Umewahi kukutana na mtu ambaye anaweza kuuza kitu chochote kwa mtu yeyote. Yaani unaenda mahali, unajiambia kabisa kwamba hutanunua, lakini unakutana na mtu, na kwa jinsi anavyokupokea, kwa jinsi anavyokusikiliza, jinsi anavyokuelezea unachouliza, unajisikia vibaya kutokununua?

Kama umewahi kuwa kwenye hali kama hiyo, basi unajua kwamba ulinunua kitu siyo kwa sababu ulikuwa unahitaji sana kitu hicho, ila kwa sababu umeshawishiwa sana na yule anayekiuza.

Wanasema kabla mtu hajanunua unachouza, anaanza kwanza kukununua wewe muuzaji. Kama upo kwenye hali inayofaa kununulika, yaani kukubalika na kuwa na ushawishi, basi hakuna atakayeacha kununua unachouza.

SOMA; BIASHARA LEO; Tofauti Ya Kuuza Na Kuchuuza…

Hivyo mipango yako yote ya mauzo lazima ihusishe kujiuza wewe mwenyewe kwanza. Hakikisha kitu cha kwanza, kabla hata mteja hajaanza kufikiria kuhusu kile unachouza, kwanza anakubaliana na wewe.

Na njia pekee ya kujiuza kwa wateja wako ni kujua kile unachouza na kujiamini sana. Watu wanasukumwa na wale ambao wako chanya na wanaojiamini kuliko wanavyosukumwa na bidhaa au huduma bora.

Hivyo kama una bidhaa bora sana lakini haupo chanya, hujiamini na huna hamasa kubwa, hutaweza kuwauzia wengi. Lakini kama hata una bidhaa ya kawaida, lakini upo chanya, unajua vizuri, unajiamini na una hamasa kubwa, utaweza kumuuzia yeyote anayeulizia tu bidhaa hiyo.

Hivyo ukiwa na mtazamo bora kabisa kuhusu wewe na kile unachouza, na ukawa na bidhaa au huduma bora, huwezi kukosa wateja. Pia hii ni njia bora sana ya kushindana, kwa sababu hata kama wapo watu ambao wanauza unachouza wewe, hakuna ambaye ni wewe. Hivyo ukiweza kujiuza wewe mwenyewe, hakuna yeyote anayeweza kushindana na wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha