Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa siyo ndoto kubwa wanazokuwa nazo, na wala siyo kiwango cha kazi ambacho wapo tayari kuchukua. Bali jinsi ambavyo wanachukulia changamoto.

Wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote wanakuwa na ndoto kubwa kwenye maisha yao. Na wote wanakuwa tayari kuweka kazi ili kufikia ndoto hizo.

Lakini kama wote tunavyojua, hakuna safari ya mafanikio iliyonyooka. Muda mfupi baada ya kuanza, kila mtu huanza kukutana na changamoto mbalimbali. Zinaanza changamoto ndogo, unazitatua ukijua umemalizana na kila kitu, mara zinakuja changamoto kubwa zaidi.

Kila unapotatua changamoto moja na kujiambia sasa unapata nafasi ya kukuza ziadi, inajitokeza changamoto nyingine.

Wale wanaoshindwa wanaona kwa changamoto nyingi wanazokutana nazo, ni bora waache maana hakuna wanakoweza kwenda. Hivyo wanaacha wanachofanya na kwenda kujaribu kitu kingine, ambapo huko pia wanakutana na changamoto.

Kwa upande wa pili, wale wanaofanikiwa wanajua changamoto ni sehemu ya safari ya mafanikio, na wanajua popote wanapokwenda watakutana na changamoto. Hivyo hawakubali changamoto ziwe sababu ya wao kuacha, bali wanazifanya changamoto kuwa kichocheo kwao kupiga hatua zaidi.

Ili kufikia malengo yoyote uliyojiwekea kwenye maisha yako, lazima ufike kwenye hatua ambayo kila changamoto unayokutana nayo inakuwa kichocheo cha wewe kufanikiwa zaidi. Unazikaribisha changamoto na kujua hiyo ndiyo njia ya wewe kukua zaidi.

Maisha yanaweza kuwa magumu sana na yenye ukatili ndani yake, unaweza kukutana na changamoto mpaka ukajiuliza hivi mbona ni mimi tu. Sasa badala ya kuona hilo kama bahati mbaya au kisirani, ona kama ni fursa kwako kufanikiwa zaidi. Maana unapokutana na changamoto zaidi, ndivyo unavyokuwa imara zaidi.

Ili kufanikiwa, lazima uchukulie changamoto kama kichocheo kwako kupiga hatua zaidi. Lazima uzikaribishe changamoto na kuzitumia kupiga hatua zaidi. Usikimbie changamoto yoyote ile kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha