Kuwanasa wateja wa biashara yako ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio ya biashara. Kwa sababu bila ya wateja kunasa, kuwa na kitu wanachokipata kwako tu, hawawezi kurudi tena kwako.

Na kama ambavyo nimekuwa nakuambia, mteja akinunua mara moja kwako, ni hasara kwako. Unaanza kufaidika na mteja pale anaponunua tena na tena na kuwaambia wengine nao waje kununua.

Hivyo lazima uwe na mbinu za kuwafanya wateja wanunue mara kwa mara na pia kuwaambia wengine pia waje wanunue kwako.

Kuwanasa wateja, hakuna tofauti na kuvua samaki kwa kutumia ndoano.

Samaki anapokuwa ndani ya maji, anakuwa na mishemishe zake, anaendelea na maisha yake ya kutafuta chakula na mengine muhimu kwake. Hivyo ukiweka ndoano isiyo na chochote, samaki ataiangalia na kupita, hatajisumbua nayo, kwa sababu anajua siyo chakula.

Lakini unapoweka chambo kwenye ndoano yako, unapoweka chakula kizuri kwa samaki, samaki anavutiwa kwenye chakula kile. Anakisogelea na kuona kweli hichi ni chakula, anavutiwa nacho na kuanza kula. Ni pale anapofungua mdomo na kula chakula ndipo anaponasa kwenye ndoano na anakuwa hana tena uhuru wa kwenda anapotaka yeye.

Hivi ndivyo biashara yako inavyopaswa kuwa. Kama upo tu kama zilivyo biashara nyingine, wateja watakupita tu, maana hakuna cha kuwafanya waje kwako. Lakini unapokuwa na kitu cha kukutofautisha na biashara nyingine, mteja anapata ushawishi wa kuja kujaribu kile unachouza. Na hapo ndipo unapaswa kumnasisha mteja, kuhakikisha haendi pengine ila kuja kwako tu.

SOMA; BIASHARA LEO; Cross-Selling Na Up-Selling, Mbinu Mbili Za Kuongeza Mauzo Bila Kuongeza Wateja.

Tofauti ya wateja wako na kuvua samaki ni kwamba wateja wako unawanasisha kwa vitu vizuri kwao na vinavyoyafanya maisha yao kuwa bora na siyo tu kwa manufaa binafsi kwako.

Mara zote kuwa na kitu cha tofauti kwenye biashara yako, kitakachokufanya wewe uonekane zaidi ya wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara unayofanya. Na kitu hicho ndiyo kitakachokuwezesha kuwanasa wateja kwako.

Angalia mfano wa makampuni ya simu, ambayo ukinunua simu au kadi yao ya simu unapewa dakika nyingi za bure. Wanachofanya ni kukuweka kwenye hali ya mawasiliano, na dakika za bure zinapoisha, itabidi uanze kununua vocha ili uendelee kuwasiliana. Unaweza kujiambia unanufaika sana na mawasiliano ya bure unayopewa, lakini ile ni chambo, ukishazoea kuwasiliana na watu, utahitaji kuendelea, na hapo ndipo utakapoendelea kununua zaidi na zaidi kutoka kwenye kampuni hiyo.

Hakikisha biashara yako inakuwa na chambo inayowavutia na kuwanasisha wateja kwenye biashara hiyo. Inaweza kuwa nafasi ya mteja kujaribu kile unachouza kabla ya kulipia, au hata nafasi ya kurudisha chochote anachonunua kama hajaridhika nacho au hakijamfaa. Inaweza pia ikawa nunua moja pewa moja, au zawadi kwa manunuzi ya kiwango fulani.

Angalia chochote unachoweza kufanya mteja anaponunua mara ya kwanza kwako, ambapo utamfanya aendelee kununua tena na tena na tena.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha