Moja ya vitu vinavyofanya tupoteze muda kwenye maisha yetu, ni wingi wa muda na siku ambazo tunafikiri tunazo.

Kila ninapokuwa nafikiria muda, huwa kauli ya Seneca inanijia kwenye akili yangu. Seneca anasema, tatizo la muda siyo kwamba hatuna wa kutosha, bali tunao mwingi kiasi kwamba tunaamua kuupoteza.

Hivi unafikiri kwa nini unajiambia kitu fulani utafanya kesho? Kwa sababu kwenye akili yako umejiaminisha kwamba kesho itakuwepo na mambo hayakuwa mazuri kesho kuliko yalivyo leo. Na hapo ndipo tunapoanza kujidanganya sana.

Vipi kama kesho haitakuwepo? Vipi kama kesho mambo yatakuwa magumu zaidi? Vipi kama kesho hutapata nafasi uliyoipata leo? Na muhimu zaidi, vipi kama leo ndiyo siku pekee ambayo unaweza kufanya hicho, na ikipita hutaweza kupata tena siku nyingine?

Chukua mfano una orodha ya wateja 100 unataka kuwasiliana nao leo, lakini huwasiliani nao na kadiri muda unavyokwenda, unajiambia utafanya kesho. Sasa chukulia mfano, kuna mtu amekuja kwako, na orodha ya wateja 100 na kukuambia wateja hawa wapo tayari kununua, kama utawasiliana nao siku ya leo tu, baada ya leo kuisha hata usijisumbue kuwatafuta. Ni hatua gani utachukua? Je utapoteza muda? Je utajiambia utafanya kesho?

Nafikiri unaona jinsi gani siku ikiwa ndiyo siku yenyewe, utajisukuma kwa namna yoyote ile kufanya kile unachopaswa kufanya.

Hivyo kwa chochote muhimu unachotaka kufanya, pale unapoanza kufikiria kwamba utafanya kesho, hebu jistue hapo ulipo na jiambie vipi kama leo ingekuwa ndiyo siku pekee ya kufanya? Na ukweli ni kwamba, mambo mengi unayojiambia utafanya kesho, ni bora kama ungeyafanya tu leo. Maana kesho hazijawahi kutabirika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha