mwandishi au mwalimu mwingine anakuambia kama unataka kufanikiwa kaa mbali sana na mikopo. Je yupi kati ya hao wawili yupo sahihi? Wote wanaweza kuwa sahihi na wote wanaweza kuwa wanakosea kulingana na hali unayopitia wewe.

Mwandishi mmoja anaweza kukuambia ondoka kwenye ajira haraka sana na kajiajiri kama unataka kufanikiwa. Mwingine anakuambia usiondoke kwenye ajira, badala yake anza biashara ukiwa ndani ya ajira hiyo, kisha ikuze huku ajira ikikusaidia kuendesha maisha. Je yupi yuko sahihi kati ya hawa wawili? Wote wanaweza kuwa sahihi na wote wanaweza kuwa wanakosea, kinachojali zaidi ni hali ambayo wewe unayo.

vitabu softcopy

Rafiki, nafikiri unaanza kuelewa nini nataka kukuambia hapa, kwenye kila kitu utakachojifunza kwa mwandishi au mwalimu mmoja, utajifunza kingine kinachopingana na hicho kabisa kutoka kwa mwalimu mwingine. Je unachukua hatua gani pale maarifa unayopata yanapingana?

Napoleon Bonaparte amewahi kunukuliwa akisema, jenerali mmoja mpumbavu anayeongoza kikosi ni bora kuliko majenerali wawili werevu wanaoongoza kikosi kimoja.

Na alikuwa sahihi sana, kwa sababu ni bora kufuata kauli moja hata kama siyo sahihi, kuliko kufuata kauli nyingi ambazo ni sahihi lakini zinachanganya. Ni bora kuchagua kufanya kitu kimoja hata kama siyo bora kabisa, kuliko kuhangaika na vitu vingi bora ambavyo hupigi hatua.

Hivyo rafiki yangu, ninachokuambia ni hichi, chagua mwandishi au mwalimu mmoja ambaye utamsikiliza na kufanya kile anachosema. Chagua mmoja ambaye kila anachokuambia utakichukua na kukifanyia kazi. Na hata kama kutakuwa na wengine wanaotoa maarifa yanayopingana na yule uliyemchagua, jifunze kwao, lakini fanya kile anachokuambia yule uliyemchagua.

Hili litakusaidia sana rafiki yangu, hata kama utakosea, lakini angalau utakuwa umefanya kitu na utakuwa umejifunza hivyo kuwa bora zaidi. Kuliko kukimbizana na maarifa mengi ambayo yanapingana na unashindwa kuchukua hatua, chagua mmoja ambaye utamsikiliza na kuchukua hatua.

Lakini hili halimaanishi kwamba hutajifunza kwa wengine, kamba hutasoma au kupata maarifa ya waandishi na walimu wengine. Utaendelea kujifunza na kuwa bora zaidi, lakini inapokuja kwenye maarifa yanayokinzana na kupingana, chagua kufanya kile anachosema mwalimu wako uliyemchagua.

Unapochagua mwalimu mmoja ambaye ndiye utakayejifunza kwake, hakikisha unajifunza kila kitu chake, hakikisha umesoma kila alichowahi kuandika kwenye maisha yake, hata kama hakihusiani na kile unachofanya. Kama ana vitabu hakikisha unasoma vyote. Kama kuna programu anazotoa hakikisha unashiriki zote.

Unachotaka ni kuzama kwenye maisha ya mwalimu wako uliyemchagua, unataka kufikiri kama anavyofikiri yeye, unataka kuuelewa msingi wake wa kufanya maamuzi, ambao utakusaidia sana wewe kwenye kufanya maamuzi pia.

Kumbuka, haijalishi kama mwalimu huyo ndiye aliye sahihi kuliko wengine wote, wala haijalishi kama ndiye anayejua zaidi. Wewe amua tu nani unaweza kumwamini, nani misimamo, imani na falsafa zake zinaendana na wewe unavyofikiri, kisha mchague yeye na zama kwenye kila ambacho ameshawahi kuandika au kufundisha.

Haya ni maamuzi bora sana ambayo utawahi kuyafanya kwenye maisha yako. Chagua sasa na amua kusimama na yule uliyemchagua huku ukiendelea kujifunza kutoka kwa wengine.

Mwisho kabisa, kama umeona ninafaa kuwa mwalimu wako, kama umenichagua kama mtu utakayenifuata kwenye maamuzi yoyote unayohitaji kufanya, basi nakukaribisha sana sana sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Watu wengi mmekuwa mnaniandikia jumbe na kunipigia simu mkitaka ushauri wa mambo mbalimbali, lakini nashindwa kuwahudumia vizuri kwa sababu hampo kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA na twende pamoja kwenye safari hii ya mafanikio.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Kama ulishachagua mwalimu mwingine unayemsikiliza na kumtumia kufanya maamuzi nashukuru pia kwa kuendelea kujifunza kupitia kazi zangu. Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku ujifunze, na unapofikia kufanya maamuzi, angalia mwalimu wako anasemaje kwenye eneo hilo kisha fuata kile mwalimu wako anasema.

Kumbuka; unapochagua mwalimu wa kumsikiliza na kumfuata haimaanishi kwamba hutakosea, utakosea sana, maana kila mtu anakosea. Inakusaidia tu kuweza kufanya maamuzi na kuchukua hatua badala ya kuhangaika na maarifa mengi ambayo huna cha kufanya.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Usomaji