Rafiki yangu mpendwa,
Wapo watu huwa wanatafuta wachawi wanaowazuia wasifanikiwe. Kama wewe ni mmoja wa watu hao, na siyo lazima tu uwaite wachawi, unaweza kuwa unaamini wapo watu wanaokuzuia kufanikiwa ndiyo maana upo hapo muda wote, hupigi hatua, nina habari njema kwako. Ni kweli kabisa kwamba kuna mtu mmoja anayekuzuia wewe usifanikiwe. Na ipo njia moja tu ya kumwona mtu huyo, nenda kasimame mbele ya kioo, na utakayemuona mbele yako ndiyo adui yako namba moja kwenye mafanikio yako.
Rafiki, siku siyo nyingi kuna rafiki yangu mmoja aliniona nikiwa na kitabu kipya cha Dr Reginald Mengi kinachoitwa I CAN, I MUST, I WILL. Rafiki huyo aliniomba akiangalie kitabu, na akakiperuzi kwa haraka, kuangalia yaliyomo, na pia kuangalia picha mbalimbali za Dr Mengi ambazo ameziweka kwenye kitabu chake hicho. Rafiki huyu alipata hamasa kubwa sana akasema inaonekana ni kitabu kizuri sana. Nikamwambia ni kweli ni kitabu kizuri sana, na napendekeza kila Mtanzania akisome.
Rafiki yule akaniambia basi naomba uniazime nikisome utakapomaliza kusoma. Nikamwambia utaratibu wa kuwaazima watu vitabu nilishaacha zamani, maana kila niliyewahi kumwazima kitabu, kwanza hakukisoma na pili, sikupata tena kitabu changu. Nikamwambia kitabu nimekinunua elfu 40 na nikamwelekeza duka. Akaniambia kwa sasa hatakuwa na bajeti hiyo mpaka mwisho wa mwezi. Nikamwambia basi hakuna shida, ila nikamwambia naweza kukununulia kitabu halafu mwisho wa mwezi ukifika unilipe hiyo fedha, akasema nisijali, atanunua mwisho wa mwezi ukifika.
Mwisho wa mwezi ulipofika, nilimwuliza rafiki yule kama tayari amekinunua kitabu, akaniambia bado, mambo yameingiliana. Basi niliachana naye na nilijifunza kitu kimoja kikubwa sana. Kuna watu wanachagua kubaki pale walipo halafu watawalalamikia wengine ndiyo sababu.
Rafiki, watu wengi hawapo tayari kutoa fedha kununua maarifa. Wengi wanaona maarifa yanapaswa kuwa bure na hata yakiwa bure bado watajiambia hawana muda wa kupata maarifa hayo.
Ninachokuambia rafiki yangu ni hiki, kama haupo tayari kutoa fedha yako kununua maarifa, unajizuia wewe mwenyewe kufanikiwa. Unajiwekea vikwazo wewe mwenyewe usifanikiwe na hilo litakugharimu sana maisha yako.
Na haijalishi unapaswa kulipa kidogo au kikubwa kiasi gani, lazima uwe tayari kulipia maarifa, lazima uwe tayari kununua vitabu, kulipia na kushiriki semina mbalimbali, kujiandikisha kwenye kozi mbalimbali hata kama hutazitumia kuomba kazi.
Hivi ni vitu vitakavyokufanya wewe kuwa bora zaidi, vitakavyokuwezesha kufanya kile unachofanya kwa ubora zaidi na hivyo kuongeza zaidi thamani yako hapa duniani.
Unapaswa kuwa tayari kulipia vitu hivi rafiki yangu.
Na hakuna mtu ambaye hawezi kulipia vitu hivi. Nasema hivi nikijiamini kabisa kwa sababu sijawahi kukutana na mtu anayetembea uchi kwa sababu hana fedha ya kununua nguo. Pia sijawahi kusikia kuna mtu amekufa njaa kwa sababu amekosa kabisa fedha ya kununua chakula. Inapokuja kwenye yale muhimu kwenye maisha yetu, huwa tunapambana mpaka tone la mwisho ili kuvaa, ili kula na ili kulala.
Sasa kwenye mahitaji hayo matatu ya msingi, ongeza hitaji moja ambalo ni kujifunza, hakikisha kabla hujanunua chochote basi unanunua maarifa. Kabla hujanunua nguo mpya, basi nunua maarifa.
Ni jambo la kushangaza sana watu watatumia fedha nyingi kununua nguo za kuficha miili, lakini hawapo tayari kutoa fedha kununua maarifa ambayo yatawawezesha kuficha akili zao. Wanavaa nguo nzuri zinazositiri miili yao, lakini kiakili wanatembea uchi, akili inakuwa wazi na isiyotumiwa vizuri.
Nisisitize rafiki, kama una fedha ya kununua nguo na chakula, una fedha ya kununua maarifa. Kama una muda wa kula kila siku, unao muda wa kutosha kujifunza kila siku.
Kuwa tayari kununua maarifa rafiki, vitu vyote vyenye thamani kubwa kwenye maisha yetu vinakuja na gharama zake. Unahitaji kulipia fedha na pia kujitoa kuweka juhudi ili kile unachojifunza kiwe na manufaa kwenye maisha yako.
Ili kuhakikisha unakuwa na kiasi cha kutosha cha fedha cha kununua maarifa, sehemu ya kipato chako inapaswa kuingia kwenye fungu la kujiendeleza kimaarifa. Kama unaweza, anza na asilimia 10 ya kipato chako, kama haiwezekani basi anza na asilimia 3. Kwenye kipato chako cha siku, wiki, mwezi au hata mwaka, asilimia 10 au 3 kwa wale waliobanwa sana, inapaswa kurudi kwenye maarifa.
Hii ina maana kwamba, kama kipato chako kwa mwezi ni shilingi milioni moja, basi laki moja inapaswa kuwa fungu la kujifunza. Kama laki moja itakuwa kubwa kwako, basi angalau elfu 30 iwe ndiyo fungu la wewe kujifunza zaidi. Hivyo kila mwezi, hakikisha unanunua maarifa kutoka kwenye fungu la kujifunza ulilojitengea.
Nikutakie kila la kheri rafiki yangu, katika kununua maarifa na kujifunza zaidi.
Kwa kumalizia, nikushauri haya muhimu;
- Nunua kitabu cha Dr Mengi, kinapatikana HOUSE OF WISDOM BOOKSHOP DAR, wasiliana nao kwa namba; 0759 349 954
- Nunua vitabu mbalimbali ninavyouza mimi, unaweza kutembelea hapa kuvipata; amkamtanzania.com/vitabu
- Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA na huduma nyingine za ukocha ninazotoa, fungua hapa kupata maelekezo zaidi; amkamtanzania.com/kocha
- Karibu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, fungua hapa kupata taarifa zaidi; https://amkamtanzania.com/2018/07/13/karibu-kwenye-semina-ya-kisima-cha-maarifa-2018-mafanikio-biashara-na-uhuru-wa-kifedha/
Kila la kheri rafiki yangu, uwe na safari bora kabisa ya kujifunza na kuwa bora zaidi kila siku.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha