Rafiki yangu mpendwa,

Miaka kadhaa iliyopita nilijipa jukumu moja kubwa sana la maisha yangu. Jukumu hilo limekuwa kwamba kila ninayekutana naye iwe ana kwa ana au kupitia kazi zangu basi asibaki kama alivyokuwa.

Yaani kukutana kwangu na mtu kuache alama chanya, ambayo miaka mingi ijayo akiangalia nyuma, anajiambia nilikuwa pale, nikakutana na huyu na sasa maisha yangu yamefika hapa.

Na sikujipa jukumu hili kwa sababu nilitaka kupata sifa kutoka kwa wengine, bali nilijipa jukumu hili baada ya kujifunza kupitia falsafa na imani kwamba uwepo wetu hapa duniani unapaswa kuwa na maana fulani.

Hivyo kila siku, yaani kila siku, iwe najisikia au sijisikii nimekuwa nakuandikia makala na kukushirikisha kwenye mitandao mikuu miwili ninayoiendesha ambayo ni AMKA MTANZANIA, www.amkamtanzania.com na KISIMA CHA MAARIFA, www.kisimachamaarifa.co.tz

Ni kazi ambayo kwa nje inaweza kuonekana rahisi sana, lakini pale unapoifanya kila siku, ndipo unajua siyo rahisi kama unavyoweza kufikiri. Ni kazi inayohitaji kujitoa hasa, kuondokana na sababu za kila aina na kukaa chini kisha kufanya kazi.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Sasa nimekuwa naandika sana, na naona wapo watu wengi kama hawawezi kwenda na kasi ya uandishi au wanaona hawana muda wa kusoma kila ninachoandika. Hivyo napenda niwasaidie kitu kimoja ili kama hawatasoma chochote ninachoandika, basi watajua wapi nasimama na wapi wanapaswa kusimama pia.

Ujumbe mkuu wa kazi zote ninazofanya upo nyuma ya neno hili moja; KAZI.

Nahubiri kitu kimoja; KUFANYA KAZI.

Ninachokuambia tena na tena na nitaendelea kukuambia kwenye kila ninachokushirikisha ni IFANYE KAZI.

Penda sana KAZI UNAYOIFANYA.

Ifanye kwa viwango vya kipekee, viwango vya juu sana.

Kwenye kila unachogusa na mikono yako, hakikisha unaacha alama yako.

Hakikisha ukifanya kazi yako, hata kama haupo, mtu akija anasema kazi hii imefanywa na fulani, kwa sababu watu wanajua aina ya kazi unazofanya.

Fanya kazi sana, na dunia haitakuwa na budi bali kukulipa sawasawa na kazi unayofanya.

SOMA; Mambo 40 Kuelekea Miaka 40 Ya Maisha Yangu (Na Vitabu Vitano Muhimu Unavyopaswa Kusoma Kwenye Maisha Yako).

Kama unatafuta njia ya mkato ya kufanikiwa, ambayo haihusishi kazi, nasikitika kukuambia kwamba umepotea njia, na unapaswa kuacha mara moja kufuatilia mafunzo ninayotoa.

Kama unatafuta mafanikio ya ghafla, ya kulala masikini na kuamka tajiri, unapoteza muda wako hapa.

Napenda sana kazi rafiki, na kama wewe ni rafiki yangu ambaye upo hapa, penda sana kazi. Na kazi itakulipa, kama utaifanya kwa namna ambayo hakuna mwingine awezaye kufanya.

Ni hilo nimependa kukushirikisha wewe rafiki yangu. Hivyo kama hutapata muda wa kusoma mafunzo yote ninayotoa, basi jua ujumbe mkuu ni kazi, WEKA KAZI, JITOE KWA AJILI YA KAZI, IPENDE KAZI na WEKA ALAMA YAKO KWENYE KAZI UNAYOFANYA.

Mwisho kabisa, kwa kuwa kazi inachosha, na wakati mwingine utakatishwa tamaa, unahitaji na kuwa na kitu cha kukuchochea zaidi pale unapokutana na magumu. Na mimi nipo kwa ajili ya hilo.

Kila unapokutana na kikwazo, kila unapokaribia kukata tamaa, ingia kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, tafuta makala chache za kusoma kuhusu KAZI, kisha rudi tena kwenye kazi yako, ukiwa na hamasa kubwa zaidi ya kwenda kushinda na KUTAWALA.

Naahidi kuendelea kukupa maarifa bora kabisa rafiki yangu, maarifa yatakayokuwezesha kuifanya kazi bila ya kuchoka wala kukata tamaa.

Kila la kheri.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha