Watu wamekuwa wanatoa sababu mbalimbali kwa nini biashara zao zimeshindwa.
Na unapowasikiliza, utawasikia wakisema mambo ya nje tu. Kwamba uchumi mgumu, kwamba watu hawana fedha, kwamba ushindani umekuwa mkali na mengine kama hayo.
Hutawasikia wakisema mambo ya ndani, ambayo ndiyo sababu kuu ya kufa kwa biashara. Mambo kama uzembe, uvivu, kukosa umakini, kukosa ubunifu na mengine ya aina hiyo, huwa ndiyo yanaanzisha kifo cha biashara. Yale ya nje yanamalizia tu kifo.
Sasa kuna kitu kimoja kinateketeza sana biashara za wengi, lakini wengi hawakijui na hivyo kinazidi kuwa hatari.
Kitu hicho ni AHADI ZISIZOTIMIZWA. Kama unawaahidi wateja wako kitu fulani, halafu wakaja na wasikipate, wateja wanapoteza imani na wewe. wanakuchukulia kama mtu mwongo na usiye mwaminifu. Sasa mteja akishakuchukulia hivi, jua kumshawishi tena ni vigumu sana.
Usijaribu kuahidi kitu ambacho unajua kabisa huwezi kukitimiza. Ni bora umwambie mteja ukweli umpoteze, kuliko kumwambia uongo, halafu aje kujua ukweli.
Kwa sababu ukimwambia mteja ukweli na akaondoka, hatakusema vibaya kwa wengine. Lakini unapomwambia uongo na baadaye akajua ukweli, atamwambia kila anayemjua awe makini na wewe, kwa sababu huwa unaahidi vitu vya uongo.
Fanya biashara kwa kuangalia miaka mingi ijayo, kama kitu huna uhakika nacho, ni bora umweleze mteja ukweli kuliko kumhakikishia kitu usichojua halafu kikamgharimu yeye.
Mara zote ahidi unachoweza kutekeleza, na umia uwezavyo lakini tekeleza kile ulichoahidi. Usiue biashara yako kwa ahadi usizoweza kutekeleza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,