Rafiki yangu mpendwa,
Kadiri maisha yanavyokuwa magumu, ndivyo watu wanavyokazana kutafuta nia rahisi na za mkato na za kurahisisha maisha. Sasa kwa kuwa matapeli na walaghai wanajua kila mtu anapenda urahisi, wanatumia njia hiyo kuwahadaa wengi na kuishia kuwatapeli fedha zao.
Nimekuwa naona watu wazuri wanaingia kwenye hii mitego, wanadanganywa mpaka wanaingia kwenye mikopo ili wapate fedha za kuwahi fursa fulani, mwishoni wanatapeliwa na wanabaki na madeni ya kulipa.
Kwa kuwa mimi rafiki yako nimejipa jukumu la kuhakikisha wewe unapata maarifa bora kabisa na yatakayokuwezesha kufanya maamuzi sahihi, leo nimekuandalia makala ya kukuwezesha kufanya maamuzi sahihi pale unapoambiwa kuna fursa nzuri kwako.
Siku hizi kumekuwa na fursa nyingi sana. Haipiti siku bila ya kupata ujumbe wa mtu anayeomba ushauri juu ya fursa fulani ambayo ameshirikisha, akitaka uhakika kutoka kwangu kama ni sahihi au la.
Huwa sipendi kuwatafunia watu kila kitu, naamini mtu anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yeye mwenyewe. Na pia siwezi kujua kila aina ya fursa kama ni sahihi au la, kwa sababu sina muda wa kujihusisha au kujaribu kila fursa. Hivyo nimekuwa na vitu vitano ambavyo nimekuwa naangalia kwenye fursa yoyote ninayoambiwa, na nikiona hata kimoja kwenye fursa hiyo, nakaa nayo mbali sana.
Nitakupa ujanja huo na wewe rafiki yangu, ili uepuke kutapeliwa na wale wanaotumia tamaa za wengine kujinufaisha.
Kabla hatujaangalia vitu hivyo vitano, kwanza nikushirikishe maeneo manne ambayo watu wanadanganywa na kutapeliwa sana.
MAENEO MANNE AMBAYO WATU WENGI WANATAPELIWA SANA.
Kuna maeneo manne ambayo watu wengi wanadanganya na kutapeliwa sana, leo nitakushirikisha kwa ufupi, siku nyingine nitayajadili kwa kina zaidi.
Eneo la kwanza; fedha za kidijitali, au kama zinavyoitwa cryptocurrency au kiongozi wao Bitcoin. Watu wanadanganywa sana na kutapeliwa eneo hili. Unahitaji kuwa makini sana na yeyote anayekuletea fursa inayohusisha eneo hili.
Eneo la pili; biashara ya kubadili fedha za kigeni mtandaoni au kama inavyoitwa FOREX, hii kaa nayo mbali sana, yeyote anayekuambia chochote kuhusu FOREX anataka kukuibia tu fedha zako. Kaa mbali kama unazipenda fedha zako na unaweza kuzitumia kwa mambo ya maana zaidi.
Eneo la tatu; biashara ya mtandao, NETWORK MARKENTING au MULTI LEVEL MARKETING. Hapa kuna utapeli mkubwa sana unaofanyika, kama haupo makini, utapoteza FEDHA, MUDA, NGUVU na hata HESHIMA YAKO kwa wengine.
Eneo la nne; kilimo na ufugaji, zile hadithi za lima matikiti au mapapai au kufunga sungura, kware na viumbe wengine, unapaswa kujipanga kweli kweli, usiingie kichwa kichwa na hesabu za kwenye makaratasi.
Sasa kwa kuwa tumeshaona maeneo manne ambayo wengi wanadanganywa na kutapeliwa, naomba nikushirikishe vitu vitano ambavyo ukiviona kwenye fursa yoyote, kaa mbali.
Huyu Ndiye Tapeli Mkubwa Anayewalaghai Watu Wengi Katika Maisha Yao.
VIASHIRIA VITANO KWAMBA FURSA UNAYOSHIRIKISHWA NI UTAPELI.
MOJA; HAKUNA KUFANYA KAZI.
Ukisikia tu mtu anakuambia kwa fursa fulani unapata mafanikio makubwa bila ya wewe kufanya kazi kabisa, mwambie asante sana na ondoka hapo haraka sana. Ukiona unaambiwa jinsi mafanikio yatakuwa makubwa bila ya wewe kusumbuka na chochote, jua unaelekea kupigwa fedha zako. Kama utaendelea kusikiliza ukijidanganya kwamba labda hiyo iko sahihi, jua umeanza kukolea na kinachofuatia ni kupoteza fedha zako.
Hakuna mafanikio bila kazi, na kadiri mafanikio yanakuwa makubwa, ndivyo kazi inavyokuwa kubwa pia. Anayekuambia hakuna kazi, mkimbie haraka sana.
MBILI; ZIPO HADITHI ZA WALIOFANIKIWA TU, HAKUNA HADITHI ZA WALIOSHINDWA.
Kwenye kila jambo ambalo unaona watu fulani waliofanikiwa, kuna wengi sana ambao wameshindwa. Sasa kama wewe unapewa mifano ya waliofanikiwa tu, na hakuna anayeoneshwa kwamba ameshindwa, kaa mbali, wewe ndiye utakayeshindwa na kushindwa kwako kutawanufaisha watu wengine.
Hakuna eneo lolote la maisha ambalo kila aliyeshiriki amefanikiwa, wengi sana wanashindwa na ukiweza kuwajua, utajifunza mengi zaidi na kwa uhalisia zaidi kuliko kuwaangalia wale tu waliojifunza.
TATU; SAFARI YA MAFANIKIO IMENYOOKA.
Utaweka fedha zako hapa, na kila wiki utakuwa unalipwa faida hii, huhitaji kufanya kingine chochote, na mwisho wa mwaka fedha yako ipo kama ulivyoiweka. Ukiamini kauli kama hiyo, unahitaji kufanyia mazoezi akili yako, maana huenda inapoteza umakini kwenye kufanya maamuzi.
Hakuna safari yoyote ya mafanikio iliyonyooka, hakuna yeyote anayeweza kutabiri kesho nini kitatokea. Ukiona mtu anakuhakikishia kitu cha siku zijazo, jua anaandaa mazingira ya kukutapeli, kaa mbali naye.
SOMA; Je Umewahi Kudanganywa Kujiunga Na Biashara Za Mtandao? Soma Hapa Ili Usidanganywe Tena.
NNE; INABIDI UCHUKUE HARAKA SASA, LA SIVYO UTAKOSA FURSA HII KWA MAISHA YAKO YOTE.
Hakuna kitu chochote ambacho unaweza kukikosa kwa maisha yako yote, isipokuwa tu maisha yako. Hivyo mtu anapokuambia unapaswa kuchukua hatua sasa kwa sababu usipochukua hatua ndiyo inakuwa imetoka na huwezi kupata tena, anakupanga ili akupige fedha zako, kaa mbali sana.
Tena mtu akikuambia inabidi uchukue hatua sasa maana utakosa, mwambie nitachukua hatua mwezi ujao, nitafute baada ya mwezi. Na usibadili msimamo wako kwenye hilo. Usiogope, hakuna chochote kimoja ukikosa kwenye maisha yako basi hutakipata tena. Kama kitu ni sahihi kwako, kitakuja tena na tena na tena, ila kwa njia tofauti.
TANO; KILA MTU ANAKIMBILIA KUFANYA.
Hii ndiyo njia rahisi kabisa ya kugundua utapeli, ukishaona watu wengi wanakimbilia kufanya kitu, wala hata usijisumbue, maana unakwenda kupotea. Unajua watu wengi hawapendi kazi, watu wengi hawana uvumilivu, watu wengi wanapenda njia za mkato, hivyo unapokuta wengi wamejikusanya popote, jua hapo siyo sahihi.
Njia nyingine ya kutumia hili ni kuangalia aina ya mtu anayekuambia kuhusu fursa hiyo, kwa mfano kama mtu mwaka juzi alikuja kwako na kampuni fulani akakuambia hii ndiyo yenyewe, jiunge, au alikuambia ufugaji wa kware ndiyo mpango mzima, mwaka jana akaja na kampuni nyingine, au akaja na sungura. Halafu tena mwaka huu, mtu huyo huyo anakuja kwako na kampuni nyingine anayokuambia hiyo ndiyo supa, au anakuambia ufugaji wa bata ndiyo kila kitu, wala usijisumbue na habari za mtu huyo. Jua tu anataka uingie ili yeye anufaike, maana haiwezekani ndani ya miaka mitatu mtu anakuja na kitu kipwa kwako kila mwaka. Angekuwa anafanya chochote anachokuambia, asingekuwa na muda wa kuja kwako na vitu vipya kila mara.
NYONGEZA; UKIMWELEZA BIBI YAKO HAWEZI KUELEWA UNAPATAJE FAIDA.
Kama unaambiwa ujiunge kwenye biashara au fursa ambayo huwezi kumwelezea bibi yako ambaye hakupata nafasi ya kujifunza mengi, na asielewe, kaa mbali. Na haijalishi inahusisha teknolojia kiasi gani, kama bibi yako mwenye miaka 70 mpaka 80 hawezi kuelewa basi na wewe mwenyewe hujaelewa hivyo upo kwenye mchakato wa kutapeliwa.
Lazima iwe rahisi kwako kuwaelezea wengine unatengenezaje fedha kutoka kwenye fursa hiyo. Kama huwezi kuwaelezea kwa lugha rahisi na inayoeleweka, umetapeliwa.
Rafiki yangu, sipendi wewe utapeliwe, kwa sababu naamini wewe ni mtu mwema, ambaye unakazana kuyaboresha maisha yako zaidi. Sitaki wengine watumie mbinu mbalimbali kukuhadaa. Jifunze haya na chukua hatua ili usitapeliwe.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha