Mahusiano yetu na wengine ni eneo muhimu sana la mafanikio yetu. Na kama Zig Zigler alivyowahi kusema, unaweza kupata chochote unachotaka kama utawasaidia wengi zaidi kupata kile wanachotaka.

Sheria ya dhahabu imekuwa inachukuliwa kama sheria muhimu sana kwenye mahusiano baina ya watu. Sheria hii inasema watendee wengine kama ambavyo ungependa wao wakutendee wewe.

Ni sheria nzuri sana, ya kuhakikisha kwamba huwafanyii wengine kile ambacho wewe hutaki kufanyiwa. Kama hutaki kuumia, basi unahakikisha huwaumizi wengine kwa namna yoyote ile.

Lakini sasa, sheria hii ina upungufu mmoja, wakati mwingine sisi wenyewe tupo tayari kujitesa, na tukaelewa kwa nini tunahitaji kujitesa, ili kupata kitu fulani cha maana kwetu. Lakini tukiweka mateso hayo kwa mtu mwingine, hataweza kuyahimili na ataona tunamnyanyasa.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Longevity Project (Ugunduzi Wa Kushangaza Kuhusu Afya Na Kuishi Miaka Mingi)

Hivyo ili kuvuka changamoto hiyo ya sheria ya dhahabu, tunapaswa kufuata sheria ya almasi, ambayo inasema wafanyie wengine vile ambavyo wao wenyewe wangependa kufanyiwa.

Kila mtu kuna namna anapenda kuchukuliwa, kuna vitu anapenda kufanyiwa, ni jukumu lako kujua hilo kwa wale ambao ni wa muhimu kwako kisha kuwafanyia hivyo.

Na usichanganye kutaka kumfurahisha kila mtu na kufanya kile ambacho mtu angependa kufanyiwa. Hapa unawatendea watu kile kilicho sahihi kwao, na ni wale watu wa muhimu zaidi kwako na siyo kila mtu. Mfano kama upo kwenye biashara, unahitaji kuwahudumia wateja kwa namna wanavyotaka wao, na siyo kwa jinsi unavyotaka wewe.

Kadhalika kwenye mahusiano mengine, unahitaji kujua upande wa pili unategemea nini na wewe kuweza kutoa kile kinachohitajika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha