Kitu kimoja nakiona kwenye biashara za wengi ni kwamba, wengi hawaheshimu biashara zao. Mtu anapokuwa ameajiriwa ataheshimu sana ajira yake. Atawahi kufika kazini na ataondoka pale muda wa kutoka unapofika. Hatajipangia tu safari zisizohusiana na kazi kama anavyotaka mwenyewe. Na hata jamii itamheshimu, haitamtegemea aamue tu chochote, kwa sababu kila mtu anajua ameajiriwa na inabidi apate ruhusa ili kufanya chochote.
Matatizo yapo upande wa pili, kwa wale waliojiajiri na wanaofanya biashara. Kwa kuwa mtu anamiliki biashara yake mwenyewe, basi anajiachia sana. Anaamua afungue biashara saa ngapi, anaweza kuamua siku fulani asifungue kabisa. Akipata safari yoyote hata isiyohusiana na biashara anaenda. Na hata jamii inayomzunguka, inategemea apatikane muda wowote, bila ya ruhusa yoyote.
Rafiki yangu, nataka ujipime kwenye biashara yako au ajira yako binafsi kwa namna moja. Angalia mtu ambaye unamjua ameajiriwa kwenye sekta binafsi na analipwa mshahara mkubwa kuliko wengine. Halafu angalia jinsi kazi yake hiyo inavyotumia muda wake na maisha yako. Halafu endesha biashara yako kama vile umeajiriwa kwenye nafasi ya yule unayemwangalia.
Kuwa na muda ambao utafungua biashara yako kila siku bila ya kuchelewa na kuwa na muda utakaofunga, bila ya kuwahi kabla ya muda huo siku yoyote. Usikubali chochote kinachotokea kipelekee wewe kufunga biashara yako. Usijiachie tu na kwenda kila safari inayojitokeza mbele yako, wewe umeajiriwa pia, na ubaya ni kwamba huna ruhusa kabisa ya kutoka kwenye biashara yako.
Najua utakuwa unajiambia sasa lengo la kuanzisha biashara ni nini? Si nilianzisha ili niwe huru, nichague jinsi ya kuendesha maisha yangu nitakavyo? Ni kweli kabisa, hilo ndiyo lengo la wewe kuwa kwenye biashara. Lakini kama biashara haijaweza kukuingizia kipato kikubwa, na hujaweza kutengeneza mfumo wa biashara kujiendesha mwenyewe, huna uhuru wowote.
Na kama kwenye biashara yako umeajiri watu, basi hakikisha wewe unafanya kazi kuliko yeyote uliyemwajiri kwenye biashara hiyo. maana changamoto nyingine imekuwa ni watu wanapoajiri wanafikiri ni nafasi yao kutokufanya kazi. Sasa ukiendesha biashara yako hivyo, wafanyakazi wako watajifunza kwamba kazi siyo muhimu sana. Lakini pale wewe unapofanya kazi zaidi ya wale uliowaajiri, watakuwa hawana budi bali kufanya kazi.
Hata kama biashara ni yako, usijiachie sana na kuamua kufanya kila unachotaka. Jichukulie kama umeajiriwa kwenye ajira inayokubana sana, na endesha biashara yako kwa namna hiyo. Utapiga hatua sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,