Rafiki yangu mpendwa,

Najua mpaka sasa umeshakutana na njia nyingi sana ambazo umeambiwa ndiyo njia sahihi kwako kufanikiwa. Unaweza kuwa umekutana na njia nyingi sana na zinazokinzana kiasi kwamba umebaki njia panda.

Wapo wanaokuambia fanya kazi sana ili kufanikiwa, wakati wengine wanakuambia tumia akili na siyo nguvu ili kufanikiwa. Wapo wanaokuambia kuna biashara fulani ambayo ukiingia hiyo basi mafanikio nje nje.

Rafiki, kwa jinsi ninavyokupenda na kukueleza ule ukweli unaopaswa kujua, nakuambia hili, hakuna njia moja ya mafanikio ambayo kila mtu akipita atafanikiwa.

Kwa hakika, alichofanya mwingine akafanikiwa sana, unaweza kufanya wewe na ukashindwa. Mafanikio yanategemea zaidi na mtu husika kuliko kwenye kanuni au kile ambacho kila mtu anafanya.

Lakini kama ipo njia moja pekee ya wewe kufanikiwa sana kwenye maisha yako, basi njia hiyo itakuwa ni kukosea. Ndiyo, kama unataka kufanikiwa sana kwenye maisha yako, basi unahitaji kukosea sana. Unahitaji kufanya tofauti na vile ambavyo wengi wanategemea ufanye.

Na siyo unafanya hivyo kwa sababu unataka kuwakomoa, bali unafanya hivyo kwa sababu ndiyo kitu muhimu kwako kufanya, ndiyo namna unavyoweza kufanya na ndiyo njia pekee kwako kufanya kile chenye maana.

Watu wengi wanakazana kukushauri na kukuelekeza uwe kama watu wengine, uache kuwa wewe na uwe kama wengine, kitu ambacho kamwe hakitakupa mafanikio makubwa.

MIMI NI MSHINDI

Hutafanikiwa kwa kuwa mtu mwingine yeyote, bali utafanikiwa kwa kuwa wewe. Hivyo kama kuna hitaji kubwa na la kwanza unalohitaji ili kufanikiwa ni kujijua kwanza wewe mwenyewe. Kujua kipi kinachokusukuma wewe, kipi kinakufanya upate hamasa kubwa. Na kipi ambacho kwa wengine wanaona ni kazi, lakini kwako ni sehemu ya maisha?

Jijue wewe mwenyewe, jua kile ambacho unakitaka hasa, jua mtindo wako na kazana kukuza vitu hivyo kila siku, kwa sababu hivyo ndiyo vitakupeleka kwenye mafanikio makubwa.

Kwa kufanya hivi, watu watakuambia unakosea sana, kwa sababu wao wanaona kwa nje na hawaoni kwa ndani. Wanataka kukuweka kwenye kundi fulani wakati wewe huna kundi, wewe ni wewe na unachofanya hakipaswi kufanana na yeyote yule.

Unapochagua safari ya mafanikio kwenye maisha, kitu kimoja unachopaswa kuondokana nacho ni kujaribu kumridhisha kila mtu. Ukishajiona unafanya vitu ili wengine wafurahi, au waone unafanya, jua umeshaingia njia ambayo siyo sahihi kwako.

SOMA; Hizi Ni Sababu Kwa Nini Baadhi Ya Watu Wanaopata Fedha Nyingi Huishia Kufa Masikini, Na Hatua Za Wewe Kuchukua.

Usiogope kupita njia yako mwenyewe, kama wanavyosema kwenye imani, kwamba kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe, basi pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio, kila mtu atapita njia yake mwenyewe, kila mtu atakutana na mateso yake mwenyewe.

Na hakuna ubaya pale unapoanza ukiamua kuchagua mtu mmoja ambaye utayaiga maisha yake kwa mwanzoni. Kwa sababu mwanzoni unaweza usijue kipi cha kufanya na kipi cha kuepuka. Hapo ndipo unapohitaji kuwa na mtu wa mfano kwako, mtu anayekuhamasisha na unayetaka kufika ngazi ambazo yeye amefika.

Lakini kuna wakati ambapo utahitaji kuacha kumuiga mtu huyo na kuwa wewe, kuna kiwango cha mafanikio utafikia ambapo hutaweza kwenda juu zaidi ya hapo kama hutaacha kumfuata mtu huyo na kuwa wewe.

Nakushirikisha hili muhimu sana kwako rafiki yangu ili uache kupoteza maisha yako kukimbizana na vitu ambavyo havitakuwa na msaada kwako.

Wakati mwingine ni bora kuchagua njia moja ambayo siyo sahihi sana, lakini ukaweka nguvu zako zote kufika kule unakotaka, kuliko ukakazana na njia unazoona ni sahihi nyingi na usichukue hatua kubwa kwenye njia yoyote kati ya zile ulizochagua.

Chagua kuishi mafanikio rafiki yangu, chagua njia ambayo itakupeleka kwenye kuwa wewe, njia itakayokuwezesha kufika unakotaka kufika, hata kama ni njia ambayo hakuna mwingine anapita. Kama ni kitu unajali, na kama upo tayari kuweka kazi ya kutosha, endelea kuweka. Mwisho wa siku dunia inalipa kazi na thamani na siyo kipi sahihi au siyo sahihi. Toa thamani kubwa kwa watu na dunia itakuwa na wajibu wa kukulipa kulingana na thamani unayotoa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha