Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya vitu vinavyowatofautisha wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni mtazamo ambao watu hao wanao. Wale wanaofanikiwa wamekuwa na mtazamo wa utele, kwamba dunia ina fursa nyingi sana kwao kuweza kufanikiwa. Hawahitaji kusubiri chochote kije kwao ndiyo wachukue hatua. Badala yake wanatoka na kwenda kuchukua hatua, wanatengeneza fursa zao na kuweza kupiga hatua.
Kwa upande wa pili, wale wanaoshindwa wamekuwa na mtazamo wa uhaba, wanaamini kwamba dunia ina uchache wa fursa, hivyo unapaswa kusubiri mpaka fursa ijitokeze na ikishajitokeza inabidi uchukue hatua haraka sana, la sivyo utaikosa na ukishaikosa haijirudii tena. Wale wanaoamini kwenye haba hawaoni haja ya kwenda kutengeneza fursa zao wenyewe, kwa sababu tayari wanaamini hakuna fursa.
Ni mtazamo upi ulionao katika mitazamo hiyo miwili inategemea na mazingira yanayokuzunguka na yale ambayo umekuwa unajifunza. Kama umezungukwa na wale walioshindwa, moja kwa moja utajikuta unaamini kwenye uhaba na hakuna hatua kubwa utakazoweza kupiga. Lakini kama umezungukwa na waliofanikiwa, utaona jinsi ambavyo wanatengeneza fursa zao wenyewe, na wewe pia utaweza kutengeneza fursa zako.
Bilionea Richard Branson ana kauli maarufu inayosema; fursa ni kama daladala, ukikosa moja, jua kuna nyingine inakuja. Huu ni mtazamo mzuri sana wa kuwa nao kuhusu fursa na mafanikio. Unaondoa ile hali ya uhaba, na inakufanya mara zote uwe tayari kwa sababu fursa ni nyingi.
Kwenye hii dunia, unaweza kutengeneza aina yoyote ya fursa unayotaka wewe. Kwa sababu hii dunia haijawahi kupata mtu wa aina yako. Haijawahi kupata mtu anayefikiri kama wewe, mwenye ndoto kama ulizonazo wewe, mwenye shauku na nguvu ya kupambana kama uliyonayo, mwenye uzoefu ambao wewe umeshaukusanya mpaka kufikia hapo ulipo sasa.
Kama utatumia kila ulichonacho, kama utatumia akili yako vizuri, ukayaangalia mazingira yako, ukawaangalia wale wanaokuzunguka, utaanza kuziona fursa nyingi sana ambazo zinakuzunguka.
Fursa ya kwanza kabisa ni matatizo yako binafsi, kitu gani unataka ambacho upo tayari kufanya chochote kukipata. Ni kitu gani unachohitaji sana, ambacho upo tayari kufanya chochote ili ukipate. Kama hupati kile unachotaka, unaweza kukitengeneza mwenyewe, kisha ukawashirikisha wengine wenye uhitaji kama wako.
Sehemu nyingine nzuri ya kuziona fursa ni kwenye matatizo na mahitaji ya wengine. Kila mtu kuna maumivu anatembea nayo, kila mtu kuna vitu anahitajia ambavyo hawezi kuvipata. Sasa jukumu lako ni kuangalia watu wengi wenye tatizo moja au uhitaji mmoja, kisha angalia unawezaje kuwasaidia watu hao na wao wakamudu kukulipa wewe. angalia elimu uliyonayo, uzoefu ulionao na mazingira yanayokuzunguka, unawezaje kuvitumia kutoa msaada kwa wengine na kuweza kupiga hatua?
Usikae tena na kusubiri fursa zije, au kufikiria kuna uhaba wa fursa. Amka na zifuate fursa, tengeneza fursa zako mwenyewe na kuwa tayari kuweka juhudi sana ili kupata kile unachotaka. Dunia ipo tayari kukupa chochote unachotaka, kama utakuwa tayari kuipa dunia kile inachotaka. Hivyo fursa kubwa ni kujua dunia inataka nini na uipe, kisha yenyewe itabidi ikupe unachotaka.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL